KAMA kuna mchezaji ndani ya Yanga anajiona bab’kubwa na kutaka kuzingua, basi asome mapema hapa kwani imeelezwa usajili uliofanywa msimu huu unamfanya kocha mkuu, Nasreddine Nabi asiumize kichwa na hakuna muda wa kubembeleza mtu kwa sasa.
Uongozi wa Yanga umesisitiza msimu huu una jambo lao na kwamba hawana muda wa kubembeleza mchezaji, kama akipigiwa simu halafu asipokee au akikosa mechi ajue namba inachukuliwa na wengine.
Hayo yamewekwa wazi na mjumbe wa Kamati ya Mashindano ya Yanga, Hersi Said alipokuwa akihojiwa jijini Dar es Salaam ambapo alisema hawana nafasi ya kumbembeleza mchezaji kama atashindwa kufuata matakwa na miongozo ya timu kwa sasa kikosini.
“Nyie si mmeona kuna mchezaji juzijuzi alifunga bao akamwaga machozi, si mmeona wenyewe. Hakuna anayetaka kupoteza nafasi yake kikosini,” alisema Hersi.
“Yanga inalipa mishahara yenyewe. Ina mifumo yake ya kuajiri watu sisi tuna-sapoti tu. Yanga ni timu kubwa huwezi kufananisha na wengine. Huwezi kumleta mchezaji kama Bangala (Yanick) halafu hajui mshahara analipwa na nani.”
Kuhusu suala la mikataba ya wachezaji aliweka wazi kuwa wachezaji wawili wa kigeni mikataba yao inakaribia kuisha na tayari wameshaanza mazungumzo nao.
“Kuna wachezaji wawili wa kimataifa mikataba yao ipo mwisho na mazungumzo yapo, ila kocha naye ana mahitaji yake,” alisema Hersi bila kuwataja, ingawa Mwanaspoti linafahamu nyota watatu wa kigeni wakiwamo washambuliaji Yacouba Songne na Saido Ntibazonkiza pamoja na kiungo Mukoko Tunombe mikata yao inaelekea ukingoni.
Chanzo cha ndani kutoka Yanga kililiambia Mwanaspoti kuwa, Ntibazonkiza amebakiza mwezi mmoja na Mukoko na Yacouba miezi saba kwa maana ya mwishoni mwa msimu huu mikataba yao inakwisha rasmi.
“Kwa upande wa nyota wa kigeni ni watatu tu hao, lakini wengine wote wana mikataba ya muda mtefu, ingawa nimesikia kuna mazungumzo sijajua nani ataachwa tusubiri muda ukifika,” kilisema chanzo hicho.