Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

VIDEO: Simba yaandika rekodi, yatinga robo fainali kibabe

Mon, 18 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

HAPA chezea Simba. Mabingwa wa Ligi Kuu Bara, Simba jana Jumamosi iliandikisha rekodi mpya Afrika kwa timu za Tanzania baada ya kuinyuka AS Vita ya DR Congo kwa mabao 2-1 na kutinga robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kutoka Kundi D ikiungana na Al Ahly ya Misri.

Wekundu wa Msimbazi ambao wamemaliza kundini katika nafasi ya pili ikikusanya alama 9, ilipata ushindi huo kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam na kuwa klabu ya kwanza ya Tanzania kuvuka hatua ya makundi tangu michuano hiyo ya CAF ilivyobadilishwa mfumo mwaka 1997.

Mabao ya nahodha Msaidizi, Mohammed Hussein 'Tshabalala' na lile la Clatous Chama dakika za jioni ziliufanya Uwanja wa Taifa kurindima kwa furaha za shangwe huku mitaani honi na shamrashamra za mashabiki zikianikiza jijini la Dar es Salaam.

Mashabiki wachache wa Yanga waliojitokeza uwanjani hapo walinywea baada ya Chama kufunga bao muhimu dakika ya 90 akimalizia mpira wa Haruna Niyonzima kushindwa kuokolewa na mabeki wa AS Vita waliokuwa wa kwanza kupata bao dakika ya 13 tu kupitia kwa Kasengu Kazadi.

Mbali na kufuzu hatua hiyo lakini Simba imevuna kiasi cha Dola 650,000 (zaidi ya Sh1.5 bilioni) na sasa inasubiri kujua itapangwa nani katika hatua hiyo inayoshirikisha klabu nane zilizopenya usiku wa jana.

Timu ambazo Simba inaweza kukutana nazo ni kati ya Wydad Casablanca ya Morocco iliyoongoza Kundi A, Esperance ya Tunisia (Kundi B) ama TP Mazembe (Kundi C).

Nyingine zilizopenya hatua hiyo mbali na Al Ahly na Simba za Kundi D, ni pamoja na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini, Horoya ya Guinea, CS Constantine ya Algeria.

Simba ikitumia msemo wa Do or Die (Kufa ama Kupona) ililianza pambano hilo kwa kasi, lakini wakakutana na kasi ya Wakongo waliotangulia kupata bao la kuongoza baada ya beki Pascal Wawa kujichanganya na kumpa nafasi Kazadi kufunga bao hilo lililopokelewa kwa furaha na mashabiki wa Yanga waliokuwa wakiunga mkono As Vita, wakisahau kwa muda machungu ya kipigo cha bao 1-0 walichoopewa timu yao mjini Iringa na Lipuli FC.

Hata hivyo Simba ilitulia na kusukuma mashambulizi makali na katika dakika ya 36 Mohammed Hussein 'Tshabalala' alifunga bao baada ya kujichanganya na kipa wa Vita aliyemuangusha wakati akiupiga mpira ulioingia wavuni na kuiswazishia timu yake.

Katika mchezo huo Simba ilikuwa na sura mpya kikosini tofauti na mchezo wao uliopita waliochapwa mabao 2-0 na JS Saoura, kwa Erasto Nyoni, Mzamiru Yasin na Emmanuel Okwi wakianza, jaopo walimkosa Jonas Mkude na Paul Bukaba waliocheza mechi iliyopita.

Dakika 45 za kwanza, Vita walionekana bora kuliko Simba kwa kutengeneza nafasi nyingi, lakini umakini wa beki ya Simba iliwafanya wapoteze nafasi nyingi za wazi, hali iliyokuwa tofauti katika kipindi cha pili ambapo Simba ndio waliong'ara zaidi hasa baada ya kumtoa Emmanuel Okwi na kumuingiza Haruna Niyonzima na baadaye Mzamiru Yasin na kumuingiza Hassan Dilunga na kuwakimbiza wapinzani wao.

Ndipo katika dakika za jioni kabisa Chama akafanya yake kwa kufunga bao lililopokelewa kwa furaha na wanamsimbazi kwani liliihakikishia Simba kutinga robo fainali.

Kabla ya mchezo huo wachezaji wa As Vita waligomea vyumba vya kubadilishia nguo na kuvaa pia viziba pua kwa hisia za kupulizwa kwa hewa chafu vyumbani humo, lakini mwishowe wakajikuta wakianguikia pua kwa kulala ugenini kwa mara nyingine mbele ya Mnyama.

Matokeo hayo yameifanya wanafainali hao wa Kombe la Shirikisho kwa msimu uliopita wakimaliza mkiani mwa kundi nyuma ya JS Saoura walitandikwa mabao 3-0 ugenini na Al Ahly.

Simba imeendeleza rekodi za kuwa klabu yenye mafanikio kwa michuano ya Afrika kwani mwaka 1974 ilifika nusu fainali ya Klabu Bingwa Afrika, kabla ya mwaka 1993 kutinga fainali ya Kombe la CAF na kupoteza kwa Stella Abidjan na mwaka 2003 kutinga makundi ya Ligi ya Mabingwa kwa kuwavua taji Zamalek.



Chanzo: mwananchi.co.tz