Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Umbali janga jipya Ligi Kuu

44421 Pic+ligi Umbali janga jipya Ligi Kuu

Sun, 3 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Wakati vita ya kuwania taji la Ligi Kuu Tanzania Bara ikipamba moto, Simba itakuwa na kazi kubwa kutetea ubingwa wake kutokana na kuwa na mechi nyingi za mikoani.

Yanga yenye pointi 61 ikishinda mechi 13 ziliobaki itafikisha pointi 100 na Simba ikishinda mechi 19 itafikisha pointi 105.

Simba itasafiri umbali wa kilomita 7,403 kwa basi au 5,316 kwa ndege kusaka pointi 27 kwenye viwanja vinane vya mikoani.

Yanga ina mechi tano mikoani ingawa haipishani na Simba katika umbali wa safari kwani itasafiri kilomita 7116 kwa basi au 5,362 kwa ndege.

Azam itasafiri umbali wa kilomita 5,999 kwa basi au 4189 kwa ndege kusaka ushindi katika mechi zake nne za mikoani.

Simba

Simba ina mechi tisa za mikoani ingawa rekodi dhidi ya wapinzani wake zinaweza kuwa mfupa mgumu kutokana na ubora wa timu hizo.

Timu hiyo itaanza safari ya kwenda Shinyanga kuikabili Stand United Jumapili Machi 3 na itasafiri kilomita 800 kwa basi ikitokea Iringa walikocheza na Lipuli. Kama itatumia ndege itasafiri kilomita 521.

Simba itacheza mechi sita Dar es Salaam kabla ya kusafiri kilomita 341 kwa basi au 196 kwa ndege kuifuata Coastal Union Tanga Aprili 15 na baadaye itasafiri kilomita 1,292 kwenda Bukoba kuvaana na Kagera Sugar Aprili 19.

Simba itasafiri kilomita nyingine 421 kwa basi au 179 kwa ndege kwenda Mwanza kuifuata Alliance Aprili 22 na itakwenda Musoma kuikabili Biashara United kwa umbali wa kilomita 222.

Timu hiyo itatumia kilomita 1,059 kwa basi au 824 kwa ndege kwenda Mbeya kuzifuata Prisons na Mbeya City Aprili 30 na Mei 3 na baadaye itasafiri kilomita 830 kwa basi au 681 kwa ndege kurejea Dar es Salaam.

Simba itacheza mechi nne Dar es Salaam kabla ya kusafiri kilomita 702 kwa basi au 548 kwa ndege kwenda Singida kuivaa Singida United Mei 20. Pia itakwenda Morogoro kwa kilomita 543 kwa basi au 392 kwa ndege kuifuata Mtibwa Sugar Mei 26 kabla ya kusafiri kilomita 194 kurejea Dar es Salaam.

Katika mechi nne zilizopita dhidi ya Stand United Uwanja wa Kambarage, Shinyanga tangu 2015 Simba imeshinda michezo mitatu na wenyeji mara moja Februari 21, 2015 Stand ilipoifunga Simba bao 1-0.

Mechi mbili za dhidi ya Coastal Union Uwanja wa Mkwakani Simba ilishinda mara moja na kutoka sare mchezo mmoja.

Katika mechi nne dhidi ya Kagera Sugar tangu mwaka 2015, Simba imeshinda mara tatu na kupoteza mchezo mmoja Aprili 2, 2017 ilipochapwa mabao 2-1.

Pia Simba ina rekodi nzuri dhidi ya Prisons kwenye Uwanja wa Sokoine Mbeya kwani katika michezo mitatu timu hiyo imeshinda mara mbili na Prisons mara moja.

Katika mechi nne dhidi ya Mbeya City tangu mwaka 2015 Simba imeshinda michezo mitatu.

Singida United imekutana na Simba mara moja Uwanja wa Namfua Mei 12, mwaka jana na kufungwa bao 1-0.

Mtibwa Sugar tangu 2014 imekutana na Simba Morogoro katika mechi nne imefungwa mara mbili na kutoka sare mbili.

Mara ya mwisho Mtibwa Sugar kuifunga Simba ni Novemba 4,2012 iliposhinda mabao 2-0.

Kocha wa Simba Patrick Aussems alisema anafurahi kuona wachezaji wake wakibadilika kila mechi na kucheza kwa kiwango bora, hivyo anaamini wataendeleza moto huo hata katika mechi za mikoani.

Yanga

Yanga itasafiri kilomita 1146 kwa basi au 853 kwa ndege kuifuta Alliance FC Jumamosi na itarejea Dar es Salaam ikitumia kilomita 561 kwenda Mtwara kuivaa Ndanda Aprili 3 na itasafiri kilometa kama hizo kurejea Dar es Salaam.

Yanga ilivunja mwiko Februari 28 mwaka jana iliposhinda mabao 2-1 Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara.

Timu hiyo itasafiri kilomita 194 kwenda Morogoro kucheza na Mtibwa Sugar Aprili 17 na Mei 9 itasafiri kilomita 1155 kwenda Musoma kucheza na Biashara United.

Kocha wa Yanga Mwinyi Zahera amekiri vita ya ubingwa ni kubwa hasa kwa timu tatu zilizo juu katika msimamo wa Ligi Kuu.

Azam

Azam itasafiri kilomita 5999 kwa basi au 4189 kwa ndege kusaka ushindi katika mechi nne za mikoani. Itasafiri kilomita 1146 kwa basi au 853 kwa ndege kwenda Mwanza kuikabili Mbao Aprili 4.

Baadaye itacheza na Mbeya City Aprili 14 na itasafiri kilomita 904 kwa basi au 712 kwa ndege kabla ya kwenda Mtwara kucheza na Ndanda Aprili 18 ambapo itasafiri kilomita 1390 kwa basi au 754 kwa ndege.

Azam itarejea Dar es Salaam kwa kilomita 561 kwa basi au 396 kwa ndege na itacheza mechi tano. Mei 5 itasafiri kilomita 999 kwa basi au 737 kwa ndege kuifuata Stand United na itasafiri kilomita kama hizo kurejea Dar es Salaam.



Chanzo: mwananchi.co.tz