Berlin, Ujerumani. Mwanariadha Volha Mazuronak wa Belarus, jana alitwaa medali ya dhahabu katika mbio za marathon za ubingwa wa Ulaya 2018, kwa wanawake licha ya kukumbwa na kadhia ya kutokwa na damu puani.
Mwanariadha huyo mwenye miaka, 29, aliwapita kidogo Clemence Calvin wa Ufaransa na Eva Vrabcova Nyvltova wa Jamhuri ya Czech.
Mazuronak alitwaa ushindi baada ya kutumia saa 2:26.22 na mwanariadha huyo hakukata tamaa hata kidogo licha ya kujikuta akitokwa na damu nyingi puani dakika za mwanzo.
Baada ya damu kuzidi kutoka mwanariadha huyo alipunguza kasi kwa mwendo wa karibu maili moja na alipomaliza mbio hizo alipongezwa sana na waratibu.
Mwanariadha anayeshikilia rekodi ya Dunia katika mbio za Marathon, Paula Radcliffe, alimmwagia sifa sana Mazuronak, kwa kichendo cha kumaliza mbio hizo licha ya kutokwa na damu nyingi.
“Kwa hakika Volha Mazuronak anastahili pongezi sana sio kwa sababu ya ushindi alioupata bali kwa ustahimilivu aliouonyesha katika mbio hizo,” alisema Radcliffe.
Nyota namba moja kwa Uingereza, Tracy Barlow, alimaliza katika nafasi ya 15, wakati kwa wanaume, Koen Naert wa Ubelgiji alishinda kwa wanaume akiandika muda bora was aa 2: 9.51 na Tadesse Abraham muethiopia aliyechukua uraia wa Uswisi, alishika nafsi ya pili huku Yassine Rachik wa Italia akishika nafasi ya tatu.