Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

VIDEO: Simba, Yanga zamlilia Ruge

44187 RUGE+PIC VIDEO: Simba, Yanga zamlilia Ruge

Thu, 28 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam.Wanamichezo nchini wamemtaja aliyekuwa Mkurugenzi wa Vipindi na Uzalishaji wa Clouds Media, Ruge Mutahaba alikuwa mbunifu katika sekta ya michezo.

Miongoni mwa wadau walioguswa na kifo cha Ruge aliyefariki Afrika Kusini ni Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, Salim Abdallah ‘Try Again’.

Simba

Akizungumza Dar es Salaam jana, Try Again alisema Ruge alikuwa na maono ya mbali katika sekta ya michezo hasa soka na anakumbuka alivyotoa mchango katika klabu ya Simba.

Try Again ambaye alikuwa Kaimu Rais wa Klabu ya Simba, alisema Ruge alikuwa mwanachama, mchezaji wa Friends of Simba na Simba Veterans.

“Amewahi kushiriki katika maandalizi ya sherehe ya Simba Day, niliwahi kumshauri aanzishe kampuni akanisikiliza na ndiye alinipa jina la Try Again la kampuni yangu ambalo ndilo linanitambulisha katika soka.

“Ruge alikuwa na mchango mkubwa Simba, alikuwa Mjumbe wa Kamati ya Masoko na Uwekezaji ya Simba mimi nikiwa mwenyekiti tumefanya naye mambo mengi,”alisema Try Again.

Yanga

Kaimu Mwenyekiti wa Klabu ya Yanga, Samwel Lukumay alisema kifo cha Ruge ni pigo kwa Taifa kwa kuwa alikuwa na ushawishi na mchango kwa idadi kubwa ya vijana.

“Ni ngumu kuamini, lakini ndiyo hivyo lazima maandiko yatimie, Ruge alikuwa na mchango mkubwa katika mambo mengi hata katika soka, nakumbuka kuna mechi moja ya Simba na Yanga alikuwa mstari wa mbele katika kuitangaza na ikateka nchi,” alisema Lukumay.

Alisema Yanga ina uhusiano mzuri na Clouds kupitia Ruge katika matangazo tangu enzi za uhai wake.

Riadha

Mwanariadha nguli na bingwa wa zamani wa dunia wa mbio za mita 1500 na mshindi wa medali ya fedha ya Olimpiki ya 1980, Filbert Bayi alisema vijana wanapaswa kujifunza kupitia Ruge.

“Vijana wakiendeleza mazuri ambayo Ruge amefanya enzi za uhai wake itakuwa ni shukrani tosha katika kumuenzi alikuwa mtu aliyejitolea kuleta maendeleo,” alisema Bayi.

Bayi alisema alimfahamu Ruge alipohudhuria katika moja ya vipindi vya michezo vilivyoandaliwa na Clouds.

Ngumi

Bingwa wa zamani wa dunia wa WBU, Rashid Matumla alisema Ruge alishiriki kikamilifu kuwaandalia mabondia mapambano.

“Binafsi Ruge amenisimamia mapambano yangu matatu, hakuishia hapo hata mdogo wangu Mbwana ameandaliwa mapambano mengi na Ruge. Alikuwa kijana mwenye mipango mingi ya maendeleo katika tasnia mbalimbali,” alisema Matumla.

Bondia Francis Cheka alisema mara ya kwanza pambano alilopigana katika ngumi za kulipwa na kupata fedha nyingi liliandaliwa na Prime Time Promotions chini ya Ruge.

“Nakumbuka Ruge na Kusaga (Joseph) walianza kuniaminisha ngumi zina pesa baada ya Kusaga kuniandalia pambano la kwanza na Matumla, lakini aliyekuwa akisimamia kila kitu alikuwa ni Ruge,” alisema Cheka.

Mwenyeki wa zamani wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Kanali Mstaafu Idd Kipingu alisema kifo cha Ruge kimewagusa wananchi wengi kutokana na namna alivyojitolea kuwaunga mkono vijana nchini.



Chanzo: mwananchi.co.tz