Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

VIDEO: Yanga SC hakuna kulala kwa Pyramids

Video Archive
Mon, 28 Oct 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mwanza. Jiji la Mwanza leo ‘litasimama’ kwa dakika 90 kutokana na mchezo wa Kombe la Shirikisho barani Afrika pale wawakilishi pekee wa Tanzania katika michuano ya kimataifa, Yanga watakapoikaribisha Pyramids kutoka nchini Misri.

Yanga itaingia katika mchezo huo utakaoanza saa 10:00 jioni ikiwa na lengo la kupata ushindi utakaowaweka katika mazingira mazuri kwenye mchezo wa marudiano ili waweze kutinga hatua ya makundi ya mashindano hayo.

Kama Yanga itapata ushindi leo na mechi ya marudiano itakayofanyika Novemba 4 nchini Misri, basi itatinga hatua ya makundi moja kwa moja.

Timu hizo ambazo ni mara ya kwanza kukutana kila upande unaonekana kuwa na morali ya mchezo.

Pyramids ambao walitua jijini hapa juzi usiku kwa ndege binafsi, walionekana kujiamini huku kocha wao mkuu, Desbre Sebastiene akiwataja wachezaji wachache wa Yanga kuwa ni tishio, lakini wamejipanga kufanya vizuri katika mchezo huo.

Sebastien aliwataja wachezaji wa Yanga, Papy Tshishimbi na Juma Balinya kuwa ni wazuri, na anawajua, lakini wao wamekuja kwa lengo la kufuata ushindi.

Pia Soma

Advertisement
Alisema wataingia uwanjani kwa umakini kuhakikisha kuwa wanafikia lengo lao la kufuzu hatua ya makundi.

“Mchezo utakuwa na ushindani kutokana na wapinzani wetu kuwa na timu nzuri, lakini tulichokuja kufanya ni kusaka ushindi. Nalijua sana soka la Tanzania, hivyo tuko tayari kwa mapambano,” alisema.

Kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera alisema hana wasiwasi na wapinzani wao kwani maandalizi waliyoyafanya yanatosha kuwamaliza Pyramids.

Alisema mbinu alizowapa wachezaji wake ikiwamo namna ya kumiliki mpira, kupiga, kupokea pasi pamoja na kufunga mabao itatosha kumaliza mchezo huo mapema.

“Nasikia wamekuja na ndege, hilo halitutishi kwani Yanga haijawahi kupanda ndege? Sisi tumejiandaa kivyetu na tunahitaji ushindi ili kujiwekea mazingira mazuri ya kufuzu kwenye makundi,” alisema Zahera.

Nahodha wa timu hiyo, Tshishimbi na beki Kelvin Yondani walisema utulivu, kujiamini na kufuata malekezo ya kocha ndio silaha itakayowapa ushindi katika mchezo wa leo.

“Tuwaombe mashabiki kujitokeza kwa wingi, mchezo huu ni muhimu sana kwa Yanga kushinda ili mechi ya marudio iwe nyepesi kwetu, tutafanya alichotuelekeza kocha lakini pia tutaongeza juhudi binafsi,” alisema Tshishimbi.

Yondani alisema, “Mimi na wengine tuna uzoefu (wa mechi za kimataifa), kwa hiyo tutawaelekeza wenzetu (wasio na uzoefu) uwanjani kuhakikisha wanasimama imara ili kufanya vizuri,” alisema beki huyo.

Mchezo huo unazikutanisha timu hizo zikiwa na rekodi tofauti ikiwamo kuanzishwa kwao, ambapo Yanga ilianzishwa 1935 ilhali Pyramids imeanzishwa 2008.

Timu hizo zimefikia hatua ya kukutana baada ya Yanga kuangukia katika Kombe la Shirikisho ilipotolewa na Zesco ya Zambia kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika wakati Pyramids wameingia kwa mara ya kwanza katika michuano hiyo katika hatua ya mtoano ili watinge hatua ya makundi.

Chanzo: mwananchi.co.tz