Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Utamu wa Yanga, Simba huu hapa

24708 Pic+yanga TanzaniaWeb

Wed, 31 Oct 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Wakati Yanga leo inateremka uwanjani kuikabili Lipuli, safu yake ya ushambuliaji imeshindwa kuonyesha makali na jukumu hilo limebebwa na wachezaji wa idara nyingine kulinganisha na watani wao wa jadi Simba.

Yanga inaikabili Lipuli katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, uliopangwa kuchezwa saa moja usiku kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Huku ikiwania matokeo ya ushindi kusogea hadi nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi, Yanga inaingia uwanjani  ikitegemea zaidi nyota wa safu ya kiungo na ulinzi kuwapa mabao kutokana na kuyumba kwa washambuliaji wake asilia.

Washambuliaji asilia wa Yanga, wamefunga idadi ndogo ya mabao katika kikosi hicho msimu huu wakiachwa mbali na wenzao wa Simba, ingawa afueni kwa timu hiyo imekuwa ikiletwa na viungo wake hasa wa ushambuliaji na mabeki ambao wamekuwa wakiibeba kuipa matokeo.

Katika jumla ya mabao 15 ambayo Yanga imefunga katika mechi zao nane walizocheza kabla ya jana, mabao matano tu ndiyo yamefungwa na washambuliaji asilia na yaliyobaki yakifungwa na viungo, mabeki.

Mabao matano yaliyofungwa na washambuliaji asilia wa Yanga, hayafiki hata nusu ya mabao yote ambayo yamefungwa na mabingwa hao wa kihistoria wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Wakati hali ikiwa hivyo kwa Yanga, mambo yanaonekana kuwanyookea washambuliaji asilia wa Simba ambao katika jumla ya mabao 21 wamefunga 16.

Mabao matano ya Yanga katika mechi nane ilizocheza hadi sasa, yamewekwa wavuni washambuliaji wawili Heritier Makambo aliyefunga matatu na Amissi Tambwe (mawili).

Makambo amefunga mabao matatu katika mechi dhidi ya Mtibwa Sugar, Coastal Union na Alliance FC wakati Tambwe akifunga mawili dhidi ya Singida.

Wakati Makambo na Tambwe wakijitutumua kuifungia Yanga mabao, washambuliaji wengine asilia, Yusuph Mhilu, Mateo Anthony na Yohana Nkomola hawana mchango hadi sasa kwa kuwa hawajafunga hata bao moja.

Hata hivyo, viungo na mabeki wake wameonekana kulibeba vyema jukumu ambalo lilipaswa kufanywa na washambuliaji wao kwa kuifungia timu yao mabao muhimu yaliyoiweka katika nafasi nzuri kwenye msimamo wa ligi.

Viungo na mabeki wa Yanga kwa pamoja wamefunga jumla ya mabao 10 ambayo ni sawa na asilimia 66.67 ya mabao yote 15 yaliyofungwa na timu hiyo katika mechi nane ilizocheza dhidi ya Mtibwa Sugar, Stand United, Coastal Union, Singida United, Alliance, Simba, KMC na Mbao FC.

Viungo walioibeba Yanga kwa kuifungia mabao ni Ibrahim Ajibu aliyepachika matatu, Mrisho Ngassa (mawili), Rafael Daud, Deus Kaseke na Feisal Salum kila mmoja amefunga bao moja sawa na mabeki Andrew Vincent 'Dante' na Kelvin Yondani.

Kwa upande wa Simba wameonekana kuwa moto wa kuotea mbali kutokana na kufunga mabao 16 kati ya 21 waliyokuwa nayo kabla ya mchezo wa juzi ikiwa ni sawa na 76.19% ya mabao yote yaliyofungwa na timu hiyo.

Washambualiaji asilia wa Simba waliofunga mabao,Emmanuel Okwi (saba), Meddie Kagere (matano) John Bocco (mawili) sawa na Adam Salamba.

Mabao matano yaliyobaki yamefungwa na viungo na mabeki ambao ni Cletus Chama (mawili), Shiza Kichuya na Asante Kwasi ambao wamefunga bao moja kila mmoja na lililobakia likiwa la kujifunga.

Washambuliaji, Marcel Kaheza na Mohammed Rashid wenyewe hadi sasa wameshindwa kupachika bao, badaa ya kusajiliwa na Simba msimu huu.

Hata hivyo, washambuliaji wa timu hizo ambao hawajafunga hadi sasa, hawapati nafasi ya kucheza mara kwa mara kwenye kikosi cha kwanza jambo linaloashiria viwango vyao vimeshindwa kuwashawishi makocha wa timu zao kuwapa nafasi.

Kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera alisema anaridhika na matokeo ya timu yake pasipo kujali ni mchezaji gani amefunga bao.

"Sisi malengo yetu ni kupata ushindi na suala la timu kupata matokeo huwa sio jukumu la mtu mmoja. Unapoona hadi mabeki wanafunga inatoa maana halisi ya timu haipaswi kumtegemea mchezaji mmoja," alisema Zahera.

Kocha wa Simba, Patrick Aussems alisema anakoshwa na jinsi washambuliaji wanavyotumia vyema nafasi wanazotengeneza kufunga mabao.

"Kwa sasa naridhika kwa sababu mwanzoni tulikuwa tunacheza vizuri lakini tukawa hatufungi mabao, washambuliaji wangu wakawa wanalaumiwa, lakini kadri muda unavyozidi kwenda, wameanza kufanya vizuri na wanafunga mabao hivyo kama kocha lazima niridhike," alisema Aussems.

Chanzo: mwananchi.co.tz