Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

VIDEO: Kagere alivyofunika Simba Day Taifa

Wed, 7 Aug 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Klabu ya Simba imewafurahisha mashabiki wake baada ya kuilaza Power Dynamos ya Zambia mabao 3-1 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, yakifungwa na Meddie Kagere.

Mashabiki wa Simba, jana waliujaza uwanja huo unaochukua jumla ya watazamaji 60,000 wakiwa wamekaa katika kilele cha tamasha lao la Simba Day.

Simba ni kama imejibu mapigo kwa watani wao wa jadi Yanga ambao Jumapili iliyopita waliujaza uwanja huo katika mchezo wao wa Siku ya Mwananchi waliotoka sare ya bao 1-1 na Kariobang Sharks ya Kenya.

Mfungaji bora wa timu hiyo, Meddie Kagere, alifunga bao la kwanza dakika ya pili kwa kiki ya mguu wa kulia, akitumia vyema makosa ya kipa wa Dynamos, Lawrence Mulenga.

Kivutio katika mchezo huo alikuwa Msudani Sharaf Shiboub ambaye alionyesha ufundi wa kucheza na mpira na kutoa pasi zilizofika kwa wachezaji wenzake.

Shiboub aliyechukua nafasi ya Mghana James Kotei, alimudu kucheza nafasi ya kiungo mkabaji na mara kwa mara alionekana akitumia nguvu.

Pia Soma

Pamoja na ubora wake, Shiboub alipata upinzani kutoka kwa kiungo wa Dynamos, Benson Sakala, aliyekuwa akitibua mipango yake mara kwa mara.

Mchezaji mwingine aliyekuwa kivutio ni nyota wa zamani wa TP Mazembe ya DR Congo, Deo Kanda ambaye alionyesha uwezo binafsi wa kuchezea mpira lakini hakuwa na madhara langoni mwa wapinzani wao.

Ngome ya Simba chini ya Pascal Wawa na Tairone Santos da Silva haikuwa na muunganiko mzuri na mara kadhaa walionekana wakitoa mwanya kwa wapinzani wao kusogea langoni mwao.

Dakika 15 za kipindi cha kwanza mpira ulichezwa zaidi katikati ingawa Simba mara kadhaa ilimtumia kiungo wa pembeni Francis Kahata kupitisha mipira upande wa kulia.

Dynamos ilibadili upepo uwanjani dakika ya 24 baada ya kupata bao la kusawazisha lililofungwa na Jimmy Dlingai kwa mpira wa kichwa uliomshinda kipa Beno Kakolanya, akiunganisha kona iliyochongwa na Konchwani Chibori.

Licha ya Simba kupata kona nne kipindi cha kwanza zilizopigwa na Clatous Chama hazikuwa na faida kulinganisha na Dynamos iliyopiga moja waliyofunga bao.

Pia Kagere hakuwa na makali kwani aliruhusu mabeki wa Dynamos kuwahi mipira iliyopigwa kwake na Mzamiru Yassin, Kanda, Kahata au Chama.

Simba iliweka kambi kwa muda langoni mwa Dynamos na dakika ya 58 ilipata bao la pili lililofungwa na Kagere kwa kichwa akiunganisha mpira wa krosi uliopigwa na Kanda. Simba ilifunga bao la tatu dakika ya 72 lililofungwa na Kagere akipata pasi ya Chama na dakika mbili baadaye Kahata alitoka na kuingia Rashid Juma.

Awali, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliyekuwa mgeni rasmi, aliwataka viongozi wa klabu na vyama vya michezo kujenga mifumo bora ya kuvipatia mapato.

Simba: Beno Kakolanya, Shomari Kapombe, Mohammed Hussein, Tairone Santos da Silva, Pascal Wawa, Mzamiru Yassin, Deo Kanda, Sharaf Shiboub/Gerson Vieira, Meddie Kagere, Clatous Chama na Francis Kahata/Rashid Juma.

Power Dynamos: Lawrence Mulenga, Larry Bwalya, Raphael Makubali, Jimmy Dlingai, John Soko, White, Mwambaba, Benson Sakala, Konchwani Chibori, Christian Ntiba, Fredirick Mulamba na Kassim Titus.

Chanzo: mwananchi.co.tz