Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Vijana Serengeti Boys wamwagiwa mamilioni

32676 Pic+yanga Tanzania Web Photo

Fri, 21 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Wachezaji wa timu ya taifa ya Serengeti Boys wamepongezwa kwa mafanikio huku wakizawadiwa fedha taslimu kwa kutwaa ubingwa wa soka kwa vijana chini ya miaka 17 Ukanda wa Kusini mwa Afrika, Cosafa mwishoni mwa wiki.

Timu hiyo iliifunga Angola penalti 6-5 baada ya kumaliza mchezo huo wa fainali bila kufungana.

Wachezaji na viongozi wa timu hiyo walikuwa kwenye hafla fupi jana kuwapongeza kwa kutwaa ubingwa huo ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya michuano hiyo itakayofanyika Tanzania mwakani.

Mengi awamwagia fedha

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni za IPP, Reginald Mengi amewapa zawadi ya fedha kama pongezi za kutwaa ubingwa wa mashindano ya vijana wa umri kwa kanda Kusini mwa Afrika.

Mengi ambaye ndiye mlezi wa timu hiyo, alisema kuwa ameamua kutoa fedha hizo ambazo hakutaka kuweka hadharani kiwango chake.

“Vijana hawa wamefanya kazi kubwa na nimeona niwape kiasi kidogo cha fedha kama motisha kwao lakini ninaamini mambo mazuri zaidi yanakuja,” alisema Mengi.

Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe alimpongeza na kumshukuru Mengi kwa jinsi anavyoisaidia timu hiyo. “Nakushukuru na nakupongeza sana mzee wetu Mengi kwani tukio hili ni la kihistoria,” alisema Waziri Mwakyembe.

TFF yakazia kanuni

Wakati vijana hao wakipongezwa, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ambalo limepanga kubadili baadhi ya kanuni za ligi ili kulinda vipaji vya vijana wadogo.

Akizungumza katika hafla hiyo, Rais wa TFF, Wallace Karia alisema kuwa kanuni hizo zinalenga kuhakikisha vipaji vya vijana havipotei.

“Tunataka tubadilishe kanuni zetu kwa baadhi ya timu ambazo zinawachukua wachezaji ambao wamefanya vizuri kwenye timu ndogo. Wanawasajili kwa mikataba minono lakini wanakwenda kuwaweka benchi hawapati nafasi ya kucheza.

Kuna wachezaji wetu ambao walikuwa ni wazuri lakini hawachezi hivyo tunataka kuweka kanuni kuzibana hizo klabu angalau ziwe zinawatoa kwa mkopo,” alisema Rais Karia.

Wazo hilo la Karia liliungwa mkono na Dk Mwakyembe ambaye naye alisema kuwa lina tija kwa soka hapa Tanzania.

“Mimi nakuunga mkono na ninatamani hizo kanuni zianze kutumika hata mchana huu wa leo kwa sababu hatuko tayari kuona vipaji vya vijana wetu vinapotea,” alisema.

Baadhi ya nyota ambao licha ya kufanya vizuri kwenye timu za vijana na kisha wakasajiliwa huku baadaye wakikosa nafasi ya kucheza ni washambuliaji Said Musa, Yohana Nkomola na Abdul Seleman.

Nyota hao walionyesha kiwango bora katika kikosi cha Serengeti Boys kilichoshiriki fainali za Afrika mwaka jana huko Gabon lakini wote wamejikuta wakisugua benchi katika vikosi vya Simba na Yanga zilizowasajili msimu huu



Chanzo: mwananchi.co.tz