Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ukuta Yanga labda upite angani

25014 Yanga+pic TanzaniaWeb

Thu, 1 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

KWA sasa Yanga ambayo iko chini ya kocha Mkongomani, Mwinyi Zahera inapiga zake mdogo mdogo na kunasa pointi tatu kila ikiingia uwanjani. Tangu kuanza kwa Ligi Kuu Bara msimu huu, Yanga haijapoteza mchezo na imetoka sare mara moja tu dhidi ya Simba, ambapo mchezo huo ulimfanya Zahera kuanza kuonekana tishio kwenye ligi kutokana na kikosi chake kuwa ngangari.

Lakini, kama hufahamu ni kuwa siri kubwa ya Zahera ni kusuka ukuta wenye mabeki katili na wanaotumia akili na nguvu nyingi katika kukabiliana na washambuliaji wakiwemo wale wasumbufu kama Middie Kagere na Emmanuel Okwi wa Simba.

Mbali na mabeki hao, pia ukuta wa Zahera una kipa aliyejikusanyia rekodi zake matata msimu huu, Benno Kakolanya ambaye amekuwa tatizo kubwa kwa washambuliaji wa timu pinzani.

Mara baada ya kubeba mikoba ya kuanza kuinoa Yanga, Zahera alitumia muda mrefu kusaka safu ya ulinzi huku akiwapiga benchi na kuwatosa baadhi ya mastaa akiwemo kipa Youth Rostand.

Takwimu zinaonyesha katika mechi saba za mwisho kwa Simba, Azam FC na Yanga ambao wako juu ya msimamo kwa sasa, Jeshi la Zahera limeonyesha uimara mkubwa katika safu yake ya ulinzi.

Licha ya kwamba haijapoteza mchezo mpaka sasa kama ilivyo kwa Azam FC, lakini katika mechi zake saba za mwisho imeshinda sita na kwenda sare moja dhidi ya Simba.

Katika ubora huo wa Yanga, kipa Kakolanya na mabeki wake wamecheza jumla ya dakika 630 bila kuruhusu bao.

Rekodi hiyo ya Yanga katika mechi hizo kwa karibu inaweza kunyemelewa na Azam, lakini wenyewe wakijitofautisha kwa kuruhusu bao moja pekee.

Azam iliruhusu bao hilo katika mchezo wa dhidi ya African Lyon kwa bao la Mganda Hood Mayanja na kuharibu rekodi ya kipa wao namba moja, Razack Abalora.

Abalora kwa bao hilo amezidiwa kidogo na Kakolanya kwa kufanikiwa kucheza dakika 540 bila wavu wake kuguswa akishika nafasi ya pili.

Simba ambao wanapiga mabao ya kutosha kwa sasa, ukuta wao bado haujafanya vizuri katika mechi zao saba zilizopita kwa kuruhusu mabao matatu.

Ukuta wa Simba ukiwa chini ya mzawa Erasto Nyoni, wageni Paschal Wawa na Juuko Murshid wamelegea kidogo kwa nyavu zao kutikiswa katika mechi tatu tofauti.

Mechi ambazo zimeiharibia Simba ambao ni mabingwa watetezi ni dhidi ya Mbao waliopoteza kwa bao 1-0 kisha kuifunga Mwadui 3-1 huku mechi ya mwisho ni dhidi ya Alliance nyumbani walioshinda kwa mabao 5-1.

Kipa namba moja wa Tanzania na Simba, Aishi Manula amejikuta akipunguza ubora wa takwimu akicheza jumla ya dakika 180 bila wavu wake kuguswa huku akicheza dakika 360 wavu wake ukiguswa.

Kocha wa Lipuli ya Iringa, Seleman Matola alikiri uimara wa Yanga uko kwenye safu ya ulinzi, imekuwa makini na kurekebisha makosa.

Alisema kama isingekuwa ubora wa mabeki wa Yanga na uzoefu walionao, kikosi chake kingeweza kupata bao ama kushinda kabisa kwenye mchezo huo.

“Tatizo kubwa kuifunga Yanga kwa sasa ni safu yake ya ulinzi, tulitengeneza nafasi nyingi za mabao, lakini kwa ubora na umakini wa mabeki mambo yalikuwa magumu sana,” alisema Matola ambaye ni kungo wa zamani wa Simba.

Kocha wa Simba Patrick Aussems aliwahi kukiri kwamba, wakati kikosi chake kinacheza na Yanga, alipata shida kuipenya ngome hiyo.

Aussems alisema safu ya ulinzi ya Yanga sio kwamba haifanyi makosa, lakini wanapofanya makosa ni rahisi kujipanga na kujisahihisha.

“Yanga wana safu nzuri ya ulinzi tulipokutana nao kama isingekuwa utulivu wa mabeki wao tungewapiga nyingi, wanafanya makosa na wanarekebisha kwa haraka. Wanajua kujipanga uwanjani na wanazungumza kila wakati,” alisema Aussems.

Mechi saba za mwisho Simba

Ruvu vs Simba 0-5

Simba vs Alliance 5-1

Simba vs Stand United 3-0

Simba vs African Lyon 2-1

Simba vs Yanga 0-0

Mwadui vs Simba 1-3

Mbao vs Simba 1-0

Mechi saba za mwisho Azam fc

Singida vs Azam 0-1

JKT Tanzania vs Azam 0-1

Azam vs African Lyon 2-1

Azam vs Coastal Union 2-0

Azam vs Tanzania Prisons 1-0

Azam vs Lipuli 0-0

Alliance vs Azam 0-1

Mechi saba za mwisho Yanga

Yanga vs Lipuli 1-0

KMC vs Yanga 0-1

Yanga vs Alliance 3-0

Yanga vs Mbao 2-0

Simba vs Yanga 0-0

Yanga vs Singida Utd 2-0

Yanga vs Coastal Union 1-0

Chanzo: mwananchi.co.tz