Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ukata kuzibeba Simba, Yanga

15527 PIC+UKATA TanzaniaWeb

Tue, 4 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Wakati tathmini ya mgawanyo wa mapato unaotokana na viingilio vya mechi ikionyesha klabu mwenyeji inapata fedha kiduchu kulinganisha na mapato ya jumla, hali hiyo inaweza kugeuka kuwa neema kwa Simba na Yanga.

Tathmini hiyo ilionyesha kwamba pamoja na kanuni za ligi kufafanua kuwa timu mwenyeji inapata mgawo wa asilimia 60 wa mapato yote yanayotokana na viingilio vya mchezo husika, kiuhalisia fungu la mgawo huwa chini ya asilimia 50 jambo linaloacha maumivu kwa klabu.

Kukosekana kwa mdhamini mkuu katika mashindano hayo, kumeonekana mwiba kwa klabu husika kwa kuwa zinapata fedha ndogo ambazo haziwezi kuendesha shughuli za kiutendaji.

Hata hivyo, hali ukata inaweza kugeuka neema Simba Yanga ambazo zinaweza kuitumia kama fursa ya kufanya vyema kwenye Ligi Kuu zikitumia unyonge wa mapato kiduchu ambayo klabu nyingine zinapata kutokana na mapato ya mlangoni na kukosekana kwa mdhamini mkuu.

Simba na Yanga ingawa nazo zitaumia kutokana na kupungua kwa mgawo wa wadhamini na kupata kiwango kidogo cha mapato ya mlangoni, zinaonekana zinaweza kumudu gharama za kujiendesha kwenye ligi wakitegemea vyanzo vingine.

Klabu hizo zina udhamini mnono wa fedha kutoka kampuni ya ubashiri matokeo ya SportPesa ambayo inazipa zaidi ya Sh930 milioni kwa mwaka ingawa miamba hiyo ina wadhamini wengine wanaoimarisha misuli yao ya kiuchumi.

Mbali na SportPesa, wadhamini wengine wa Yanga ni maji ya Afya na Azam Media wakati Simba wamo MO Energy na Azam Media.

Pia Simba na Yanga zinajivunia mtaji wa wanachama na mashabiki wake ambao huzichangia fedha ili kusaidia shughui za uendeshaji.

Mfano, hivi karibuni Yanga imekuwa ikiendesha kampeni ya kuichangia timu hiyo kwa njia ya simu za mkononi ambapo kwa mwezi uliopita ilikusanya Sh28 milioni wakati Simba ina kundi maalumu la kuichangia Sh 10 milioni kwenye kila mchezo ambao timu hiyo inacheza.

Pia Simba imekuwa ikibebwa na fedha za mfanyabiashara Mohammed Dewji ‘MO Dewji’ ambazo amekuwa akitoa kusaidia uendeshaji wa klabu hiyo, Yanga licha ya kutokuwepo kwa mwenyekiti wake, Yusuf Manji, imekuwa ikipata jeuri ya fedha zinazotolewa na kamati za mashindano na usajili, kugharamia mishahara, posho na huduma nyingine muhimu.

Baadhi ya viongozi wa klabu zinazoshiriki Ligi Kuu, wametoa maoni kwa nyakati tofauti kuhusu gharama za uendeshaji wa klabu unavyowaweka katika nafasi ndogo ya kutwaa ubingwa msimu huu.

Mwenyekiti wa Mbao, Solly Njasi alisema ukata wa uendeshaji kwa klabu hizo unaweza kuchochea wachezaji wasiokuwa waaminifu kurubuniwa na wapinzani ili kucheza chini ya kiwango.

Hata hivyo, alionya kuwa sheria itachukua mkondo wake ikibainika mchezaji au kiongozi wa klabu kuingia katika mtego wa kuhujumu timu kwa kisingizio cha ukosefu wa fedha.

“Ni kweli hali ni ngumu kuendesha timu hasa kipindi hiki ingawa kwa upande wetu tuna unafuu kidogo kwa kuwa tuna mdhamini, lakini kuna timu nyingin ni tatizo.

“Mfano hata katika mbio za ubingwa, timu kama Azam, Simba na Yanga zina nafasi nzuri ya mojawapo kuchukua taji kutokana na uwezo wao wa kifedha ambao umewasaidia kufanya usajili mzuri na hata kwenye mechi ziko vizuri, lakini timu nyingine zilizobaki zinajiendesha kulingana na hali iliyopo,” alisema Njasi.

Akizungumzia kanuni ya timu mwenyeji kuchukua mapato yote, alisema alikuwa miongoni mwa viongozi wa klabu walioshiriki kutengeneza kanuni hiyo na hana wa kumlaumu.

“Hili suala sio la TFF wala Bodi ya Ligi, sio kweli kwamba kwenye viwanja vya nje tulikuwa tunapata fedha nyingi, kuna mechi sisi tulicheza Manungu tukapata laki moja, Azam tumewahi kupata laki tatu, hivyo bora ujipange kuhamasisha mechi ya nyumbani ili kuchukuwa mapato yote,” aliongeza mwenyekiti huyo.

Naye Katibu Mkuu wa Kagera Sugar, Hamisi Madaki ana hofu ligi ya msimu huu ikakosa msisimko kutokana na ukata unaozikabili idadi kubwa ya timu zinazoshiriki Ligi Kuu.

Madaki alisema Simba, Yanga na Azam zina nafasi kubwa moja kati ya klabu hizo kutwaa ubingwa kwa kuwa zitakuwa kwenye ubora wao kulinganisha na timu nyingine.

“Mazingira ya soka letu yanaeleweka, lakini changamoto ni kubwa kanuni ya timu mwenyeji kuchukua mapato yote kwetu haitunufaishi na tunakoelekea kuna wasiwasi wa ushindani kukosekana baina ya timu zenye uwezo fedha na nyingine,” alisema Madaki.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Lipuli Ramadhani Mahano alidokeza ingawa wanapitia kipindi kigumu, lakini ni mufa mwafaka kwa mashabiki kujitokeza kwa wingi kwenye mechi za nyumbani ili kupata mapato yatakayopunguza makali na ugumu wa uendeshaji wa klabu.

Chanzo: mwananchi.co.tz