Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ukata waziweka njia panda Klabu Ligi Kuu

47826 UKATA+PIC

Thu, 21 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mwanza. Wakati Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa imefikia raundi ya 31 baadhi ya klabu zimedai zinaweza kushindwa kumaliza mashindano hayo kutokana na ukata mkubwa unaozikabili.

Kitendo cha Ligi Kuu kukosa mdhamini, kimezidisha ugumu wa timu hizo kushiriki kikamilifu mashindano hayo msimu huu.

Baadhi ya klabu zimefikia uamuzi wa kuachana na makocha wao na nyingine zinapiga hesabu ya kuwatema baadhi ya wachezaji wa kigeni kutokana na mtikisiko wa kiuchumi.

Klabu za mikoani zinazoshiriki Ligi Kuu zimeonekana kuathirika zaidi kulinganisha na Simba, Yanga ambazo zina udhamini wa Kampuni ya SportPesa.

Mtikisiko huo wa kiuchumi haukuiacha salama Stand United ambayo imeamua kuachana na kocha wake Amars Niyongabo raia wa Burundi kutokana na ukata.

Akizungumza na gazeti hili, Mwenyekiti wa Stand United, Elyson Maheja alisema wameachana na Niyongabo kwa kuwa hawana fedha za kumlipa mshahara na posho.

“Tuliamua kuachana na Niyongabo kutokana na hali ngumu ya uchumi baada ya kufanya hesabu tukaona hatutaweza kumgharamia,” alisema Maheja.

Pia Maheja alisema wanatafakari kuachana na wachezaji wa kigeni kwa kuwa hawawezi kulipa gharama kwa mchezaji mmoja Sh2 milioni kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

“Mchezaji wa kimataifa analipiwa Sh2 milioni hujaweka usajili, posho, mishahara na fedha za ITC. Sisi tulikuwa nao wanane sawa na Sh16 milioni ambazo ni karibu na bajeti ya klabu, sasa tutawalipaje”? alisema Maheja.

Mwenyekiti wa Mashindano wa Alliance FC, Yusuph Budodi alidai baada ya Ligi Kuu kukosa udhamini, wanatumia jina la taasisi kukopa fedha benki ili kuwahudumia wachezaji.

Alisema baadhi ya fedha wanatoa katika shule za taasisi hiyo na kulipa mishahara ya wachezaji na makocha jambo alilodai ni kinyume na utaratibu wa uendeshaji wa klabu.

Budodi alisema pia mfumo wa usimamizi wa soka hauna tija na alitoa mfano katika fedha za mapato za mechi dhidi ya Yanga licha ya kupatikana zaidi ya Sh40 milioni walipewa Sh19 milioni.

Akizungumzia suala hilo, Mwenyekiti wa Mbao Solly Njashi alisema njia pekee wanayotumia ni kuzungumza vyema na wachezaji na benchi la ufundi.

Mwenyekiti wa Biashara United, Selemani Mataso alisema wachezaji wanadai zaidi ya miezi miwili na hawana uhakika wa kumaliza mashindano hayo.

Katibu wa Mwadui, Ramadhani Kilao alisema mtikisiko wa kiuchumi umeiweka njia panda timu hiyo kama itamaliza ligi au vinginenvyo licha ya wachezaji wake kuonyesha uvumilivu.



Chanzo: mwananchi.co.tz