Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Viporo vya Mechi kufutwa Ligi Kuu

7205e1853e52517a6f0dcab37f0c8800 Ligii Kuu kumaliza viporo vya timu zinazoshiriki michuano ya kimataifa

Thu, 5 Aug 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) imesema msimu ujao hakutakuwepo viporo kwa timu zitakazoshiriki michuano ya kimataifa baada ya kufanya maboresho ya kanuni mbalimbali za ligi.

Ilizoeleka kila msimu timu zinazoshiriki michuano ya kimataifa kuwa na viporo vingi, kwa mfano Simba ilikuwa nyuma dhidi ya wenzake karibu mechi nane, kitendo kilichotafsiriwa kuwa huenda wanabebwa.

Akizungumzia suala hilo Ofisa Mtendaji Mkuu wa TPLB, Almasi Kasongo alisema ili msimu ujao usiwe na viporo kabisa wamejadiliana na wadau kutoka klabu za Ligi Kuu na kuamua wawe wanasimamisha mzunguko ule ambao timu nyingine zitakuwa zinawakilisha kimataifa.

“Baada ya kutafuta njia sahihi za kuondokana na viporo tumekubaliana kwa kauli moja kuwa ligi iwe inasimama pale, ambapo timu zetu zitakwenda kuwakilisha kimataifa wakirudi inaendelea na lengo ni kuleta ushindani na klabu zimebariki,”alisema.

Alisema muafaka huo umekuja baada ya kuwepo kwa kikao cha maboresho ya kanuni za ligi sambamba na kuangalia changamoto za msimu uliopita kilichowakutanisha viongozi mbalimbali wa klabu.

Msimu ujao timu zinazotarajiwa kuwakilisha nchi katika michuano ya kimataifa ni Simba na Yanga Ligi ya Mabingwa, Azam FC na Biashara United Kombe la Shirikisho Afrika.

Katika hatua nyingine, Kasongo alisema Ligi Kuu inatarajiwa kuanza rasmi Septemba 29, mwaka huu na kwamba wakati wowote watatoa ratiba kamili ili timu zianze maandalizi.

Kabla ya kuanza kwa ligi hiyo, kutakuwa na mchezo wa Ngao ya Jamii utakaozikutanisha Simba na Yanga kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa kuanzia saa 11:00 jioni.

Wadau wa klabu waliokuwepo kwenye kikao hicho ni Mwenyekiti wa Yanga Dk Mshindo Msolla aliyepongeza ushirikishwaji huo wa bodi ya ligi akisema anatumai michuano ijayo itakuwa mizuri zaidi. Alisema wao wamejipanga vizuri kwani msimu ujao matunda ya uwekezaji wa miaka miwili ndio yataanza kuonekana kwao kutokana na usajili waliofanya kuboresha kikosi chao.

Mwenyekiti wa Simba Murtaza Mangungu alisema mjadala huo wa kanuni ulikuwa ni mzito, lakini hatimaye wameafikiana na hivyo anategemea ligi ijayo itakuwa bora kama tu mambo waliyojadili na kuyapitisha yatazingatiwa.

Msemaji wa Ruvu Shooting Masau Bwire alisema kanuni za Ligi Kuu zitakazotumika msimu ujao zimeboreshwa, zitaiongoza ligi katika misingi inayotakiwa

Chanzo: www.habarileo.co.tz