Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Vodacom yashusha presha klabu Ligi Kuu

12209 VODA+PIC TanzaniaWeb

Thu, 16 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Yasisitiza hawajajitoa, mazungumzo yanaendelea na majibu kamili yatatolewa mambo yakikamilika.

Dar es Salaam. Siku moja baada ya Bodi ya Ligi kutangaza Ligi Kuu Bara kuanza bila mdhamini na kutaka timu zijitegemee, waliokuwa wadhamini wa ligi hiyo, Kampuni ya Simu za Mkononi ya Vodacom imeshusha presha timu na kusema watulie kwanza.

Hatua hiyo imekuja baada ya Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi (TPLB), Boniface Wambura, kusisitiza kuwa Ligi Kuu msimu huu itaanza bila kuwa na mdhamini mkuu kwa sababu hawajafikia makubaliano na kampuni yoyote.

Kwa miaka saba sasa, Kampuni ya Vodacom imekuwa ikidhamini ligi hiyo na msimu huu imeelezwa kuwa hawajafikia makubaliano na TFF kudhamini ligi hiyo ambayo msimu ujao itakuwa na timu 20 badala ya 16 za awali.

Vodacom wanena

Baada ya taharuki iliyozikumba baadhi ya klabu, gazeti hili jana lilimtafuta Mkuu wa Kitengo cha Masoko na Mawasiliano, Vodacom Tanzania, Nandi Mwiyombella ambaye alisema hawajajitoa rasmi, kwa kuwa mazungumzo bado yanaendelea.

“Vodacom Tanzania, tumejizatiti katika kukuza vipaji vya vijana wa Tanzania, hili tumekuwa tukilifanya kupitia programu zetu mbalimbali za michezo, hii ni pamoja na kudhamini Ligi Kuu ambayo tumeidhamini kwa zaidi ya miaka saba sasa.

“Udhamini huu utaendelea na kwa sasa tunaendelea na majadiliano kati yetu na TFF, mazungumzo yakikamilika tutakuja na jibu sahihi. Ahsante,” alisema Nandi alipowasiliana na Mwananchi moja kwa moja kufahamu nafasi ya kampuni hiyo na udhamini kwa klabu hizo.

TFF iliingia mkataba wa miaka mitatu na Vodacom wenye thamani ya Sh 6.6 bilioni ambao ulimalizika mara baada ya kwisha kwa msimu uliopita.

Endapo Vodacom itajiondoa, kunazifanya klabu kukosa takribani Sh80 milioni kwa msimu, fedha hizo zilikuwa zikitolewa kwa awamu nne kwa mwaka, kila awamu timu zilikuwa zikipewa Sh20 milioni kabla ya ligi kuanza.

Katika udhamini huo, bingwa alipata Sh80.4 milioni, mshindi wa pili Sh40.2 milioni na wa tatu, Sh28.7 milioni. Mshindi wa nne Sh22 milioni na timu yenye nidhamu, Sh17 milioni.

Mchezaji bora na mfungaji bora, kila mmoja aliingiza kibindoni Sh 5.7 milioni, wakati kipa bora alituzwa Sh 5 milioni, kocha na mwamuzi bora kila mmoja alijipatia Sh8.6 milioni.

Hata hivyo, TFF imeweka wazi kuwa ligi hiyo imebaki na wadhamini wenza wawili ambao ni Azam Media wanaotoa Sh162 milioni kwa mwaka na Benki ya KCB itayotoa Sh 15 milioni kwa kila timu kwa mwaka.

Hata hivyo, Wambura pia alithibitisha kuwa bado wapo katika mazungumzo na Vodacom pamoja na kampuni kadhaa kwa ajili ya kudhamini ligi hiyo.

Alisema kinachojadiliwa zaidi ni mahitaji ya maboresho mbalimbali ya mkataba uliomalizika.

“Ukiangalia awali Vodacom walikuwa wanatoa jezi seti mbili nyumbani na ugenini na vifaa vingine kama viatu na vingine lakini msimu huo kulikuwa na timu 16 na vifaa vilikuwa havitoshelezi kwa kila timu ndio maana tunataka kama tukisaini mkataba mpya timu zifaidike zaidi ya hapo.

“Uamuzi wa kuongeza timu tulishirikiana na klabu zote za Ligi Kuu na tulikubalina lakini hata hii si sababu ya kuchelewa kupata mdhamini bali tunataka ambaye tutasaini nae mkataba aweze kutoa zaidi ya vile ambavyo tulikuwa tukipata katika mkataba wa awali,” alisema.

Timu zazidi kuugulia maumivu

Wakati TFF ikisema hayo, timu zisizokuwa na wadhamini zimeendelea kuugulia maumivu na meneja Lipuli FC ya Iringa, Mrisho Selemani, alisema wao ni miongoni mwa timu zitakazoathirika kutokana na kukosekana kwa mdhamini mkuu.

Meneja huyo alisema kuwa timu hiyo ambayo haina chanzo cha uhakika cha mapato, hadi sasa haina mdhamini yoyote wa kuwasaidia japo hela ya maji ya kunywa wachezaji hivyo kukosekana kwa wadhamini ambao husaidia japo fedha kidogo za nauli kwao litakuwa pigo la aina yake.

“Kukosekana kwa wadhamini ni jambo litakaloleta athari kwa baadhi ya timu zinazoshiriki Ligi Kuu, mfano sisi hatuna wadhamini kabisa kwa hiyo tutakuwa kwenye kipindi kigumu sana katika Ligi ya msimu huu,” alisema.

Msemaji wa Mtibwa Sugar, Thobias Kifaru, alisema kuwa kukosekana kwa wadhani kunaongeza mzigo wa gharama kwa klabu hasa ikizingatiwa kumeongezeka timu nne zaidi.

Endapo mdhamini atakosekana, kuna uwezekano mkubwa wa ligi kutawaliwa na klabu za Simba, Azam FC, Yanga pamoja na timu za majeshi za Tanzania Prisons, JKT Tanzania, Ruvu Shooting na zile za kampuni kama Mwadui FC, Mtibwa Sugar na Kagera Sugar.

Ligi Kuu Bara imepangwa kuanza Agosti 22 mwaka huu ikishirikisha timu 20 kwa mara ya kwanza kutoka timu 16 za awali.

Imeandika na Thobias Sebastian na Charles Abel.

Chanzo: mwananchi.co.tz