Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

VIDEO: Migogoro tangu wacheza chandimu hadi Yanga ya sasa

Thu, 21 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Taja jina la ‘Yanga’ sehemu yoyote, na mwitikio wake utakuwa ‘Daima Mbele, Nyuma Mwiko’ ama ‘Yanga Imara Daima’. Katika umri wa miaka zaidi 80, iwe katika uhai wa mwanadamu au taasisi, ni umri mkubwa na wa heshima ya aina yake. Yanga siyo tu mojawapo ya klabu kongwe zaidi Afrika Mashariki, bali Afrika kwa ujumla.

Yanga ndio mabingwa wa kihistoria wa ligi ya soka Tanzania tangu ilipoanzishwa rasmi mwaka 1965 ikiwa imenyakua ubingwa Ligi Kuu Bara mara 27.

Haya ni mafanikio makubwa katika soka la nyumbani, lakini mbali ya michuano ya ukanda wa Afrika Mashariki na Kati ambayo imenyakua mataji mara tano, Yanga haijawahi kufanya lolote la kujivunia sana katika Bara la Afrika, japokuwa imeshiriki mara nyingi katika Kombe la Klabu Bingwa Afrika sasa Ligi ya Mabingwa Afrika, mara mbili katika Kombe la Washindi Afrika ‘Mandela Cup’ (ambalo sasa limefutwa), pia katika Kombe la CAF (sasa Kombe la Shirikisho).

Inaelezwa kwamba, mwaka 1926, makundi ya vijana wa Dar es Salaam yaliyokuwa na kawaida ya kujumuika katika viwanja vya kuchezea mpira vya Jangwani waliamua kuunda timu waliyoipachika jina la Jangwani.

Leo hii siyo rahisi kwa klabu kukosa hata mpira wakati wa kuanzishwa kwake. Lakini haikuwa hivyo kwa Jangwani Boys. Watu wale 20 walioanzisha klabu hiyo hawakuwa wanajua wapi au namna gani wangepata mpira wa kuchezea ama jezi. Zama zile viatu vya kuchezea mpira vilikuwa ni msamiati mgeni kwa Waafrika. Iliwachukua miezi kadhaa kwa Jangwani Boys kupata mpira halisi, lakini kabla ya hapo walikuwa wakitumia mpira wa makaratasi (ndiki).

Wachezaji wengi wa Yanga wa miaka ya 1920 na 1970 walikuwa ni wafanyakazi wa Bandari. Kutokana na sababu hii mwaka 1928 wakajiita Navigators na ikawa timu ya kuheshimiwa miongoni mwa timu za Waafrika mjini Dar es Salaam kutokana na uwezo wake uwanjani.

Hata hivyo, mwaka 1929 kukatokea kutokuelewana baina ya wanachama na wachezaji ambapo baadhi yao, wakiongozwa na wale wenye asili ya Kiasia, wakajitenga na kuanzisha klabu ya Sunderland (sasa Simba). Hapo ndipo uhasama ulipoanza baina yao.

Baada ya kucheza kwa kutumia jina la Navigators kati ya mwaka 1928-1929, timu hiyo ilibadili jina na kujiita Taliana, baadaye ikajiita New Youngs hadi ilipobadili na kujiita Young Africans mwaka 1935.

 

MASHINDANO

Katika miaka ya mwanzoni mwa 1930 ilifanikiwa kucheza Ligi Daraja la Pili Kanda ya Pwani iliyokuwa ikisimamiwa na Chama cha Ligi ya Soka cha Dar es Salaam - DFLA, ambacho kilianzishwa mwaka 1926. Baadaye ikatwaa Kombe la Kassum. Makao yao sasa yalikuwa yamehamia kwenye Mtaa wa Ndovu hadi mwaka 1969 walipohamia katika Mtaa wa Mafia na Nyamwezi baada ya kununua nyumba kwa shilingi 12,000/=.

Yanga wakati huo ilikuwa na wachezaji maarufu kama makipa Taha Athumani Hussein na Abdulhamid Ramadhan ambaye alitambulika sana kimataifa baada ya kuisaidia Tanganyika kutwaa ubingwa wa Gossage ilipozishinda Kenya na Uganda mwaka 1949, 1950 na 1951. Wachezaji wengine walikuwa Saidia Msafiri, Jamil Ramadhan, Mtoro Ramadhan ‘Meja’, Mambo Mzinga, Hafidh Ahmed, Isihaka Mzee, Juma Shaaban, Omari John, Hatibu Mtoto na Juma Mbimb.

Yanga ilianza kuimarika zaidi mwanzoni mwa miaka ya 1940, ambapo mwaka 1942 ilitwaa Kombe la Sunlight (sasa Taifa Cup) lililokuwa likishindaniwa na timu za Majimbo wakati wa ukoloni pamoja na klabu kadhaa zilizopenda kushiriki.

Mwaka 1948 Yanga ikaanza kutumia rangi za njano na kijani, ambazo hadi leo ndizo alama zake. Katika miaka ya 1960 Yanga ilitwaa vikombe mbalimbali kama; Healtho, Afro-Shirazi, Ukombozi, Mapinduzi (Wananchi) Zanzibar, Kombe la TAAA, Kombe la Songambele, Kombe la Nyota, Ngao ya Chama cha Soka Tanzania, Kombe la Dereva Teksi, Kombe la Mei Mosi, Kombe la Share, Kombe la Maendeleo na mengineyo.

Ilitwaa Ubingwa wa Taifa kwa mara ya kwanza baada ya kuwachapa mahasimu wao wakubwa katika soka, Sunderland, mabao 5-0 katika mchezo wa mwisho Juni 1, 1968.

Huu ulikuwa mwanzo wa mafanikio ya miaka mitano katika ligi ya nyumbani na michuano ya kimataifa hasa kwenye Kombe la Kwame Nkrumah (sasa Ligi ya Mabingwa Afrika). Mwaka 1969 Yanga ilitwaa ubingwa wa Pwani na Ubingwa wa Taifa kama ilivyofanya miaka ya 1970, 1971 na 1972. Baada ya kutibuliwa mwaka 1973 na Simba, Yanga ilitwaa tena Ubingwa wa Taifa mwaka 1974.

Mwaka 1970 ikatangazwa kwamba klabu hiyo ingekuwa na jengo lake la ghorofa mbili kwenye makutano ya mitaa ya Twiga na Jangwani mjini Dar es Salaam. Mpango huo ukapewa msukumo mkubwa na kupata msaada wa shilingi milioni mbili kutoka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya Rais Sheik Abeid Amani Karume ukiwa ni mchango wa klabu ya Wananchi yaani African Sports Club.

Uwanja wa nyumbani wa Yanga, Kaunda Stadium, ulianza kujengwa mwaka 1973 kwa gharama ya shilingi milioni 3 ambazo zilipatikana kwa michango kutoka kwa taasisi mbalimbali na wahisani wengine. Uwanja huo ulikadiriwa kuingiza watazamaji 14,000.

 

MIGOGORO

Kama kuna mgogoro ambao ungeweza kuibomoa kabisa Yanga basi ulitokea mwaka 1976. Yanga ikawafukuza wachezaji 21 wa kutegemewa. Kutokana na sababu hii, Yanga chini ya kocha mzalendo Percival Peter Mandawa, haikuwa imara na mwaka 1977 ikajikuta ikichabangwa mabao 6-0 na mahasimu wao wa jadi, Simba katika mechi ya ligi. Na tangu hapo haikufanya vizuri hadi mwaka 1981 ilipotwaa ubingwa wa ligi kufuatia matokeo ya suluhu na Pan African.

Mgogoro ukaibuka tena mwaka 1986, ambao uliisababishia Yanga ishindwe kuutetea ubingwa wake mwaka huo. Mgogoro huo ulipamba moto zaidi mwaka 1987, huku pande mbili zikiwa zinapingana. Upande wa uongozi ulikuwa unajiita Yanga-Ukuta na upande wa wanachama waliokuwa wakiupinga uongozi walijiita Yanga-Katiba.

Mwaka 1994 ukatokea mgogoro mwingine mkubwa ambapo wanachama walitaka klabu iwe kampuni huku wafadhili wakipinga. Uongozi ukawafukuza baadhi ya wachezaji.

Mwaka 1996 ukatokea mgogoro tena na kuzaliwa kundi la wanachama lililojiita ‘Mau Mau’ ambalo lilikuwa likiupinga uongozi. Vita ya makundi ikaendelea na baadaye kuzaliwa makundi ya Yanga Asili na Yanga Academia, mgogoro ambao ulikuja kumalizwa mwaka 2002.

Hii ndiyo Yanga mabingwa mara 27 wa Ligi Kuu Bara sasa wapo kwenye mgogoro wa kiuongozi baada ya mwenyekiti wao Yusuf Manji kutangaza kujizuru.



Chanzo: mwananchi.co.tz