Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

VIDEO: Azam, Simba vita iko hapa Ligi Kuu

Video Archive
Wed, 4 Mar 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mabeki wa Azam leo wana kazi kubwa mbele ya washambuliaji wa Simba timu hizo zitakapocheza mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Mchezo huo unakuwa wa 24 kwa timu hizo kukutana katika Ligi Kuu tangu Azam ilipopanda daraja mwaka 2008, pia ni mara ya pili msimu huu kuvaana baada ya mzunguko wa kwanza Simba kushinda bao 1-0.

Safu ya ulinzi ya Azam inayoongozwa na kipa Mghana, Razack Abalora, Nicolas Wadada, Bruce Kangwa, Aggrey Morris, Yakub Mohammed na Daniel Amoah imeruhusu mabao manane katika michezo 10 ya hivi karibuni hivyo inaonyesha inafungika kirahisi.

Katika michezo hiyo Azam imefunga mabao 11 ikiwa ni wastani wa bao moja kila mchezo wakati Simba imepachika 21.

Mabeki wa Azam wanatakiwa kuwa makini dhidi ya Meddie Kagere mwenye mabao 14, Francis Kahata (4), Deo Kanda (4) kila John Bocco (3) na Luis Miquissone (2). Azam itapata ugumu kwani Simba pia ina rekodi nzuri ya kufunga mabao kupitia wachezaji wa viungo na hilo limedhihirika kwa Hassan Dilunga mwenye mabao sita.

Pia kitendo cha Luis kufunga katika mechi mbili mfululizo za ligi kitaongeza kasi katika safu ya ushambuliaji ya Simba hivyo kuwapa wakati mgumu mabeki wa Azam. Hata hivyo Simba nayo inapaswa kuwa makini na Obrey Chirwa ambaye ndio mfungaji bora wa Azam akiwa amefunga mabao manane.

Pia Soma

Advertisement
Chirwa amekuwa katika kiwango bora msimu huu akishirikiana na Shabani Chilunda, hivyo wachezaji hao leo ndio wanabeba matumaini ya Azam.

Aidha, Simba inaingia katika mchezo huo ikiwa na rekodi bora dhidi ya Azam katika mechi zao zote walizocheza.

Tangu mwaka 2008 Azam imekutana na Simba mara 23 na wapinzani wao wameshinda mara 10, yenyewe mara sita na zimetoka sare michezo saba.

Ugumu wa mchezo huo pia umezungumzwa na mshambuliaji wa Azam Idd Kipagwile aliyesema Simba ni timu ngumu, lakini wanakwenda uwanjani kupambana.

“Simba ni timu nzuri ukiangalia safu ya ushambuliaji ina muunganiko mzuri, lakini na sisi tumejipanga kuwakabili kwasababu tunataka pointi tatu, ”alisema Kipagwile.

Wakati Kipagwile akieleza ugumu huo, nahodha wa Simba, John Bocco alisema watahakikisha wanashinda mchezo huo ili kuongeza morali ya kuwakabili watani zao wa jadi Yanga Jumapili wiki hii.

“Tumejiandaa vizuri kushinda kwasababu tunataka pointi tatu ili tuendelee kuongoza ligi na kukaribia kutwaaa ubingwa. Pia ushindi utatupa morali tunapoelekea mechi yetu na Yanga,”alisema Bocco.

Azam inavaana na Simba ikiwa nafasi ya pili kwa pointi 48 na wapinzani wao wanaongoza ligi kwa pointi 65.

Chanzo: mwananchi.co.tz