Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Usajili wa Nchimbi waibua mzozo

89143 Nchimb+pic Usajili wa Nchimbi waibua mzozo

Thu, 19 Dec 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Klabu za Azam na Polisi Tanzania zimeingia vitani kumgombea Ditram Nchimbi ikiwa ni muda mfupi baada ya mchezaji huyo kudaiwa kusajiliwa na Yanga.

Nchimbi ambaye yuko Uganda na timu ya Taifa ya Tanzania Bara ‘Kilimanjaro Stars’, jana alitarajiwa kutia saini mkataba wa kujiunga na Yanga.

Akizungumza jana, Kaimu Katibu Mkuu wa Polisi Tanzania, Frank Lukwaro alisema wanamtambua Nchimbi ni mchezaji wao mpaka msimu wa 2019/2020 utakapomalizika.

Lukwaro alisema mshambuliaji huyo alijiunga na klabu hiyo kwa mkopo akitokea Azam, hivyo ina haki ya kupata sehemu ya fedha endapo atauzwa.

“Kuna gharama tuliingia wakati tunamuomba mchezaji kama Yanga imemsajili hatuwezi kumwachia bila kuwekewa mezani milioni 15 kama fidia ambazo tulimuhudumia muda aliokuwa hapa.

“Kama unatumika ujanja wa kumsajili mchezaji bila maridhiano kwa timu zote wasiwe na matumaini ya kumpata kwasababu hata TFF inapomuhitaji haitumi barua Azam inatuma kwa Polisi Tanzania,” alisema Lukwaro.

Fedha za kumuuza Nchimbi zitatumika kununua mchezaji wa kuziba nafasi yake kabla ya dirisha la usajili kufungwa Januari 15, mwakani.

Wakati Lukwaro akitoa kauli hiyo, Mtendaji Mkuu wa Azam, Abdulkarim Amin ‘Popat’ alisema Nchimbi ni mchezaji wao halali na Polisi Tanzania haina mamlaka ya kumuuza.

“Tulimpeleka Ditram Nchimbi Polisi Tanzania kwa mkopo, hakuna sehemu katika barua yetu inayosema atacheza kwao moja kwa moja.

Baada ya Yanga kuleta ofa yao tuliwauliza Polisi Tanzania kama wanamtaka wakasema hawana uwezo wa kumnunua kwahiyo tuliendelea na mchakato wa kuwauzia Yanga kwasababu wamekuja na ofa, iko wazi Nchimbi ni mchezaji wetu halali alikwenda Polisi Tanzania kwa mkopo,”alisisitiza Popat.

Mchezaji huyo alitia saini mkataba wa miaka miwili Azam na amebakiza miezi saba kabla ya kutolewa kwa mkopo wa mwaka mmoja kwenda Polisi Tanzania.

Nchimbi amefunga mabao matatu katika Ligi Kuu Tanzania Bara akiifunga Yanga. Pia amewahi kucheza Majimaji ya Songea, Mbeya City, Njombe Mji na Mwadui ya Shinyanga.

Katika hatua nyingine nahodha wa UD Songo ya Msumbuji Luis Miquissone, ameziingiza vitani Yanga na Simba ambazo kila moja inawania saini yake.

“Sipendi kuzungumza na vyombo vya habari Simba nimezungumza nao lakini maongezi hayakuwa marefu kama ambavyo ilikuwa Yanga ambao wameonyesha uhakika wa kunitaka.

“Uhakika wa Yanga unatokana na wao kuzungumza mpaka na wakala wangu ambaye wamekubaliana kutuma tiketi ya ndege ili nije Tanzania kutia saini mkataba. Hata Simba mazungumzo yetu hayakuwa mabaya lolote linaweza kutokea,” alisema Miquissone.

Wakati huo huo, mshambuliaji wa Yanga Issa Bigirimana ameandika barua ya kuvunja mkataba wake na klabu hiyo. Bigirimana aliyejiunga na Yanga akitokea APR ya Rwanda, amefikia uamuzi huo baada ya kukosa namba kikosi cha kwanza.

Chanzo: mwananchi.co.tz