Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Viungo watikisa usajili Ligi Kuu

9254 PIC+VIUNGO TanzaniaWeb

Wed, 1 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Wakati Klabu za Ligi Kuu Tanzania Bara zikisubiri kwa hamu uhakiki wa usajili zilizofanya, safu ya kiungo imetikisa mchakato huo uliokamilika Alhamisi iliyopita saa sita usiku.

Tathmini iliyofanywa na gazeti hili kwenye usajili wa baadhi ya timu zitakazoshiriki Ligi Kuu msimu ujao, imebaini kuwa idara ya kiungo imepewa kipaumbele cha kwanza na idadi kubwa ya klabu kulinganisha na safu za ulinzi na ushambuliaji.

Simba iliyotwaa ubingwa wa Ligi Kuu msimu uliopita, imeonekana kujikita zaidi katika kuimarisha safu ya kiungo kwa kujumuisha majina ya nyota 11 wanaocheza nafasi hiyo yakihusisha waliokuwemo msimu 2017/2018 na wapya walioongezwa kwenye dirisha kubwa la usajili.

Wachezaji wapya wanaocheza kwenye safu ya kiungo ambao Simba imewaongeza kikosini kupitia dirisha kubwa la usajili ni Hassani Dilunga, Claytous Chama, Abdul Hamisi na Marcel Kaheza.

Wachezaji hao wanaungana na akina Jonas Mkude, James Kotei, Mohammed Ibrahim, Shiza Kichuya, Haruna Niyonzima, Said Ndemla, Mzamiru Yassin na Rashid Juma ambao walikuwemo kwenye kikosi cha timu hiyo msimu uliopita.

Kilichofanywa na Simba ndicho kimetokea kwa wawakilishi wa Tanzania Bara katika Kombe la Shirikisho Afrika msimu ujao, Mtibwa Sugar ambayo imekamilisha usajili huku ikiwa na idadi kubwa ya wachezaji wanaocheza safu ya kiungo.

Mtibwa Sugar imejumuisha viungo 10 kwenye kikosi chake ambao ni Henry Joseph, Shabani Nditi, Salum Kihimbwa, Ismail Aidan, Haruna Chanongo, Ally Makarani, Salehe Khamis, Ayoub Semtawa, Abuu Juma na Abdul Yusuf.

Wakati Simba na Mtibwa ambazo zitaiwakilisha Tanzania Bara kwenye mashindano ya kimataifa msimu ujao zikijaza idadi kubwa ya viungo, Azam, Yanga na Singida United nazo zimefuata mkumbo kwa kusajili kundi kubwa la wachezaji wa viungo.

Yanga yenyewe imesajili jumla ya viungo 13 huku Azam ikiwasilisha majina ya viungo wanane wakati Singida United imesajili wachezaji 11 wa nafasi hiyo.

Viungo ambao wamejumuishwa kwenye usajili wa Yanga ni Thabani Kamusoko, Jafari Mohamed, Raphael Daud, Maka Edward, Said Juma, Deus Kaseke, Emmanuel Martin, Juma Mahadhi, Pato Ngonyani, Paul Godfrey, Feisal Salum na Papy Tshishimbi

Nyota wanaocheza nafasi ya kiungo ambao wamesajiliwa na Azam ni Stephan Kingue, Tafadzwa Kotinyu, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Frank Domayo, Enock Atta, Joseph Mahundi, Bryson Raphael na Ramadhani Singano ‘Messi’.

Wachezaji 11 wa nafasi ya kiungo ambao Singida United imewasajili ni Rashid Simkoko, John Tibar, Assad Juma, Lubinda Mundia, Mohammed Tello, Hans Koffie, Benedict Jr, Godfrey Mwashiuya, Frank Zakaria na Mohammed Titi.

Timu nyingine zilizojaza viungo ni Mbeya City yenye wachezaji 10 sawa na Ruvu Shooting yenye idadi kama hiyo ya wachezaji.

Usajili wa idadi kubwa ya viungo unatoa taswira kuwa huenda msimu ujao kukapatikana idadi kubwa ya mabao kwani mara kwa mara safu ya kiungo ndio imekuwa chanzo kikuu cha kutengeneza nafasi za mabao na kuifanya timu itawale mchezo jambo ambalo huchangia kwa kiasi kikubwa kuzalisha mabao.

Hata hivyo, wakati timu nyingi zikionekana kuimarisha safu yake ya kiungo, Biashara United iliyopanda Ligi Kuu kwa mara ya kwanza, yenyewe inaonekana inataka kuwa na safu imara zaidi ya ulinzi kuliko timu nyingine.

Timu hiyo kutoka mkoani Mara imesajili jumla ya wachezaji 14 wanaocheza kwenye safu ya ulinzi, idadi ambayo ni kubwa zaidi kuliko timu nyingine.

Baadhi ya mabeki kati ya hao 14 waliosajiliwa na Biashara United ni Joseph Mapembe, Sospeter Maiga, Derrick Mussa, Lenny Vedatus na Godfrey Malibiche.

Wengine ni Abdul Madjid, Lameck Abel, Kazee Maginga, Edgar Bwire na Frank Sekule.

Chanzo: mwananchi.co.tz