Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Vita ndio imenoga: Kocha Zahera anasa dawa ya Simba

44235 Zahera+pic Vita ndio imenoga: Kocha Zahera anasa dawa ya Simba

Thu, 28 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

VINARA wa Ligi Kuu Bara, Yanga alfajiri ya leo Alhamisi imepaa kwenda Mwanza, lakini huku nyuma kocha wake, Mwinyi Zahera akinasa janja ya Simba ambayo imekuwa ikila viporo vyake na kupunguza pengo la pointi na kikosi chake.

Yanga inaifuata Alliance keshokutwa Jumamosi kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, huku ikitofautiana alama 13 na wapinzani wao hao ambao juzi wametoka kuvunja rekodi Uwanja wa Samora, Iringa kwa kuilaza Lipuli mabao 3-1.

Simba ilikuwa haijawahi kuifunga Lipuli tangu irejee Ligi Kuu kabla ya juzi kuifanyizia kwa mabao ya Clatous Chama (mawili) na Meddige Kagere na kufikisha alama 48 kutokana na mechi 19, sita pungufu na ilizonazo Yanga iliyocheza 25 na kuvuna pointi 61.

Ipo hivi. Kabla ya kuondoka leo, Yanga jana asubuhi ilifanya mazoezi ya mwisho Uwanja wa Chuo cha Polisi, Kurasini kuanzia saa 3:30 mpaka 5:00 asubuhi na katika mazoezi hayo alikuwa akimtumia sana Papy Kabamba Tshishimbi kuzuia na kutengeneza mabao ya timu hiyo ambapo mwisho wa tizi hilo Zahera alisema ni maalumu ya kuikimbia Simba kileleni.

Kocha Zahera alionekana kumsuka kiungo huyo katika maeneo mawili ambayo alitaka kuona pia wachezaji wengine wakifanyia kazi maelekezo yake. Katika kumsuka upya Tshishimbi na kuwa roho ya timu kama zamani, Zahera aliwagawa wachezaji wake katika makundi mawili ambayo kila moja lilikuwa na wachezaji 14, ambao wanne walinasafa na kumi walikuwa pembeni wakipasiana.

Mara ya kwanza Tshishimbi aliwekwa katika kundi la watu wanne ambao walisafa na alitaka kumuona akitafuta mpira kwa nguvu na kupora kwa wachezaji wa pembeni.

Baada ya Tshishimbi kuonesha uweazo katika kukaba na kunasa mipira mingi, Zahera alimbadilisha na kumuweka kwa waliokuwa wakipasiana na alitaka apige pasi nyingi kwa haraka bila kukutwa au kuporwa na wachezaji waliokuwa wakikaba. Mazoezi yote hayo, Tshishimbi alikuwa akipangiwa na Zahera muda alipokuwa akifanya vizuri alikuwa akipongezwa na kutakiwa kufanya zaidi, ila pale alipokosea kocha wake alionekana kuwa mkali na hakutaka kuona akifanya hivyo mara kwa mara.

Mara baada ya kumalizika kwa mazoezi hayo Zahera, alisema Tshishimbi alikuwa akicheza vibaya kwa sababu alikuwa anacheza huku akiuguza maumivu ya mguu yaliyomsumbua, ila kwa sasa ameiva na atamtumia ili timu ipate matokeo ili kuzidi kuwakimbia Simba na wapinzani wengine kwenye Ligi Kuu.

“Nilichofanya ni kumweleza tu ukweli na kubalia hali yake ilivyo. Inabidi apumzike kwa muda ili upate muda wa kutosha kupata matibabu na kupona kabisa kuliko kucheza huku akiwa na maumivu ambayo yanamfanya kuonekana mchezaji wa kawaida,” alisema Zahera.

“Baada ya kukubaliana na hali alikubali kuwa nje kwa muda wote huo na alipata matibabu stahiki kabisa ambayo yamemrudisha uwanjani, na ili aweze kuwa katika kiwango chake bora ni lazima nimpangie mazoezi magumu ya kumuongezea ufiti ili kurudi katika hali yake ya zamani.

“Sifa ya kwanza kwa Tshishimbi ni kucheza kwa kutumia nguvu muda mwingi si kama Ibrahim Ajibu au Mrisho Ngassa kwa maana hiyo lazima nimtengeneze katika mazoezi ya nguvu ili awe bora zaidi ya mechi hizi mbili alizocheza na kuwa kama hapo awali,” alisema Zahera.

“Matayarisho ambayo tumeyafanya katika mazoezi haya ndio ambayo tutakwenda kuyatumia katika mechi dhidi ya Alliance, ili kujiongezea alama nyingine tatu, wapinzani wetu wanakuja kwa kasi, hivyo lazima nasi tujiweke sawa kuhakikisha tunafanikiwa kubeba tiketi ya CAF,” alisema.

DANTE MAJANGA, MAHADHI KARUDI

Naye Mratibu wa Yanga, Hafidh Saleh alisema kikosi chao kabla ya kuondoka kilifanya mazoezi ya nguvu kwa ajili ya mechi dhidi ya Alliance lakini katika safari yao ya Mwanza ambayo wataondoka Alfajiri ya leo Alhamisi kuna baadhi ya wachezaji ambao watakosekana.

“Beki wetu wa kati Andrew Vincent ‘Dante’ atakosekana katika safari na mechi kwa jumla na tutaondoka tukiwa na wachezaji 20. Kwa kuwa tunakwenda kucheza moja tu hakutakuwa na shida. Lakini kitu kizuri ni kwamba Thabani Kamusoko na Juma Mahadhi wamerejea ndani ya kikosi na walifanya mazoezi ya nguvu na wenzao,” alisema Saleh.



Chanzo: mwananchi.co.tz