Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Vyuma nane Yanga, faili la Injinia lina balaa!

Kambole Pic Data Vyuma nane Yanga, faili la Injinia lina balaa!

Wed, 16 Jun 2021 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

FAILI la bosi wa Yanga, Injinia Hersi Said lina sapraizi kibao kwa mashabiki wa klabu hiyo. Kocha Nesreddine Nabi amempa majina nane ambayo anayataka kwenye ripoti yake.

Tafsiri ya ripoti hiyo ni kwamba kuna uwezekano mkubwa kwenye kikosi cha kwanza cha Yanga msimu ujao kikawa na sura tatu za zamani na wengine wote nane wapya.

Nabi hajaridhika na ubora wa kikosi hicho na amependekeza kufumua sehemu kubwa kwenye ripoti yake ingawa vigogo wa Yanga wameamua kufanya majina hayo siri kubwa.

Mwenyekiti wa Kamati ya ufundi ya Yanga, Dominic Albinus ameliambia Mwanaspoti kwamba ripoti ya kocha Nabi waliyoipokea imetaka kufumulia ka idara tatu ambazo ni ulinzi akigusa maeneo yote kuanzia kwa makipa na mabeki wake.

“Kwanza nifafanue kwamba wako wanaodhani ni kama Hersi anakwenda kujisajilia anachotaka yeye hii sio sahihi Hersi anafanyia kazi yale tuliyojadiliana na makocha na sisi kama uongozi kupitisha,” alisema Albinus.

“Kocha ametaka mfano safu ya ulinzi nzima itaguswa yaani zile nafasi zote nne kule nyuma,” alisema Albinus.

Yanga tayari imeshamalizana na beki Djuma Shaban wa AS Vita akija kama beki wa kulia kuja kupambana na Kibwana Shomari aliyecheza mechi nyingi msimu huu.

Mbali na Djuma pia Mwanaspoti linajua, Yanga inamalizana na beki wa kushoto wa KMC, Bryson David lakini pia wakitafuta kwa siri beki wa maana wa kati ambaye kama atapatikana kuna uwezekano wakaachana na nahodha wao Lamine Moro ambaye kwenye siku za karibuni amechafuka kinidhamu.

Pia Mwanaspoti limedokezwa kunaweza kufanyika mabadiliko katika eneo la golikipa hasa kutokana na Ramadhan Kabwili kutaka kuondoka akapate muda wa kucheza zaidi huku pia Metacha Mnata ikielezwa anataka kuondoka.

Albinus ambaye pia kitaaluma ni kocha wa soka aliongeza kwamba eneo lingine ambalo Nabi anataka kutafutiwa watu imara ni kiungo mchezeshaji pamoja na winga mmoja mwenye makali.

“Kocha anataka tumletee kiungo mchezeshaji anayejua kazi yake na mwenye ubora wa sasa aliowaona hapa hajaridhika nao lakini pia anataka winga mmoja mzuri mwenye kasi na anayejua kutengeneza nafasi za mabao,” alisema.

Mwanaspoti linafahamu Yanga inakaribia kumalizana na kiungo Mercey Vumbi Ngimbi ambaye ni nahodha wa Union Maniema iliyomaliza nafasi ya tatu katika Ligi Kuu nchini DR Congo akiwa pia katika timu ya taifa.

Hesabu za usajili wa winga mzawa, akili ya mabosi wa Yanga zipo kwa Dickson Ambundo wa Dodoma Jiji ambaye mazungumzo yao bado hayajakamilika lakini yapo kwenye hatua nzuri.

Aliongeza kwamba eneo la mwisho ambalo Nabi ametaka umakini ni usajili wa washambuliaji wa kati wa wawili wenye makali ya kutupia kuchukua nafasi za Michael Sarpong na Fiston Abdul ambao wanaweza wasishuhudie hata bingwa wa msimu huu akiinua ndoo.

Hersi bado kaganda nchini Afrika Kusini akisaka saini ya mshambuliaji Lazarous Kambole ambaye watamchukua kwa mkopo wa msimu mmoja huku bado wakivutana juu ya maslahi binafsi ya mchezaji haswa mshahara.

Bado Yanga inaumiza kichwa ni mshambuliaji yupi wa pili wamalizane naye atakayeweza kuungana na Kambole endapo wakimalizana na Kaizer Chief.

Albinus alisema aina ya usajili wanaoufanya sasa sio tena wa kuunda kikosi bali kukamilisha kikosi imara kitakachoshusha mataji kwa msimu ujao kwa kuwa kazi ya kuunda timu ilishaanza huko nyuma.

“Kwasasa tutakwenda kumalizana na watu wa maana kimyakimya na mwisho tutawatangazia wanachama na mashabiki wetu,niseme tu awamu hii tukisema tunamtaka fulani basi mjue tutampata, tutafanikiwa,” aliongeza Albinus na kuwataka mashabiki wa klabu hiyo kutulia wakati huu wakifanya yao. Yanga wanapambana kusuka kikosi kipya baada ya kutoridhishwa na kile cha msimu huu ambacho hakijawafurahisha.

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz