Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Usione Mwakinyo anang’ara amepitia msoto mkali

49143 Mwakiny+pic

Thu, 28 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Hassan Mwakinyo, ambaye ni nembo ya Tanzania kwa sasa katika masumbwi hakuibuka tu, alipambana hadi kufika hapo alipo.

Septemba 8, 2018 itabaki kwenye kumbukumbu ya bondia huyo kwani ndipo umaarufu wake ulipoibuka baada ya kumchapa aliyekuwa bondia namba nane wa dunia, Sam Egginton wa Uingereza.

Pambano hilo liliacha mshtuko si tu Uingereza, bali kwenye familia ya ndondi duniani kutokana na rekodi ya Egginton ambaye alikalishwa chini kwa Technical Knock Out (TKO) raundi ya pili akiwa nyumbani.

Mafanikio ya Mwakinyo yalianzia hapo, alipanda kwenye ubora wa dunia na kuwa bondia namba 16 duniani na namba moja Afrika kwenye uzani wa super welter.

Baada ya hapo, alipata mwaliko wa kutembelea bungeni, pia kualikwa nyumbani kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

Jumamosi iliyopita, Mwakinyo kwa mara nyingine aliteka vyombo vya habari alipomchapa Sergio Gonzalez kwa TKO raundi ya tano nchini Kenya. Ushindi huo ulimfanya Rais John Magufuli kumwalika Ikulu, Dar es Salaam kwa ajili ya chakula cha mchana na timu ya Taifa iliyofuzu kucheza Fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon).

Katika hafla hiyo iliyofanyika Jumatatu iliyopita, Rais aliwazawadia viwanja wanamichezo hao vilivyoko Dodoma kama pongezi kwa kuiwakilisha nchi vyema.

Tofauti na Mwakinyo unayemfahamu, Mwananchi linakuletea mambo mengine usiyoyafahamu kuhusu bondia huyo anayetamba kwa sasa.

Hajawahi kupigwa kihalali

Rekodi ya bondia huyo, inaonyesha amecheza mapambano 17, amepigwa mara mbili, moja likichezwa nchini dhidi ya Shaban Kaoneka na Lendrush Akopian lililofanyika Urusi.

“Ni mapambano ambayo hadi leo matokeo yake yananiumiza, sikupigwa kihalali ingawa rekodi haiwezi kufutika,” anasema Mwakinyo ambaye anadhaminiwa na SportPesa Tanzania.

Anasema pambano lake na Kaoneka, kamba ya ulingo ilikatika bila kufahamu, wakati pambano likiendelea bahati mbaya alidondoka hapo hapo akaambiwa amepigwa kwa KO.

Pambano la Urusi la mwaka 2017, lilikuwa la ubingwa wa WBC wa vijana ambapo walimaliza raundi zote 10.

Mwamuzi, Daniel Van de Wiele alimtangaza Akopian kuwa bingwa wa majaji watatu.

Jaji Alexander Kalinkin na Andrey Kurnyavka walitoa ushindi kwa Mrusi wa pointi 100-89 na Olena Pobyvailo alitoa pointi 99-90.

“Lilikuwa pambano nililocheza ugenini, kwa vyovyote vile ilikuwa lazima matokeo yawe vile,” anasema Mwakinyo.

Amewahi kutoa boko kwenye soka

Mashabiki wa KMC wana historia ya alichokifanya mchezaji wao, Ally Ally timu yao ilipocheza na Yanga hivi karibuni ambapo alijifunga bao safi lililowapa Yanga pointi tatu.

Kwa Mwakinyo pia amewahi kukutana na ‘boko’ hilo na kulazimika kukimbia moja kwa moja kwenye soka.

“Ilikuwa kwenye mechi ya soka mtaani kwetu huko Tanga, hatukuwa tumefungana, lakini kabla ya mpira kumalizika, nilijifunga na pale pale nikakimbia kwenye mpira mpaka leo sijarudi tena,” anasema.

Mwakinyo ukiachana na ngumi, yeye ni shabiki kindakindaki wa mabingwa watetezi wa Ligi Kuu, Simba.

Alipitia msoto balaa

Kabla ya kumchapa Eggington, Mwakinyo alipitia msoto (hali ngumu) akitafuta kutoka.

“Ilifikia mahali, nimetoka mazoezini, njaa inauma, nyumbani hakuna kitu, nilichokifanya niliangua dafu nikanywa na chai siku ikapita, wakati huo nilikuwa najiandaa kucheza na Egginton,” anasema.

Marehemu baba yake alikuwa bondia

Mwakinyo ni ‘mto wa nyoka’ kwenye ndondi kwani amefichua kuwa baba yake, Hamza Mwakinyo pia alikuwa bondia.

“Nilikuwa napenda kumfuatilia mzee wakati akifanya mazoezi, nikajikuta napenda, hivyo nikashawishika kujifunza ngumi,” anasema.

Atembelea MCL

Juzi, Mwakinyo alitembelea makao makuu ya Mwanachi Communications Limited (MCL), Tabata Relini jijini Dar es Salaam.

Katika ziara hiyo, alitembelea vitengo mbalimbali na kukaribishwa kwenye kikao cha wahariri.

Katika mahojiano maalumu, Mwakinyo alibainisha kuwa bado ana safari ndefu kwenye ngumi na ndoto zake ni kufika anga za mabondia kama Floyd Maywether, Manny Pacquiao na Jarret Hurd.

Mkurugenzi Mtendaji wa MCL, Francis Nanai alimpongeza na kusisitiza kampuni hiyo itaendelea kushirikiana naye bega kwa gega.

Nanai alimzawadia Mwakinyo fedha taslimu Dola 100 za Marekani (takriban Sh225,000) pamoja na magazeti yanayochapishwa na kampuni hiyo ambayo ni Mwananchi, Mwanaspoti na The Citizen.

Mwakinyo anawashauri vijana kupambana katika kutafuta na kutokatishwa tamaa na hali ngumu kwani njaa ni suala la muda huku akisisitiza kuwa mafanikio yanaanza na mtu mwenyewe kuwa tayari na kumtanguliza Mungu katika kila jambo.



Chanzo: mwananchi.co.tz