Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

VIDEO: Hesabu zashikilia ushindi Simba

Wed, 28 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Baada ya maandalizi mazito nje ya uwanja, hesabu na mbinu sahihi ndani ya dakika 90 dhidi ya Mbabane Swallows ya Swaziland leo, zimeshikilia ndoto na mipango ya Simba kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu.

Simba haijashiriki mashindano hayo kwa miaka mitano mfululizo tangu ilipoondolewa kwa aibu na Recreativo do Libolo ya Angola kwenye hatua ya awali mwaka 2013 kwa kipigo cha jumla cha mabao 5-0 ikifungwa 1-0 nyumbani na kupoteza mabao 4-0 ugenini.

Simba ina kila sababu ya kuhakikisha inautumia vyema mchezo wa nyumbani ili kujiweka katika mazingira mazuri ya kufuzu raundi ya kwanza ya mashindano hayo msimu huu.

Ikiwa na kikosi kilichokamilika kila idara, uzoefu wa kutosha unaobebwa na rekodi tamu kimataifa, Simba ina deni la kuibuka na ushindi mnono kwenye Uwanja wa Taifa ili kuweka hai ndoto zake za kufika mbali kwenye mashindano hayo.

Wakati Mbabane ikiwa imeshiriki katika mashindano ya Afrika kwa ngazi ya klabu mara tisa tangu ilipoanzishwa, Simba imecheza mara 24.

Mafanikio makubwa ya Mbabane ni kucheza hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho Afrika mara mbili, Simba imefuzu hatua ya makundi mara moja mwaka 2003, kucheza fainali ya Kombe la CAF mwaka 1993 na kucheza nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 1974.

Simba imekuwa tishio inapokutana na timu kutoka Kusini mwa Afrika katika hatua kama hizi za mwanzoni ikiwa nyumbani ambapo katika mechi 10 kuanzia mwaka 2000 imeshinda mara saba, kutoka sare moja na kufungwa mbili, ikipachika mabao 18 na kuruhusu saba.

Katika mechi hizo 10 imefunga mabao 22, imefungwa sita. Kipigo kikubwa ilichokitoa ni mabao 4-0 dhidi ya Elab Club ya Comoro na Gendarmarie Nationale ya Djibout. Kichapo kikubwa ilichopokea ni mabao 3-2 kutoka kwa TP Mazembe mwaka 2011.

Ndani ya uwanja Simba ina kikosi kipana na tishio hasa katika safu ushambuliaji inayoongoza kwa kufunga mabao kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara. Simba imefunga mabao 23 katika mechi 12 ilizocheza, pia ina safu imara ya ulinzi ambayo inashika nafasi ya pili kwa kuruhusu mabao manne nyuma ya Azam FC iliyofungwa matatu. Tofauti na Mbabane ambao hawako sawa kwenye Ligi ya Swaziland ambapo wamefunga mabao matano na kufungwa matatu katika mechi tano.

Simba ina nafasi ya kumaliza biashara mapema na kuigeuza mechi ya marudiano Swaziland kama sehemu ya maandalizi ya mchezo wa raundi ya kwanza ambayo inaweza kuwakutanisha na mshindi wa jumla baina ya Nkana Red Devils ya Zambia au UD Songo ya Msumbiji.

Sifa kubwa ya Mbabane inapokuwa ugenini inacheza soka la kufunguka na kujaribu kuwalazimisha wapinzani wasivuke nusu ya uwanja, jambo ambalo limekuwa likiwawezesha kupata matokeo mazuri inapocheza mechi ya marudiano nyumbani.

Mechi zote tano ambazo Mbabe imecheza ugenini kwenye mashindano ya kimataifa mwaka 2017 na 2018 imefungwa mabao matano.

Mshambuliaji Felix Badenhorts ndiye mtu wa kuchungwa, ndiye tegemeo lao kwenye mashindano ya kimataifa akiwa amefunga mabao manne kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika msimu 2018.

Mwingine ni Sabelo Ndzinisa ambaye katika mechi tisa za mwisho alizoichezea timu hiyo amefunga mabao matano.

Kocha wa Simba, Patrick Aussems amesema maandalizi yamekwenda vizuri na mpango ni kucheza kwa umakini kuanzia safu yao ya ulinzi hadi ushambuliaji.

“Tumejiandaa muda mrefu, tunategemea kuanza vizuri mchezo wetu wa kwanza tutashambulia na kujilinda kwa umakini wa kutosha,” alisema Aussems.



Chanzo: mwananchi.co.tz