Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Unapoifikiria Simba vs TP Mazembe, unapatwa na hofu

48504 Edo+pic

Mon, 25 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

ACHANA na pambano la jana Jumapili la Taifa Stars pale Uwanja wa Taifa, majuzi karatasi ilionyesha Simba itacheza dhidi ya TP Mazembe katika pambano la robo fainali. Mechi ya kwanza itachezwa Dar es Salaam. Mechi ya pili itaenda kuchezwa katika mji wenye vumbi wa Lubumbashi pale DR Congo.

Unapatwa hofu unapofikiria mechi hii. Simba ilishinda mechi zote tatu za nyumbani hatua ya makundi. Ilianza dhidi ya JS Saoura. Ikashinda dhidi ya Al Ahly na kisha ikaitafuna mchana kweupe AS Vita. Hizi timu mbili za mwisho zina uzoefu zaidi na soka la Afrika.

Kwanini mechi ya Simba na Mazembe inaleta hofu? Ndio, inaleta hofu zaidi kuliko mechi za makundi. Hatua hii ni ya mtoano. Hatuhesabu pointi. Simba ilivuka katika makundi kwa sababu ya pointi lakini ina rekodi mbovu ya kufungwa mabao mengi ugenini.

Kama ingekuwa mtoano Simba ingekuwa imetolewa na Al Ahly. Ingekuwa imetolewa na Vita. Simba ilichezea mabao 5-0 Cairo halafu mechi ya marudianoikashinda 1-0 Dar es Salaam. Ilichezea mabao 5-0 pale Kinshasa halafu ikashinda 2-1 Uwanja wa Taifa.

Mechi pekee ambayo Simba ingeweza kumtoa mpinzani wake ni dhidi ya Saoura. Ilishinda mabao 3-0 nyumbani, kisha ikafungwa 2-0 ugenini. Ni hiki tu ndicho ambacho kinaweza kuipitisha Simba dhidi ya Mazembe.

Simba ina matatizo mawili katika matokeo yake ambayo yanatia hofu unapofikiria mechi yao dhidi ya Mazembe. Haifungi mabao ya kutosha nyumbani na inaruhusu mabao mengi ugenini. Tabia hii ni mbaya unapofikia hatua ya mtoano.

Unaweza kuwa mjanja mjanja katika suala la pointi lakini linapofika suala la ngumi za nyumbani na ugenini ujanja huu unafika mwisho. Hakuna suala la pointi tena.

Ni suala la nani ana matokeo mazuri baina ya mechi mbili.

Na kitu kingine tofauti zaidi ni ukweli Simba ilipata fursa nzuri ya kutafakari mechi zake dhidi ya Al Ahly na Vita kwa sababu zilianzia ugenini. Licha ya kufungwa mabao mengi lakini iliweza kurudi nyumbani na kutafakari.

Tatizo mechi hii dhidi ya Mazembe inaanzia Dar es Salaam na inaishia Lubumbashi. Hiki ni kipimo kikubwa cha akili kwa Simba. Ni tofauti na zile mechi ambazo zilianzia Cairo na Kinshasa kisha zikamalizikia Dar es Salaam. Hii ni mechi tofauti katika ukomavu wa akili wa Kocha Patrick Aussems na wachezaji wake.

Simba inabidi iondoke na ushindi mkubwa Dar es Salaam, pengine bila ya kuruhusu bao la ugenini kwa Mazembe, kisha ikapambane kusaka sare ugenini.

Hiki ndio kitu ambacho Kocha Aussemes ameshindwa kutuonyesha, hasa katika mechi kubwa za ugenini.

Aussems anatia mashaka kama anaweza kuizuia Mazembe isipate mabao mengi pale Lubumbashi. Simba inapocheza ugenini huwa inacheza kama ipo Dar es Salaam. Haina nidhamu ya ulinzi. Haitengenezi mfumo mzuri wa kujihami na badala yake timu inafunguka tu.

Inakwenda kucheza dhidi ya Mazembe ambayo inajulikana kwa kuutumia vema uwanja wa nyumbani. Huwa haina masikhara ikiwa kwake. Uwanja wake wa nyumbani pengine ndio uwanja wa ugenini unaohofiwa zaidi na Waarabu wa Afrika Kaskazini pengine kuliko uwanja wowote wa soka Afrika.

Kitu kingine kigumu zaidi kwa Simba katika pambano hili ni ukweli kwamba Mazembe itatua Dar es Salaam ikijua Al Ahly alifia pale Temeke. Itakuwa inajua kwamba wapinzani wao wa jadi wa Congo, AS Vita walifia pale Temeke. Watajipanga zaidi pengine kuliko wakati mwingine wowote ule.

Watajipanga huku wakiingiwa na hofu kuhusu uvumi uliopo kwamba kuna mambo mengine zaidi ya nje ya uwanja ndiyo ambayo yalisababisha wakubwa wenzao wakafa pale Temeke.

Itakuwa mechi ngumu kwa Simba ndani na nje ya uwanja.

Kila la kheri kwa Simba. Chochote kizuri itakachofanya sasa kitakuwa kizuri zaidi pengine kuliko ilichofanya dhidi ya kina Al Ahly katika hatua ya makundi. Sio tu kwa sababu itafika nusu fainali, hapana, lakini pia itaonyesha ukomavu wa kuanzia mechi nyumbani halafu ikamalizia kazi ugenini.

Na mara zote kazi ngumu inakuwa ugenini. Hata hivyo, iliwahi kufanya hivyo miaka 16 iliyopita pale Cairo. Unakumbuka ilichokifanya mbele ya Zamalek?



Chanzo: mwananchi.co.tz