Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ukizubaa dakika hizi Simba, Nkana umeumia

31476 Simba+pic TanzaniaWeb

Thu, 13 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Kocha wa Simba, Patrick Aussems ameweka wazi anakwenda kuivaa Nkana Red Devils kwa kucheza soka la kushambulia, katika mchezo wa raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika huku rekodi zikionyesha timu hizo zinafunga sana mabao dakika 15 za mwisho katika kila kipindi.

Simba itavaana na Nkana mjini Kitwe, Zambia katika mchezo wa kwanza wa kuwania tiketi ya kuingia hatua ya makundi.

Aussems alisema hataki kuingia katika mchezo huo kupata sare ya ugenini ili aweze kuiondoa Nkana akiwa nyumbani, badala yake atacheza soka la kushambulia kama ilivyokuwa dhidi ya Mbabane Swallows na kupata ushindi mnono ugenini.

“Sina wachezaji wanaojilinda. Nina wachezaji wenye vipaji na uwezo mkubwa wa kushambulia, kwa hiyo tunakwenda kusaka ushindi ugenini,” alisema Mbelgiji huyo.

Simba inakwenda katika mchezo huo ikijivunia safu ya ulinzi iliyoruhusu mabao matano tu katika mashindano yote msimu huu.

Safu ya ulinzi Simba ikiongozwa na kipa Aishi Manula, mabeki Shomari Kapombe (majeruhi), Nicolaus Gyan, Mohammed Hussein, Erasto Nyoni na Pascal Wawa imeruhusu mabao manne tu kati mechi 12.

Ngome ya Simba itaanza kuonja misukosuko wakati itakapoikabili Nkana iliyoweka rekodi ya kufunga mabao 66 katika msimu huu wa Ligi Kuu Zambia.

Katika mabao 66, washambuliaji watatu walifunga mabao 40 ambao ni Idris Mbombo alifunga mabao 20, wakati Walter Bwalya na Ronald Kampamba kila moja akifunga mabao 10.

Siku zote namba hazidanganyi. Takwimu za Nkana na Simba kwenye michezo yao 10 iliyopita, zinaonyesha timu hizo huwa na kasi zaidi ya kufunga mabao kuanzia dakika ya 31 hadi 45 na dakika ya 76 hadi 90.

Ndani ya michezo 10, ambayo Simba imecheza ikiwemo miwili ya awali kwenye Ligi ya mabingwa Afrika dhidi ya Mbabane Swallows na tisa ya Ligi Kuu Bara, wameshinda jumla ya mabao 28.

Simba imefunga mabao saba kuanzia dakika ya 31 hadi 45 na sita katika dakika ya 76 hadi 90 za michezo 10 ya mwisho dhidi ya Mbabane Swallows, Lipuli, JKT Tanzania, Ruvu Shooting, Alliance, Stand United, African Lyon, na Mwadui FC.

Mchezo uliopita, Simba iliiondoa Mbabane Swallows kwa jumla ya mabao 8-1, katika mchezo wa kwanza Dar es Salaam, Novemba 28 ilishinda kwa mabao 4-1, ambayo yalifungwa na washambuliaji John Bocco dakika ya nane, (33), Meddie Kagere (80) na kiungo Clatous Chama dakika ya 90.

Katika mchezo wa marudiano, Simba ilishinda mabao 4-0, ambayo yalifungwa na Chama mara mbili kwenye dakika ya 28 na 32, Okwi (51) na Kagere dakika ya 63.

Hiyo inaonyesha namna gani vile ambavyo kikosi cha Mbelgiji Patrick Aussems kilivyo na kasi ya kushambulia kwenye dakika hizo za mwishoni mwa kipindi cha kwanza na pili.

Rekodi za Simba zinaonyesha mbali na mabao hayo saba ambayo wamepata kwenye dakika hizo, pia wana uwezo wa kufunga kuanzia dakika ya kwanza hadi ya kumi na tano na katika dakika hizo wana mabao matano.

Uhatari mwingine wa Simba, upo kipindi cha pili na takwimu zao zinaonyesha kuwa wamefunga mabao sita ndani ya michezo yao 10 ya hivi karibuni kuanzia dakika ya 76 hadi 90.

Pia wana uwezo wa kufunga dakika ya 16 hadi 30, wanamabao matatu, kuanzia dakika ya 46 hadi 60 wana mabao manne.

Wapinzani wao Nkana hawako nyuma ndani ya michezo yao 10 ya hivi karibuni wana jumla ya mabao 19 ambayo manne kati ya idadi hiyo wamefunga kuanzia dakika ya 31 hadi 45 huku matano yakiwa kipindi cha pili kuanzia dakika ya 76 hadi 90.

Katika mechi ya awali wa Ligi ya Mabingwa Afrika, Nkana ilitumia dakika zao za mwishoni mwa kipindi cha kwanza na pili kuwamaliza wapinzani wao UD Songo ya Msumbiji kwa jumla ya mabao 3-1.

Katika mchezo wa kwanza waliocheza Msumbiji, Nkana iliibuka na ushindi wa 2-1, ugenini yaliyofungwa na Harrison Chisala dakika ya 34 na Festus Mbewe dakika ya 80.

Wakati wa marudiano wakiwa nyumbani Zambia, waliumaliza mchezo dakika mbili za nyongeza baada ya 45 kumalizika kupitia kwa Kelvin Mubanda kuibuka na ushindi wa bao 1-0.

Pia Nkana wana uwezo wa kufunga kati ya dakika ya kwanza hadi 15 na 16 hadi 30 na 61 hadi 75 kila baada ya dakika hizo ndani ya michezo 10 wana mabao matatu.

Ni bao moja tu ambalo wamepata ndani ya michezo yao 10 ya hivi karibuni kuanzia dakika ya 46 hadi 60 na ilikuwa Oktoba 13 kwenye mchezo wa Ligi Kuu Zambia dhidi ya Lusaka Dynamos, lililofungwa na Idris Mbombo.

Hakuna ubishi hata kidogo kwamba mchezo wa Nkana na Simba, unaweza kuamuliwa kwa mabao yatakayofungwa mwishoni mwa kipindi cha kwanza na cha pili kutokana na rekodi zao zilivyo kwenye michezo yao 10 ya hivi karibuni.



Chanzo: mwananchi.co.tz