Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ukweli Ndivyo ulivyo: Kumbe tatizo wala sio makocha

84823 Makocha+pic Ukweli Ndivyo ulivyo: Kumbe tatizo wala sio makocha

Tue, 19 Nov 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

MASHABIKI wa Yanga kwa sasa roho zao zimetulia. Hii ni baada ya kuona Kocha Mwinyi Zahera keshatimuliwa. Sio kama Zahera alikuwa tatizo Yanga. Zahera kafurushwa kwa ule utamaduni wa klabu za soka za Tanzania. Ni ile kasumba kwamba timu ikifungwa tu, basi vyovyote iwavyo basi kocha hafai na lazima atimuliwe.

MASHABIKI wa Yanga kwa sasa roho zao zimetulia. Hii ni baada ya kuona Kocha Mwinyi Zahera keshatimuliwa. Sio kama Zahera alikuwa tatizo Yanga. Zahera kafurushwa kwa ule utamaduni wa klabu za soka za Tanzania. Ni ile kasumba kwamba timu ikifungwa tu, basi vyovyote iwavyo basi kocha hafai na lazima atimuliwe. Zahera wala sio wa kwanza na hawezi kuwa wa mwisho Yanga na hata kwenye timu nyingine. Ndio soka letu lilivyo! Mashabiki na hata viongozi na wanachama hawaangalii timu imefungwa na nani? Hawapendi tu kufungwa. Wanaona raha na kujisikia fahari timu zao zikishinda bila kujua zinashindaje! Sare ama kufungwa ni misamiati migumu vichwani mwao. Kwa sasa msala umehamia Msimbazi. Mashabiki na hata baadhi ya viongozi wameanza kumjadili Kocha Patrick Aussems. Wanataka atimuliwe klabuni. Ukiuliza sababu wala hakuna. Timu imecheza mechi tisa, imeshinda saba na kutoka sare moja na kupoteza moja kama watani wao, Yanga. Lakini tayari kocha ameonekana hafai. Ugonjwa ni ule ule. Mashabiki, wanachama na viongozi wameshamkinai. Uvumilivu kwa klabu za Tanzania ni mitihani kwa makocha. Ni tatizo kubwa kwa wachezaji wanaosajiliwa kwenye klabu hizo. Sio klabu tu hata, katika timu ya taifa. Leo Etienne Ndayiragije anaonekana lulu kwa vile tu Stars inapata matokeo mazuri. Ingekuwa imetolewa na Sudan katika mbio za CHAN 2020, asingepewa mkataba mpya wa kudumu katika timu hiyo na pengine angeshatimuliwa. Huyu Meddie Kagere angetua Simba na mguu mbaya kama aliotua nao Obrey Chirwa Jangwani, huenda habari ingekuwa nyingine! Wadau wengi wa soka sio  wavumilivu. Pia hawana heshima kwa timu pinzani. Vichwani mwao huamini timu zao ni bora na hazifungiki. Ikitokea zimefungwa, mzigo wa lawama hutupiwa makocha. Hawaangalii ubora wa vikosi vyao dhidi ya wapinzani. Hawaangalii ufundi unaotumika uwanjani na kujua udhaifu wa timu zao ni upi. Hawaangalii hata aina ya wachezaji waliopo kwenye vikosi vyao dhidi ya timu pinzani. Kwa mfano kwa sasa ukisikia kelele za watu wa Simba dhidi ya Aussems ni timu kushindwa kucheza vizuri, lakini wanasahau msimu uliopita Msimbazi ilikuwa imejaza wanaume wa shoka. Emmanuel Okwi, James Kotei, Haruna Niyonzima, Juuko Murshid, Asante Kwasi na Nicholas Gyan wote hawapo msimu huu. Wamewaacha wenzao, Meddie Kagere, Pascal Wawa na Clatous Chama kwa mapro wa kigeni kukinukisha na wazawa waliokuwapo msimu uliopita. Leo Simba mbele haina John Bocco aliye majeruhi. Utatu wa Bocco, Okwi na Kagere uliifanya timu itishe kwa kutupia nyavuni. Sio kwenye Ligi Kuu Bara tu hadi mechi za kimataifa, ndio maana haikuwa ajabu kwa Simba kufika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika 2018-2019.   Simba ya leo ukimdhibiti Kagere, basi hakuna wa kutupia nyavuni. Msimu uliopita akidhibitiwa yeye, Bocco na Okwi wanafunga. Akidhibitiwa Okwi, basi ujue Bocco na Kagere wanafunga. Akizuiwa Bocco, lazima Kagere na Okwi watupie. Simba ya leo ina Kagere pekee kama straika. Wilker da Silva bado hajawa fiti. Kuna watu Msimbazi waliamua kufanya biashara ya kuwaleta Wabrazili bila kufikiria. Naweza kubeti kwamba, hata Aussems hakujua ujio wa wachezaji hao, ila alitaarifiwa tu juu kwa juu kwa simu akiwa mapumziko Ulaya kwamba, ‘Tumekusajilia Wabrazili watatu watakusaidia’. Naye aliitikia tu; ‘hewala ngoja nirudi niwaone!’ Alipokwenda nao kambini Afrika Kusini aliwashtukia Wabrazili hao na kujua kabisa hawezi kufika mbali. Sio kwa Gerson Fraga, Tairone Santos da Silva wala Wilker. Hii ni kwa sababu soka la Afrika na viwanja vyake havikuwa rafiki kwa nyota hao wa Brazili. Waliowaleta Wabrazili hao Msimbazi, ni wazi walikuwa wanajua wanachokifanya. Walikuwa na kumbukumbu ya Gabriel Barbosa wa Coastal Union ya Tanga alivyochemka alipokuja nchini. Walikuwa wanajua namna Yanga ilitaabika na kina Andrey Coutinho na Geilson Santos Santana ‘Jaja’ walioletwa na Marcio Maximo. Ni wazi watakuwa wakumbuka hata alipoondoka Jaja baada ya kujishtukia mwenyewe, mbadala wake Emerson De Oliveira Neves Rouqe naye alichemka. Lakini, kwa kuwa wenye ‘dili’ waliamua kufanya mambo na kumuuzia Aussems mbuzi kwenye gunia na sasa wanamgeuka. Ukitafakari kwa kina unaweza usipate majibu, hivi kulikuwa na sababu gani za kuwatema kina Kotei na kuwaleta Wabrazili hao? Nyota waliondoka mikataba yao ilikuwa ikifahamika kwanini haukufanyika mchakato wa kuongeza mapema? Lakini, ishu hii haipo Simba tu, hata Yanga, Azam na klabu nyingine ni mwendo ni huo huo. Hao kina Maybin Kalengo, Issa Bigirimana, Juma Balinya, Muharami Issa ‘Marcelo’ na wengine ukifuatilia wametua Jangwani sio kwa mipango ya kocha, ila wachache fulani ndani ya timu. Hapo ndipo unapobaini kuwa kumbe lawama hizi wanazopewa makocha, wakati mwingine sio sahihi. wanabebeshwa mzigo wa lawama kwa makosa ya viongozi, wanachama na mashabiki wa soka wa klabu husika. Ukitaka kujua viongozi ndio tatizo, subiri dirisha dogo utasikia asilimia kubwa ya wachezaji waliosajiliwa dirisha kubwa, wanaachwa na kuchukuliwa wengine na klabu kubebeshwa mzigo wa kuvunja kandarasi zao. Kwa kuthibiti jambo hili ni wajibu kwa viongozi, wanachama na mashabiki wa soka ni kujenga utamaduni wa kuvumilia makocha na hata wachezaji na kuwaacha wafanyekazi zao bila kuingiliwa. Kama mabosi wa Chelsea wasingemuacha Frank Lampard afanye kazi yake bila kumuingilia ama kumghasi, huenda The Blues wasingekuwa hapo walipo katika Ligi Kuu ya England. Timu ilianza vibaya chini yake ikipoteza na kutoka sare mechi nyingine kuliko ilizoshinda. Lakini Lampard na vijana wake walivumiliwa na kufanya yao na leo wamekuwa moto kuliko ilivyotarajiwa. Klabu zinapaswa kuwavumilia makocha na wachezaji, pia zikijenga utamaduni wa kukaa nao muda mrefu kutengeneza timu zenye ushindani. Vinginevyo kila msimu tutashuhudia ingia toka ya makocha na wachezaji.

Chanzo: mwananchi.co.tz