Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ulega ataka lega ataka michezo iweke wazi hesabu zao

1691b1a886e3120f50c4803db95b53ea Ulega ataka lega ataka michezo iweke wazi hesabu zao

Mon, 25 Jan 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

UCHUMI imara ni moja ya mambo yanayoweza kuchagiza maendeleo katika sekta ya michezo nchini na kuibua vijana wengi wenye vipaji watakao kuwa na uwezo wa kushindana na kuitangaza nchi kimataifa.

Kwa muda mrefu sasa timu zetu nyingi zimekuwa na changamoto ya kuwapata vijana wa aina hiyo kutokana na mfumo wetu kutokuwa mzuri wa kufanya uchunguzi wa kuwapata wenye vipaji na kuviendeleza.

Tuna michezo mingi, soka, baiskeli riadha, mpira wa kikapu na michezo mingine timu zetu za taifa zimekuwa zikifanya vibaya kwenye mashindano mbalimbali kutokana na kukosa usimamizi mzuri.

Mashirikisho na vyama vya michezo ambavyo kimsingi ni wasimamizi wa karibu kwa ujumla wamekuwa wakilalamika kukosa watu wenye weledi na masuala ya utawala kiasi cha kushindwa kusimamia hata fedha kidogo wanazopata kwa wadhamini kuendesha shughuli hizo.

Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais John Magufuli, inatambua mchango wa sekta hiyo na inatarajia kuanza kutenga bajeti kusaidia maendeleo ya shughuli za michezo ili timu za taifa zifanye vyema kwenye mashindano mbalimbali.

Serikali imepania kufanya mabadiliko kuhakikisha Tanzania inarudia kwenye ubora kama ilivyokuwa miaka ya nyuma, ambapo timu za taifa ikiwemo ya mpira wa miguu, riadha na mingine zilikuwa zinafanya vyema kimataifa.

Pamoja na serikali kutoa ahadi hiyo kwa mashirikisho na vyama bado wamekuwa wakihimiza umuhimu wa viongozi husika kuwa wawazi katika matumizi ya fedha zinazotolewa na wadhamini kwa ajili kuwapa moyo wadhamini wengine kujitokeza kudhamini sekta hiyo.

Pia wanawaomba viongozi kufanya kazi kwa kushirikiana na serikali kwa ukaribu kwakuwa serikali imeandaa mpango wa kuona sekta hiyo inapiga hatua kwa kipindi cha miaka mitano .

Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Abdallah Ulega anasema mashirikisho pamoja na vyama vya michezo nchini ni wakati wa kujifunza kwenye mahesabu ya fedha na kutengeneza uwazi kuwalinda wadhamini waliopo na kuwavutia wengine.

Akizungumza jijini Dar es Salaam juzi wakati wa hafla ya kukabidhi hundi ya masomo kwa vijana 26 waliofanya vizuri katika mashindano ya mpira wa kikapu kwa udhamini ea Benki ya CRDB, Ulega pamoja na mambo mengine anasema hatua hiyo itazidi kuchochea ukuaji wa sekta ya michezo nchini.

Anasema kumekuwepo na malalamiko mengi kutoka kwa baadhi ya wadau wa michezo nchini juu ya ufujaji wa fedha zinazotolewa na wadhamini kwa ajili ya kudhamini ndani ya mashirikisho na vyama hivyo.

“ Kimsingi ni jambo linalowakatisha tamaa wadau hao kujitokeza kudhamini Michezo . “Kubwa hapa ni wahusika wote ndani ya vyama na mashirikisho ya michezo kuwa na weledi utakaowafanya wadhamini hawa kuwa na moyo wa kuendelea kujitokeza kudhamini michezo na kuibua vipaji vingi kutoka kwa vijana wetu,” anasema Ulega.

Aidha, akizungumzia udhamini huo wa CRDB kwa vijana 26 watakaokwenda kujiunga na masomo katika vyuo mbalimbali nchini, Ulega anaipongeza benki hiyo kwani huo ni mfano mzuri unaopaswa kuigwa na wadau mbalimbali yakiwemo makampuni.

“Niwapongeze kwa kuonesha mfano mzuri kwa kuwabeba vijana hawa lakini pia kuamua kudhamini mchezo huu wa basketball nchini, niwaombe wadau wengine kuendelea kujitokeza kudhamini mchezo huu na mingine ili kuongeza idadi ya wanamichezo nchini, “anasisitiza Ulega.

Aidha, anawataka vijana hao waliopata udhamini huo kwenda kufanya juhudi katika masomo na michezo pamoja na kuzingatia suala la nidhamu wakati wote wawapo vyuoni ili kujiweka katika mazingira mazuri ya kuwa wana michezo bora baadae.

“Michezo ni ajira kama utaonesha nidhamu ya kuheshimu kwani kuna vijana wengi wamefanikiwa kwenye maisha yao kupitia sekta hii, ambayo kimsingi mataifa mengine yametia nguvu,anasema Ulega.

Naye mjumbe wa Bodi ya benki hiyo, Martin Waioba akizungumza kwa niaba ya uongozi anasema udhamini kwa vijana hao umelenga kuendelea kuwapa motisha na wengine mashuleni na vyuoni kuweka mkazo katika michezo.

Anasema katika kuhakikisha wanaofika malengo yao ya udhamini wa vijana hao , benki hiyo imetoa kiasi cha zaidi ya Sh milioni 50 ili kufanikisha masomo kwa wanafunzi hao kwa kipindi cha mwaka mmoja.

Anasema utaratibu uliowekwa na benki hiyo, wataendelea kuwadhamini vijana hao katika miaka mingine ya masomo endapo watafanya vizuri katika mwaka wao wa kwanza wa masomo kwa kuzingatia vigezo walivyoviweka.

Kwa kawaida Msajili wa Klabu na Vyama vya Michezo anawajibika kupeleka wakaguzi wa hesabu katika mashirikisho hayo ili kujua vinatumiaje mapato yao, lakini hilo sidhani kama linafanyika,?

Chanzo: habarileo.co.tz