Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Vigogo sita wawekewa pingamizi Uchaguzi Yanga

52605 Pic+uchaguzi

Tue, 16 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam.Wakati mchakato wa usaili na pingamizi kwa wagombea katika uchaguzi wa klabu ya Yanga ukielekea ukingoni, wagombea sita wamewekewa pingamizi.

Mchakato wa usaili uliokwenda sanjari na kamati ya uchaguzi kupokea mapingamizi uliofanyika kwa siku tatu utahitimishwa leo Jumanne.

Habari kutoka ndani ya kamati ya uchaguzi ya Yanga imelitonya MCL Digital kuwa mpaka leo Aprili 16 saa 10:00 Asubuhi, wagombea sita walikuwa wamewekewa pingamizi.

Wagombea hao ni waliokuwa wajumbe wa kamati ya utendaji kwenye uongozi uliopita ambao walijiuzuru, Hussein Nyika, Thobias Lingalanga, Samwel Lukumay na Siza Lyimo, wengine ni Elias Mwanjara na Palina Conrad.

"Sababu za mapingamizi hayo walioweka wamedai ni uzoefu na maadili, lakini wale ambao walikuwa kwenye kamati ya utendaji iliyopita wenyewe wamewekewa pingamizi kwasababu hawakuwasilisha bajeti ya mapato na matumizi walipokuwa kwenye uongozi," alisema mjumbe wa kamati ya uchaguzi ambaye aliomba hifadhi ya jina.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Sam Mapande alipoulizwa alisema yuko mahakamani hawezi kuzungumzia suala la wagombea hao kuwekewa pingamizi.

Habari zaidi kutoka kwenye kamati ya uchaguzi ilibainisha kwamba, wajumbe watakutana Leo Jumanne kwa ajili ya kukamilisha mchakato wa usaili na kupitia pingamizi walizowekewa baadhi ya wagombea.

"Kama nilivyosema awali, mchakato wa usaili ulifanyika kwa siku tatu kuanzia Jumapili iliyopita na ulikwenda sanjari na kupokea pingamizi, jambo ambalo litahitimishwa Leo (Aprili 16) kabla ya kutoa matokeo ya pingamizi na wagombea kuelekea hatua nyingine ya uchaguzi."



Chanzo: mwananchi.co.tz