Dar es Salaam. Ofisa Habari wa Ruvu Shooting, Masau Bwire amesema hakuwa na lengo la kuwafyatulia bastola au kuwadhuru mashabiki wa Yanga waliokuwa wanamzonga juzi baada ya kumalizika kwa mchezo baina ya timu hizo mbili.
Heritier Makambo ndiye aliyepeleka kilio Ruvu Shooting baada ya kuifungia timu yake bao la ushindi dakika ya 94 na kufanya matokeo kumalizika Yanga ikishinda 3-2.
Baada ya mchezo huo, mashabiki wengi wa Yanga waliimvamia Bwire na kuanza kumzonga wakati akielekea katika gari lake.
Tukio hilo lilitokea juzi mara baada ya mchezo huo kumalizika ambapo mashabiki hao wa Yanga waliokuwa wakishangilia ushindi wao ghafla wakakutana na Bwire akiwa anaelekea eneo ambalo aliegesha gari yake.
Wakati mashabiki hao wakimzonga Bwire wakimdhihaki kwa timu yake kukubali kipigo mwisho msemaji huyo akionekana kubadilika kwa kuwa mkali.
Wakati tukio hilo likiendelea ghafla Bwire alijikuta akitoa bastola yake ubavuni kushoto na walipoiona wakakimbia.
Baada ya kutoa bastola hiyo Bwire alipata upenyo na kukimbilia katika gari yake huku akionekana kuchukizwa na tukio la kuzongwa na mashabiki hao.
Hata hivyo Kamishina mstaafu wa Jeshi la Polisi, Jamal Rwambo alilazimika kumsihi Bwire kupunguza hasira kisha msemaji huyo kuondoka haraka eneo la kuegesha magari.
Bwire alisema hakuwanyooshea bastola mashabiki wa Yanga na kama kuna mtu alifanyiwa kitendo hicho ajitokeze hadharani aseme.
“Kweli nilikuwa na bastola nje ya uwanja na wakati natoka, mashabiki walinivamia, walinizingira na kunizongazonga kiasi cha wengine kuanza kunipapasa mifukoni, wakaniibia na simu yangu.
“Baada ya kuona mashabiki wamezidi na wanadiriki hata kunisachi mifukoni, kweli nilikuwa na bastola niliweka sehemu ambayo nilijua sasa wanaweza hata kuichukua (ubavuni kushoto) ikabidi niitoe niishike mkononi ambapo niliona ni sehemu salama zaidi na ndio maana nilipoitoa tu nikatoka spidi na kwenda kwenye gari baada ya kuona nimepata njia.
“Sikuitoa bastola kwa lengo kumtishia au kumdhuru mtu na kama ningekuwa na lengo hilo basi ningefyatua juu ila wakati naitoa mahali ilipokuwepo mwanzo ili niishike mkononi ndio labda wengine waliona wakaogopa,”alisema Bwire.
“Hata Kamishina mstaafu wa Jeshi la Polisi, Jamal Rwambo alikuwepo pamoja na mwenyekiti wa Sputanza, Mussa Kissoky walishuhudia tukio na wanajua sikuwa na lengo ambalo wengi walifikiria.
Alipotafutwa Kamanda wa Polisi Kanda Malumu ya Dar es Salaam,Lazaro Mambosasa ili aliongelee suala hilo, simu yake ilipokewa na msaidizi wake ambaye alisema kamanda yuko bize katika maadhimisho ya miaka 50 ya Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) ambapo mgeni rasmi alikuwa Rais John Magufuli.