Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

VIDEO: Penalti ya Bocco gumzo

Mon, 8 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Maelfu ya mashabiki wa Simba waliofurika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam hawakuamini kilichotokea baada ya timu yao kushindwa kupata ushindi dhidi ya TP Mazembe ya DR Congo huku nahodha John Bocco akigeuka gumzo.

Gumzo kubwa katika mchezo wa jana, alikuwa Bocco aliyekosa mabao mawili na kukosa mkwaju wa penalti.

Dakika ya 59 Simba ilipata penalti baada ya Meddie Kagere kupiga krosi ambayo beki wa TP Mazembe alishika ndani ya boksi na mwamuzi Mustapha Gharbal kutoka Algeria aliamuru pigo hilo.

Bocco ambaye aliyefunga mabao matatu katika Ligi ya Mabingwa Afrika, alipaisha penalti na kuwafanya maelfu ya mashabiki kushika vichwa wasiamini kilichotokea kwa mshambuliaji huyo.

Pamoja na kukosa penalti, Bocco amekuwa msaada mkubwa kwa Simba katika mechi zote tangu kuanza kwa mechi za hatua ya awali katika mashindano hayo msimu huu.

Mashabiki wa Simba waliokuwa na kiu ya kuendeleza ushindi katika mechi za Ligi ya Mabingwa Afrika, walitoka uwanjani wasiwe na furaha baada ya suluhu hiyo.

Simba iliyoilaza AS Vita ya DR Congo mabao 2-1, ilishindwa kugusa nyavu za TP Mazembe, baada ya washambuliaji wake kushindwa kutumia vyema nafasi walizopata.

Matokeo hayo yameiweka Simba katika hali ngumu katika mchezo wa marudiano utakakaofanyika Lubumbashi, Aprili 13, saa 10:00 jioni.

Pamoja na suluhu hiyo, Simba bado ina nafasi ya kusonga mbele endapo itapata sare ya mabao yoyote yale lakini kinyume cha hapo, itakuwa safari imemalizika na kurejea kumalizia viporo vya Ligi Kuu Tanzania Bara.

Ingawa Simba haikupoteza mchezo huo, mashabiki wake walionekana kupigwa na butwaa na idadi kubwa walishindwa kushuka majukwaani kwa kuwa walizoea kushangilia ushindi mara zote kwenye uwanja huo tangu mechi za hatua ya awali za timu hiyo.

Mchezo ulivyokuwa

TP Mazembe ilitangulia kutengeneza nafasi dakika ya nne baada ya nyota wake Jackson Muleka kukosa bao akiwa katika nafasi nzuri alipomlamba chenga beki Pascal Wawa, lakini alishindwa kuweka mpira wavuni.

Muleka baada ya kumpiga chenga kipa Aishi Manula alijidondosha na mwamuzi Gharbal kutoka Algeria alimuonya kwa kadi ya njano.

Dakika ya sita Wawa hakuendelea na mchezo baada ya kuumia na nafasi yake kujazwa na beki Mganda Juuko Murshid.

Simba ilibadilika na dakika ya 15 beki Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ alipiga kiki kali akiwa katika nafasi nzuri lakini ilipaa.

Simba ilitengeneza mashambulizi na dakika 31 beki Zana Coulibaly alipiga mpira wa krosi uliomkuta Kagere ambaye alipiga ‘tik tak’ iliyogonga mwamba.

Hata hivyo, viungo Clatous Chama na Haruna Niyonzima walishindwa kupenyeza mipira kwa akina Bocco na Kagere ambao walikuwa wakihaha kutafuta mabao.

Mabeki wa TP Mazembe Kelvin Mondeko na Chongo Kabaso walikuwa makini hasa kwa Kagere na Bocco ambao walikuwa wakiingia mara kwa mara ndani ya eneo lao la hatari.

Umbo refu la Mondeko lilimnyima fursa Kagere kucheza mipira ya juu iliyopigwa na viungo wa Simba, hivyo alilazimika kucheza pasi za chini.

Dakika ya 54 Simba ilimtoa Chama na kuingia Emmanuel Okwi kwenda kuongeza nguvu katika eneo la ushambuliaji. Pia TP Mazembe ilimtoa Rainford Kalaba na kuingia Mechak Elia.

Dakika 53, Bocco alikutana uso kwa uso na kipa wa TP Mazembe Sylvain Gbohouo lakini alipiga mpira ambao ulipanguliwa na kipa huyo.

Dakika ya 84 Simba ilipata faulo ambayo ilipigwa na Okwi, lakini kiki yake ilitoka nje na dakika ya 90 TP Mazembe ilikosa bao baada ya mpira uliopigwa uligonga mwamba.

Kocha wa Simba Patrick Aussems alisema kutopata matokeo nyumbani si jambo jema, lakini wanajipanga kwa mechi ya marudiano na mkakati wake ni kushinda ugenini pia. Alisema Simba ina nafasi ya kufuzu nusu fainali kwa kupata ushindi katika mechi ya marudiano mjini Lubumbashi.

“Tulipata nafasi za kufunga lakini ndio hivyo. Nakubaliana na kiwango cha wachezaji wangu walicheza vizuri kwa kufuata maelekezo yangu,” alisema Aussems raia wa Ubelgiji..

Kwa upande wake kocha wa TP Mazembe, Mihayo Kazembe alisema haukuwa mchezo rahisi na mashabiki wameshuhudia mechi yenye ushindani.

“Tunarudi Lubumbashi kwa maandalizi mengine, tunakwenda kujipanga kwa kuongeza nguvu ili tupate ushindi katika mechi yetu ya marudiano,” alisema Kazembe.



Chanzo: mwananchi.co.tz