Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Utata wagubika sakata la wachezaji wa Lipuli kukamatwa na Polisi, TFF yasema litaondoka na mtu

82321 Pic+lipuli Utata wagubika sakata la wachezaji wa Lipuli kukamatwa na Polisi, TFF yasema litaondoka na mtu

Wed, 30 Oct 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Wakati mechi ya Polisi Tanzania na Lipuli ikitarajiwa kuchezwa saa chache zijazo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Juma Bwire amesema hakuna mchezaji yeyote aliyekamatwa jana na jeshi hilo kama ilivyoelezwa.

Hata hivyo, Katibu wa Chama cha Soka Mkoa wa Iringa, Ally Ngara amedai kuwa wachezaji wa Lipuli walikamatwa na polisi lakini waliachiwa jana jioni.

"Nimeenda mahabusu sijamkuta mchezaji yeyote, Jeshi la Polisi halijakamata mchezaji yeyote huo ni uzushi tu," amesema Kamanda Bwire na kuongeza kwamba amepata taarifa za kuwapo kwa vurugu zilizotokea baina ya timu hizo jana.

Amesema uchunguzi wa Polisi umebaini kwamba chanzo cha mgogoro huo ni timu zote mbili kwenda uwanjani, “kila moja ilikuwa na mambo yake zikagongana… hakuna kingine."

Amesema baada ya mvutano huo hawakufikishana kituoni, “waulizwe vizuri, waliishia huko njiani, hakuna aliyeingizwa kituoni," alisisitiza.

Hata hivyo, Ngara alitofautiana na Kamanda Bwire akidai kuwa uongozi wa Lipuli uliwaita wachezaji klabuni ambako ni kwenye Uwanja wa Samora wakati huo Polisi walikuwa wakifanya mazoezi.

"Awali, Polisi walitaka watu wote watoke uwanjani hadi meneja wa uwanja, kwani walikuwa wakifanya mazoezi pale. Walifanikiwa kuwatoa wakidai wanalinda uwanja, jambo ambalo meneja wa uwanja alilipinga. Jioni Lipuli waliwaita wachezaji wao klabu ambako ni pale uwanjani na Polisi wakaanza kuwafukuza na kuwakamata katika maeneo tofauti na kuwapeleka polisi," amesema.

Alidai kuwa usiku huohuo wachezaji hao waliachiwa lakini kutokana na taharuki ndani ya klabu hiyo ya Iringa, viongozi waliomba mechi hiyo isogezwe mbele lakini viongozi wa chama cha soka cha mkoa walizungumza na TFF na kukubaliana ichezwe.

Alisema katika kikao cha maandalizi, makamu mwenyekiti wa Polisi alieleza kwamba taarifa hizo za kutokea kwa vurugu zilikuwa zinalenga kuwachafua.

"Tuliwaita viongozi wa Lipuli ambao walitaja hadi gari la Polisi lililohusika, lakini tulichobaini Polisi waliowachukua wachezaji wa Lipuli walifanya kwa utashi wao tu, kama ingekuwa ni agizo, kamanda wa mkoa asingetoa ushirikiano," alisema.

Alipoulizwa kuhusu tukio hilo, kiongozi mwandamizi wa TFF ambaye hakutaka jina lake litajwe alisema shirikisho haliwezi kukubali kuchafuliwa kwa mambo ambayo hayahitajiki michezoni.

"Wachezaji hawako kambini, wanakwenda uwanjani usiku kufanya nini, hata Lipuli wanavyodai wachezaji wao wameumizwa, subirini muone kama hawatapangwa kwenye mechi ya leo," amesema.

Alisema hawako tayari kuona ligi inachafuliwa na kwamba wanazo taarifa za wote waliohusika na tukio hilo akiahidi kuwa baada ya mechi watashusha rungu kwa kila aliyehusika.

Chanzo: mwananchi.co.tz