Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Vigingi vitatu kwa Tarimba Yanga

8949 Vigingi+pic TZW

Tue, 12 Jun 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Klabu ya Yanga imeunda Kamati Maalum ya kuivusha timu hiyo katika kipindi cha mpito, lakini vigogo hao wanatakiwa kuruka viunzi vitatu vigumu ili kupata mafanikio.

Kamati hiyo ilipata baraka za wanachama katika mkutano mkuu wa klabu hiyo uliofanyika juzi kwenye Ukumbi wa Bwalo la Maofisa wa Polisi Oysterbay, Dar es Salaam.

Vigogo waliopewa dhamana ya kuivusha Yanga ni Mwenyekiti, Tarimba Abbas na Makamu Mwenyekiti, Mecky Sadick, wajumbe ni Abdallah Binkleb, Hussein Nyika, Samwel Lukumay, Mashauri Lucas, Yusuphed Mhandeni, Hamad Islam, Makaga Yanga, Ridhiwani Kikwete, Majid Suleiman na Hussein Ndama.

Wakati Tarimba aliwahi kuwa Rais wa Yanga, Nyika na Lukumay ni Wajumbe wa Kamati ya Utendaji ambao pia wamo kwenye Kamati ya Mashindano na Usajili.

Wajumbe wa Kamati ya Mashindano na Usajili ni Mashauri, Ndama, Islam, Mhandeni na Majid. Sadick aliwahi kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam na Kilimanjaro.

Kiunzi cha kwanza kwa kamati hiyo ni kuhakikisha nyota waliomaliza mikataba yao wanatia saini kuendelea kubaki kwenye timu hiyo, kusimamia usajili wa wachezaji wapya ambao wataiongezea ufanisi Yanga.

Pia kusimamia malipo stahiki kwa baadhi ya wachezaji waliopo katika kikosi na kuhakikisha timu hiyo inafanya vyema kwenye Kombe la Shirikisho Afrika.

Wakati mchakato wa mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji wa klabu hiyo ukiendelea huku Serikali ikiipa siku 60 za kuziba mapengo ya viongozi waliojiuzulu, kamati hiyo yenye wajumbe 12 itakuwa kazini kuhakikisha inairudisha Yanga kwenye mstari wa ushindani kwa kuipatia kikosi imara.

Mtihani wa kwanza kwa kamati hiyo inayoongozwa na Tarimba ambaye ni Mkurugenzi wa Utawala na Uendeshaji wa SportPesa, ni kusaka fedha za nyota wake muhimu waliomaliza mikataba kuhakikisha wanaendelea kubaki kwenye timu hiyo.

Zaidi ya nyota sita tegemeo wa Yanga wamemaliza mikataba na wamekuwa wakinyemelewa na klabu za Simba na Azam ambazo zimekuwa zikimwaga fedha kwenye dirisha la usajili ili kuvutia wachezaji mbalimbali.

Nyota ambao kamati ya Tarimba inapaswa kuwalinda kwa nguvu zote ni Kelvin Yondani, Obrey Chirwa, Andrew Vincent, Hassani Kessy, Beno Kakolanya na Juma Abdul anayedaiwa tayari ameshamalizana na Azam.

Wakati ikipambana kuwabakiza wachezaji hao, kamati hiyo itakuwa vitani kufanya usajili bora wa nyota wa ndani na nje ya nchi kuziba mapengo ya wachezaji walioondoka au kuongeza ufanisi kwa nafasi zilizotetereka msimu uliomalizika.

Yanga inapaswa kusajili takribani nyota saba wapya wanaocheza nafasi ya kipa, beki wa kati, kiungo mshambuliaji, viungo wa pembeni na mshambuliaji wa kati.

Kiunzi cha pili ambacho vigogo hao wanatakiwa kukiruka ni kuisaidia timu hiyo kulipa madeni ya baadhi ya wachezaji wake ambayo yametokana na malimbikizo ya fedha za usajili walipokuwa wanatia saini mikataba ya kucheza Yanga.

Tatu; kamati hiyo ina jukumu zito la kuhakikisha timu hiyo inafanya vizuri kwenye hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Hadi sasa, Yanga inashika mkia kwenye Kundi D ikiwa na pointi moja nyuma ya USM Alger yenye pointi nne, huku Gor Mahia na Rayon Sports zikiwa na pointi mbili kila moja.

Yanga inakabiliwa na mechi mbili ngumu na muhimu dhidi ya Gor Mahia ambayo itacheza mwezi ujao ugenini na nyumbani.

Michezo hiyo miwili mfululizo, imeshikilia hatima ya Yanga kufuzu hatua ya robo fainali na ikiibuka na ushindi, itaweka hai matumaini ambapo itafikisha pointi saba lakini ikipoteza, itakuwa katika nafasi finyu ya kupenya kwenda hatua inayofuata.

Kocha na mchambuzi wa soka, John Tegete alishauri mambo matatu ya msingi ambayo kamati hiyo inapaswa kuyafanya ili timu icheze kwa ufanisi katika mashindano yanayoikabili.

“Kwanza wanapaswa kusajili wachezaji ambao wana viwango visivyotofautiana sana ambao watakuwa na ushindani wa namba, kuanzia mazoezini hadi kwenye mechi tofauti na kikosi walichonacho sasa ambacho wachezaji wengi walisajiliwa wakiwa na uwezo mdogo kwa sababu tu Yanga haikuwa vizuri kiuchumi.

“Lakini pia wasifanye usajili kwa kukurupuka. Waangalie mahitaji ya msingi ya timu na wasajili watu kulingana na mahitaji hayo badala ya kutaka kujaza kundi kubwa la wachezaji wanaocheza nafasi moja kama ilivyofanya timu fulani hapa nchini.

“Usajili usiendane na kasumba ya kutaka kusajili kwa kuangalia kigezo cha huyu anaipenda Yanga au haipendi. Wakifanya hivyo wanaweza kujikuta hawapati wachezaji wazuri,” alisema Tegete.

Kocha Kennedy Mwaisabula alisema Yanga inapaswa kufanya mabadiliko makubwa kwenye kikosi chake kwa kuwa waliopo wengi hawana hadhi ya kuitumikia timu hiyo.

“Nina imani kubwa na kamati iliyoundwa kwa sababu wajumbe wake wanaufahamu vyema mpira wa miguu hivyo kwa kushirikiana na benchi la ufundi nadhani watafanya usajili imara utakaoirudisha timu kwenye mstari.

Chanzo: mwananchi.co.tz