Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Vigogo Savio, ABC vyatuma salamu Ligi ya Taifa

Wed, 31 Oct 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Baada ya ushindi, kocha wa Savio, Evarist Mapunda amesema ana matumaini ya kutwaa ubingwa na kuwavua mabingwa watetezi Oilers.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Mapunda alidai ndoto yao ni kucheza mashindano ya kimataifa mwakani, baada ya kuanza vyema juzi jioni.

"Ndoto yetu ni kucheza mashindano ya kimataifa ushindi wa leo (juzi) ni mwanzo mzuri kwa kuwa unatuelekeza katika malengo yetu,"alisema Mapunda.

Kocha huyo alisema ushindani ni mkubwa hasa kwa timu za Dar es Salaam, lakini amesisitiza wamejiandaa vyema kutwaa ubingwa.

Savio ambao ni mabingwa wa Ligi ya Mpira wa Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam (RBA) na ABC zilishinda mechi zao za Ligi ya Taifa ya Mpira wa Kikapu (NBL), kwenye Uwanja wa Harbours, jijini.

ABC ilitakata katika mchezo huo baada ya kuilaza Vijana pointi 72-62 na Ukonga Kings  ilitoka kichwa chini baada ya kuchapwa pointi 69-63.

Katika mchezo mwingine, DB Lionesses iliichapa VBQ pointi 50-47 kwenye mashindano hayo yanayoshirikisha timu 11 zikiwemo tatu za wanawake.

Kamishna wa Ufundi na Uendeshaji wa Mashindano wa Shirikisho la Mpira wa Kikapu Tanzania (TBF), Manase Zablon alisema mshindi wa kwanza na pili wataiwakilisha nchi kwenye mashindano ya kimataifa ya Kanda ya Tano Afrika mwakani.

Manase alisema kwa wanawake, kila timu itacheza mechi nne za nyumbani na ugenini zikishindana katika mtindo wa ligi ili kupata bingwa.

"Wanaume zitacheza katika makundi kabla ya kuanza robo fainali Alhamisi ijayo na mechi za robo fainali zitachezwa kwenye Uwanja wa Ndani wa Taifa,” aliongeza Manase.

Mkurugenzi huyo alisema mechi za makundi zitachezwa Kurasini  na Novemba Mosi, mechi za robo fainali zitapigwa Uwanja wa Taifa wa Ndani, Dar es Salaam.

Chanzo: mwananchi.co.tz