Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Uwanja unavyowatesa viongozi Simba

10346 Pic+uwanja TanzaniaWeb

Mon, 6 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Achana na Tamasha la Simba Day litakalofanyika Agosti 8 kwenye Uwanja wa Taifa, hilo lipo, lakini kuna hili, makocha wa klabu ya Simba wameueleza uongozi wa klabu ya Simba kwamba hawataki kusikia wanacheza mazoezi kwenye viwanja vibovu visivyo na hadhi.

Mara kadhaa, makocha wamekuwa wakiwalazimisha kama si kuwakatalia viongozi viwanja vya mazoezi kwa kuwa havina ubora na vinasababisha majeraha kwa wachezaji na wakati mwingine kusababisha tatizo la enka.

Kwa muda mrefu sasa, Simba imekuwa ikihaha uwanja wa mazoezi na kufikia hatua ya ‘kudandadanda’ kwenye viwanja vya wengine kama ule wa Boko Veterans au Polisi Kurasini na wakati mwingine viwanja vya Gymkhana, Dar es Salaam. Gharama za kutumia uwanja wa Boko ni Sh300,000 kwa siku.

Kaimu Rais wa klabu ya Simba, Abdallah Salim ‘TryAgain’ anakiri kusema kati ya mambo yanayowaumiza kichwa ni suala la Simba kukosa uwanja, lakini akasema mwezi huu haumaliziki kwa kuwa makocha wamekuwa wakiwasumbua.

TryAgain anasema kuwa kuna suala la kesi ambalo liko mahakamani na hataki kulizunguzia na kwamba kwa mwelekeo wake, mambo yanaweza kufunguka na wakapata njia ya uwanja.

“Ninachotaka kusema ni kwamba watu wawe na subira, mwezi huu wa nane haumaliziki, tukimaliza Simba Day tunakwenda Bunju, hilo ndilo tunalotaka kulifanya kwa sasa, Simba klabu kubwa lazima kuwa na uwanja wake,” anasema.

Anasema makocha hawataki kupeleka wachezaji kwenye baadhi ya viwanja kwa kuwa havina ubora na akasema viwanja vizuri ni gharama hivyo ni wakati sasa Simba kupunguza ama kuondoa gharama hizo kwa kujenga uwanja wa kisasa wa Bunju.

Simba imekuwa ikihangaika uwanja wa mazoezi na huwa inatumia Uwanja wa Boko Veterans kwa ajili ya mazoezi ambao hutozwa Sh300,000 kwa siku.

Mikakati ya Uwanja wa Bunju

Uongozi wa klabu ya Simba kwa sasa upo katika maandalizi ya tamasha kila mwaka la Simba Day, sasa baada ya tamasha hilo, Simba itaanika mikakati ya ujenzi wa uwanja wao wa mazoezi huko Bunju nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam.

Jambo hilo litakalomaanisha kuwa muda si mrefu ujao klabu hiyo itaachana na viwanja vya kukodi kwa ajili ya mazoezi, mechi za kirafiki na zile za mashindano.

Klabu hiyo inayoshikilia taji la ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, kwa sasa inakaribia kujivunia uwekezaji uliofanywa na bilionea kijana Mohammed Dewji ‘MO’ ambaye amekuwa akimwaga pesa katika kufanikisha mambo ya kimaendeleo.

Akisisitiza hilo, Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Simba, Said Tully naye amefunguka kwa kirefu kwa kubainisha kuhusu mpango wa kuanza ujenzi wa uwanja wao uliopo Bunju.

Tully anakiri kuwa kwa sasa wapo katika mchaka mchaka kwa ajili ya kufanikisha Simba Day, lakini wakimaliza watatoa tamka rasmi kuhusiana na maandalizi ya ujenzi huo.

Anadokeza kuwa katika ujenzi wa uwanja huo itahusisha uwanja wa mazoezi wa timu ya wakubwa, uwanja wa timu ya vijana wadogo, nyumba za kuishi wachezaji wanapokuwa kambini yaani Hosteli, sehemu ya kulia chakula, vyumba vya huduma ya kwanza na ukumbi wa mikutano.

Anasema ujenzi huu utachukua sehemu ndogo tu ya eneo lao lililopo Bunju na kwamba hapo baadaye wanatarajia kujenga uwanja mkubwa ambao utakuwa maalumu kwa mechi za mashindano ikiwemo Ligi Kuu Tanzania Bara na michuano mingine.

“Kama uongozi hili la kujenga uwanja ndilo jambo linalotuumiza vichwa kwa sasa, lipo katika mipango yetu mikuu, tayari tunazo nyasi za bandia kama utazikumbuka zile ambazo zilikwama kipindi kile pamoja na vitu vingine vyote, tukimaliza jambo hili lilitutinga klabu itawaiteni ili kutoa tamko rasmi kuhusu suala la ujenzi,” anasema na kuongeza.

“Mipango ikienda kama tulivyopanga nadhani Simba itakuwa na uwanja wake wa mazoezi wa kisasa na siku si nyingi tamko rasmi litatoka juu ya hili na haraka kazi ya ujenzi itaanza,” anasema Tully.

Anasema kuna mambo wanayaweka sawa upande wao na serikali kuhusu kujenga uwanja huo na wapo katika hatua za mwisho kabisa.

Anaelezea namna wanavyoshindwa kufikia malengo ya timu yao kutokana na kukosa uwanja na wakati mwingine kocha hulazimika kuahirisha program yake ya maandalizi kutokana na kutumia viwanja vya kukodi.

Simba klabu iliyoanzishwa mwaka 1936 hadi leo ingali inategemea viwanja vya kukodi kwa ajili ya mazoezi pamoja na mechi na hutumia Uwanja wa Taifa na ule wa Uhuru kama viwanja vya nyumbani katika kuchezea mechi zake za Ligi na michuano mingine.

Kutokana na kutokuwa na uwanja Simba hulazimika kufanya mazoezi kwa kuhamahama kutokana na sababu mbali mbali, kwa mazoezi imekuwa ikitumia zaidi viwanja vya Chuo cha Bandari, Chuo cha Polisi Kurasini, Klabu ya Gymkhana, White Sands Hoteli na Boko Veterans.

Gharama za kukodi uwanja ni kuanzia Sh 300,000, kwa awamu iwe ni mazoezi ya asubuhi au ya jioni na kama ni mara mbili kwa siku inamaanisha watatumia Sh 600,000 kwa siku kwa uwanja peke yake.

Chanzo: mwananchi.co.tz