Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Usajili Yanga unavyomuweka kikaangoni Zahera

79006 Zahera+pic

Tue, 8 Oct 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Hapana shaka presha kwa kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera ipo juu kwa sasa baada ya timu hiyo kuondolewa na Zesco United kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu.

Pamoja na Yanga kuangukia hatua ya mchujo ya Kombe la Shirikisho, bado mambo yanaonekana kutonyooka kwa Zahera kwa sababu pia timu hiyo ilianza vibaya Ligi Kuu kwa kuchapwa bao 1-0 na Ruvu Shooting.

Mbali na matokeo, Yanga inaonekana kushindwa kucheza kitimu na imekuwa ikicheza kwa kutegemea zaidi uwezo na juhudi binafsi ya mchezaji mmojammoja badala ya juhudi za pamoja za kikosi kizima.

Kama hali ikiendelea hivyo, kuna uwezekano mkubwa Zahera akapewa mkono wa kwaheri na Yanga ikafungua milango kwa kocha mwingine.

Ni vigumu kwa Yanga kumvumilia Zahera msimu huu kama ambavyo walifanya msimu uliopita na sababu kubwa inayochangia hilo ni usajili ambao klabu hiyo imefanya msimu huu.

Ni usajili ambao umetumia kiasi kikubwa cha fedha huku pia ukitokana na mapendekezo ya kocha huyo ambaye aliahidi kwamba kama yatafanyiwa kazi, Yanga itakuwa na timu tishio.

Pia Soma

Advertisement
Hata hivyo mambo yanaonekana yanaanza kwenda kinyume na kile kilichotegemewa jambo ambalo linaweka rehani maisha ya Zahera ndani ya timu hiyo.

Spoti Mikiki inakuletea tathmini ya namna gani usajili ambao Zahera alipendekeza unavyoweza kuwa chanzo cha kumuondoa ndani ya Yanga.

Uwiano haukuzingatiwa

Kwa timu yoyote ile pindi inapofanya usajili ni lazima izingatie uwiano mzuri wa idadi ya wachezaji katika kila nafasi ili hata pale inapotokea mchezaji mmoja anakosekana kwasababu tofauti, awepo mwingine wa kuziba pengo lake kwani vinginevyo timu inaweza kujikuta iko matatani.

Hata hivyo ni tofauti na usajili wa Yanga ambao umetokana na mapendekezo ya Zahera msimu huu kwani kuna nafasi ambazo zimejaza idadi kubwa ya wachezaji huku nyingine zikiwa na upungufu jambo linalofanya kikosi chake kisiwe na uwiano mzuri.

Nafasi ambayo ina idadi kubwa ya wachezaji ni ile ya beki wa kati ambapo kuna wachezaji saba ambao kiasili wanacheza eneo hilo ambao ni Ally Ally, Selemani Mustafa, Ally Sonso, Cleofas Sospeter, Kelvin Yondani, Lamine Moro na Andrew Vincent ‘Dante’

Katika hali ya kushangaza, upande wa mabeki wa pembeni hakuna namba ya kutosha ambapo kuna mabeki wawili tu wa kulia ambao ni Juma Abdul na Paul Godfrey ‘Boxer’ huku kushoto pia kukiwa na beki mmoja tu ambaye ni Issa Muharami ‘Marcelo’ ingawa pia amekuwa akimtumia Jafari Mohammed ‘Rasta’ ambaye kiasili sio beki wa pembeni.

Matokeo yake, kutokana na majeruhi na kutokuwa fiti kwa baadhi ya wachezaji wa nafasi ya mabeki wa pembeni, Yanga imekuwa ikilazimika kuwatumia mabeki wa kati kucheza kwenye nafasi hizo jambo limekuwa likiifanya iwe na udhaifu kwenye nafasi hizo kulinganisha na zile ambazo hupanga wachezaji sahihi wanaozicheza.

Nafasi nyingine ambayo imejaza idadi kubwa ya wachezaji ni ile ya kiungo ambayo ina Deus Kaseke, Papy Tshishimbi, Jafari Mohammed, Feisal Salum, Mohamed Issah, Rafael Daud, Abdulaziz Makame na Said Juma ‘Makapu’

Hata hivyo Yanga haijatazama nafasi ya winga ambapo imesajili mawinga watatu kwa ajili ya kuwatumia upande wa kulia na kushoto ambao ni Mrisho Ngassa, Patrick Sibomana na Issa Bigirimana.

Pia Yanga imesajili mshambuliaji mmoja tu ambaye kiasili ni namba tisa naye ni David Molinga huku ikiwa na nyota watatu ambao hucheza namba kumi nao ni Sadney Urikhobi, Juma Balinya na Maybin Kalengo.

Changamoto inayoikuta Yanga ni kwamba watatu hao pindi wanapokuwa uwanjani huwa hawatulii kwenye boksi la timu pinzani jambo ambalo limekuwa likichangia timu hiyo kuyumba katika mechi zake.

Upangaji wa kikosi

Kikosi kilichopo sasa cha Yanga kimetokana na mapendekezo ya Zahera mwenyewe lakini katika hali ya kushangaza amekuwa akiyumba katika kukipanga kuanzia kile cha kwanza na pia hata katika ufanyaji wa mabadiliko timu inapokuwa inacheza.

Kwanza amekuwa akiwaweka benchi baadhi ya wachezaji ambao wanamudu kucheza kwenye nafasi fulani au wale wanaoonekana wako vizuri pasipo sababu yoyote huku akilazimisha kuwatumia wachezaji wengine katika nafasi wasizostahili.

Mfano katika mchezo wa marudiano dhidi ya Zesco United wiki iliyopita, Zahera alimpanga beki wa kati, Ally Ally upande wa kulia huku kwenye benchi akiwa na Juma Abdul ambaye ndiye kiasili hucheza katika upande huo.

Mfano mwingine ni mshambuliaji Juma Balinya ambaye angalau amekuwa akionyesha uwezo wa kufumania nyavu na kuwapa nafasi ya kucheza kwa muda mrefu David Molinga, Sadney Urikhobi na Maybin Kalengo

Ufanisi duni wa nyota wake

Hakuna jambo gumu kwa kocha kama pale wachezaji ambao umewapendekeza katika ripoti yako ya usajili kushindwa kufanya kile ambacho kinatarajiwa na badala yake wakaonyesha kiwango duni.

Hali kama hiyo ndio inamkuta Zahera kwa sasa kutokana na baadhi ya wachezaji wake hasa wale wapya kuonesha mapema dalili za kuchemka jambo ambalo linaweza kuigharimu timu hiyo ikiwa viwango vyao havitaimarika.

Mfano wa wachezaji hao ni Issa Bigirimana aliyenaswa kutoka APR ya Rwanda, Maybin Kalengo, Issa Muharami ‘Marcelo’ na Ally Ally.

Inashangaza kuona licha ya umri wake mkubwa, Mrisho Ngassa aliyewahi kuwika Taifa Stars anakuwa mchezaji tegemeo kikosini kulinganisha na nyota wengine ambao wana umri mdogo.

Chanzo: mwananchi.co.tz