Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Umakini, pumzi vimeigharimu Taifa Stars Misri

64826 Stras+pic

Sat, 29 Jun 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Udhaifu wa safu ya ulinzi na kiungo kwa timu ya taifa ‘Taifa Stars’ vimechangia kuiangusha timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ kwenye mchezo muhimu wa Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) dhidi ya Kenya juzi, ambao Tanzania ilipokea kichapo cha mabao 3-2 na kuaga rasmi mashindano hayo mwaka huu.

Licha ya kuanza mchezo huo kwa kasi na kutawala sehemu kubwa ya kipindi cha kwanza ambacho ilifunga mabao mawili, safu ya ulinzi ya Stars ilifanya makosa ya kizembe na kupoteza umakini na kuizawadia Kenya mabao matatu yaliyozima rasmi ndoto ya Tanzania kupata ushindi wa kwanza kwenye mashindano hayo ambayo imeshiriki kwa mara ya pili baada ya kufanya hivyo mwaka 1980.

Safu hiyo ya ulinzi ya Stars ilishindwa kukabili mipira ya juu ambayo Kenya waliitumia mara kwa mara hasa waliporejea kipindi cha pili wakijivunia faida ya wachezaji wengi warefu walionao katika kujenga na kufanya mashambulizi yake. Tanzania iliruhusu mabao mawili yalitokana na mashambulizi ya juu.

Bao la kwanza la kusawazisha la Kenya, lilitokana na uzembe wa mabeki kuchelewa kuokoa mpira wa friikiki uliookolewa vibaya na kipa Aishi Manula ambao ulidondokea kwa Michael Olunga aliyeujaza kimiani kwa staili ya ‘tik-tak’.

Kana kwamba haitoshi, bao la pili la kusawazisha lililofungwa na Johanna Omolo lilitokana na uzembe na kukosa umakini kwa mabeki wa Stars ambao walimruhusu kiungo huyo kupiga kichwa kuunganisha krosi ya Ayub Masika ambaye alipokea pasi fupi ya kona kutoka kwa Eric Ouma.

Iwapo ukuta wa Stars ungetimiza jukumu lake ipasavyo, ni wazi kwamba Omolo asingefunga bao hilo kwani hakupaswa kuwa huru kuunganisha mpira huo, lakini hata Masika aliyepiga krosi naye hakuwa amedhibitiwa ipasavyo.

Pia Soma

Mbali na mabao hayo mawili ambayo yalikuwa ya kusawazisha, hata bao la tatu lilitokana na uzembe wa walinzi na viungo wa Stars kumsindikiza Olunga na kumpa nafasi ya kupiga shuti lililomshinda Manula ambaye jana alionekana kutokuwa kwenye fomu yake.

Lakini makosa yote hayo ya safu ya ulinzi ya Stars yalichagizwa na udhaifu wa safu ya kiungo ambayo iliwaruhusu Kenya kupora pasi na kujenga mashambulizi jambo ambalo lilifanya lango la Stars kuwa matatani mara kwa mara hasa katika dakika 45 za kipindi cha pili.

Hali ilikuwa mbaya zaidi kwa kiungo cha Stars mara baada ya kufanyika mabadiliko ya kumtoa Mudathir Yahya na kumuingiza Himid Mao na kisha yale ya kutolewa Erasto Nyoni aliyeumia na kuingia Frank Domayo, kwani timu nzima ilirudi nyuma na kuruhusu Kenya kusogea kwa kasi kwenye eneo la ulinzi na kutengeneza idadi kubwa ya nafasi za mabao.

Nyoni aliituliza vyema timu na kuichezesha huku Mudathir akifanya kazi kubwa ya kutibua mipango ya Kenya pamoja na kuunganisha safu ya kiungo na ushambuliaji, lakini kwa bahati mbaya walioingia walishindwa kutimiza vyema jukumu la waliotangulia, hali iliyoiweka Stars matatani.

Akizungumzia kipigo hicho, kocha wa Stars, Emmanuel Amunike alikiri kuwa uzembe na makosa ya wachezaji kutotimiza kile walichoelekezwa ndio kumeigharimu timu hiyo.

“Kama hujui kutawala mchezo ni lazima uadhibiwe. Kuna mambo mengi ya kichizi yaliyofanyika na tulifanya makosa mengi. Hatukujipanga vizuri na ukabaji wetu haukuwa sahihi.

“Hili ni jambo ambalo tumekuwa tukilifanyia mazoezi siku hadi siku lakini wachezaji ni wachezaji. Kama kocha, unasimama nje ya uwanja na unakuwa hauna msaada. Hakuna uelewa kwenye timu. Tumekosa uzoefu. Ni jambo linalopaswa kulifungua macho soka la Tanzania. Ukweli ni kwamba hatuko kwenye nafasi ya kushindana,” alisema Amunike.

Nahodha Mbwana Samatta alisema makosa ya jumla ambayo yalifanywa na timu yamewaangusha na kuwapa mwanya wapinzani wao kupata ushindi.

Chanzo: mwananchi.co.tz