Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

VIDEO: Bondia Mwakinyo atua Mwananchi na kupata zawadi

Video Archive
Wed, 27 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Bondia Hassan Mwakinyo amesema heshima aliyopewa na Kampuni ya Mwananchi Communication Limited (MCL) haijawahi kutokea.

Mwakinyo alifanya ziara ya saa moja makao makuu ya Mwananchi jijini Dar es Salaam amesema, kampuni hiyo imempa heshima ambayo hakuitarajia.

"Watu wengi maarufu wamewahi kutembelea Mwananchi, lakini sikuwahi kuona wamepewa zawadi, ila mimi," alisema Mwakinyo kwa hisia ofisi hapo.

Bondia huyo ambaye aliwasili Mwananchi saa 5:06 akiwa ameambatana na wadhamini wake kutoka kampuni ya SportPesa Tanzania alitembelea vitengo mbalimbali ndani ya ofisi hiyo ikiwamo HR, Utawala, studio za MCL Digital, Maktaba ya Mwananchi, Kitengo cha Michezo (Sports Unit) na kuingia kwenye kikao cha Wahariri na vitengo vingine tofauti vya habari.



"Sijui niseme nini, lakini Mwananchi imenipa heshima, katika ofisi hii wanakuja watu wengi maarufu hawajawahi kupewa zawadi, lakini mimi," alisema Mwakinyo kwa hisia alipoingia kwenye kikao cha wahariri wa MCL.

Awali Mwakinyo alimtembelea Mhariri Mtendaji Mkuu wa MCL, Bakari Machumu alimpongeza kwa hatua aliyofikia kwenye ngumi huku akimtania namna alivyomtisha mpinzani wake, Sergio Gonzalez kwenye pambano la nchini Kenya.



"Wakati mpinzani wako akiwa chini, ulikuwa kwenye kamba za ulingo kwa stahili ya kupata mzuka wa kutaka kuzichapa kwanini ulifanya vile? Machumu alimuuliza Mwakinyo ambaye alisema ile ilikuwa moja ya mbinu za kumtisha mpinzani wake kwani alimuonyesha yeye (Mwakinyo) bado yuko fiti na kama Gonzales atasimama basi atamuua na kweli mpinzani wake hakurudi.

Bondia huyo pia alimtembelea mkuu wa Kitengo cha Michezo (Mcl Sports Unit), Ndaya Kasongo kabla ya kumalizia ziara yake kwenye ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa MCL, Francis Nanai.

"Haijawahi kutokea, Mwananchi mmeniheshimu, nafarijika kwa hilo na niwaahidi tu kwamba nitapambana zaidi ili nitimize ndoto zangu," amesema.

Katika mahojiano maalumu, Mwakinyo alibainisha kwamba bado ana safari ndefu kwenye ngumi na ndoto zake ni kufika levo ya mabondia kama Floyd Maywether, Manny Pacquiao na wengine wanaofanya vizuri duniani.

Mkurugenzi MCL atoa neno kwa Mwakinyo

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Mwananchi Communication Limited (MCL), Francis Nanai amesema kampuni hiyo itaendelea kushirikiana na Bondia Hassan Mwakinyo.

Nanai alitoa kauli hiyo alipotembelewa na bondia huyo ofisini kwake.

Mwakinyo alipewa zawadi mbalimbali ikiwamo fedha na magazeti yanayochapishwa na kampuni hiyo ya Mwananchi, Mwanaspoti na The Citizen.

Katika ziara hiyo, Nanai alimpongeza Mwakinyo kwa kuiletea sifa nchi katika masumbwi akisisitiza kuwa MCL itaendelea kufanya kazi na bondia huyo.

"Niliangalia pambano lako la Kenya ngumi ulizomchapa yule jamaa, sio za kawaida, hongera sana.

"Tutaendelea kushirikiana zaidi na zaidi kwani lengo la Mwananchi ni kuona Tanzania inafanya vizuri katika nyanja mbalimbali, tumefanya kwa Taifa Stars na sasa ni kwako, hii ni zamu yetu," alisema Nanai.



Bondia huyo namba moja nchini kwenye uzani wa super welter alisema amefarijika kukutana na mkurugenzi huyo na kumuahidi kuendelea kufanya mazuri zaidi kwenye ngumi.

Huku akifurahia zawadi mbalimbali kutoka kwa Nanai, Mwakinyo alisema zimemuongezea hamasa na kuamini kwamba Mwananchi imeendelea kutambua kipaji chake tangu hajacheza pambano la Uingereza lililompa umaarufu.

Hassan Mwakinyo: Mimi siyo Super Star

Licha ya umaarufu wa bondia Mwakinyo amesema bado hajawa maarufu.

Amesema yeye ni mtu wa kawaida na bado ana safari ndefu zaidi ili aweze kutimiza ndoto ya kuwa 'super star'.

"Mimi ni mtu wa kawaida sana, siyo star kama ambavyo watu wengi wamekuwa wakinichukulia," amesema Mwakinyo.



Amesema kuna wakati baadhi ya watu waliomzunguka wamekuwa wakimtaka kutofanya baadhi ya mambo kwa kuwa yeye ni maarufu.

"Nimekuwa nikiwambia bado sijawa maarufu kama ambavyo wao wanafikiria, bado mimi ni mtu wa kawaida ambaye nina ndoto za kuwa maarufu," amesema.



Chanzo: mwananchi.co.tz