Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Uganda yaibeba Stars fainali Afrika

16619 Pic+uganda TanzaniaWeb

Tue, 11 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Pointi moja ya ugenini iliyopata Taifa Stars dhidi ya Uganda, itakuwa ni dhahabu kwa timu hiyo endapo itachanga vyema karata zake katika mechi nne zilizobaki za kuwania kufuzu Fainali za Afrika (Afcon) zitakazofanyika mwakani nchini Cameroon.

Baada ya kuonyesha kiwango bora kinachotia matumaini, Taifa Stars ina mlima mrefu mbele wa kupanda ili kukata tiketi ya kushiriki Afcon kupitia Kundi L ambalo pia lina timu za Uganda, Lesotho na Cape Verde.

Soka la nidhamu hasa kwenye safu ya ulinzi, kujitolea na kujituma kwa nyota wa Taifa Stars dhidi ya Uganda ‘The Cranes’ juzi usiku, limegeuka kivutio kwa wengi wakiamini linaweza kuwa chachu ya kufuzu fainali hizo.

Taifa Stars inayotakiwa kushika nafasi moja kati ya mbili za juu za kundi lake kufuzu Afcon baada ya kupita miaka 39 tangu iliposhiriki mwaka 1980, inapaswa kuitumia pointi moja iliyopata dhidi ya Uganda kama mtaji wa kutimiza malengo yake ingawa italazimika kupiga hesabu kali zitakazoibeba mbele ya Uganda, Cape Verde na Lesotho.

Katika michezo minne ambayo Taifa Stars imebakiza, italazimika kuvuna pointi tatu kwenye mechi mbili ilizobakiza ugenini dhidi ya Lesotho na Cape Verde.

Ushindi wa angalau mechi moja ugenini dhidi ya timu hizo maana yake utaongeza pengo la pointi baina ya Taifa Stars na timu husika, lakini pia utampunguza nguvu mpinzani mmoja katika vita ya kuwania kufuzu fainali hizo.

Endapo itatimiza lengo hilo, Taifa Stars itakuwa na kibarua kingine kigumu cha kupata pointi sita katika mechi mbili itakazocheza dhidi ya Cape Verde na Uganda.

Endapo hesabu hizo zitakwenda vyema Taifa Stars itamaliza hatua ya makundi ikiwa na pointi 11 ambazo pasipo shaka zitaiwezesha kumaliza katika moja ya nafasi mbili za kufuzu Afcon kwa kila kundi.

Tofauti na miaka ya nyuma, safari hii Taifa Stars ipo kwenye nafasi nzuri ya kufuzu Afcon kutokana na sababu kadhaa ikiwemo kundi kubwa la wachezaji wanaocheza soka la kulipwa nje ya nchi wakiongozwa na nahodha Mbwana Samatta anayecheza KRC Genk ya Ubelgiji.

Sababu nyingine inayoiweka Taifa Stars kwenye nafasi nzuri ya kufuzu Afcon ni kuongezeka kwa idadi ya timu zitakazoshiriki mashindano hayo kutoka 16 hadi 24.

Kwa mujibu wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF), makundi 12 ya kuwania kufuzu, yatatoa jumla ya timu 24 zitakazofuzu moja kwa moja kwenda fainali za mataifa ya Afrika.

Hilo linaweza kuchochea hamasa kwa wachezaji wa Taifa Stars kupata hamu ya kutaka kurudia kile kilichofanywa mwaka 1980 wakiamini ongezeko la idadi ya timu ni fursa kwao.

Sababu nyingine ni kucheza dhidi ya timu ambazo sio tishio kwa kiasi kikubwa na zinazoweza kufungika hata pindi zinapocheza kwenye viwanja vyao vya nyumbani.

Baada ya kumalizana na Uganda, Oktoba 10, Taifa Stars itaivaa Cape Verde ugenini kabla ya timu hizo kukabiliana tena jijini siku nne baadaye.

Kibarua kitakachofuata baada ya kucheza na Cape Verde, ni kuvaana na Lesotho ugenini, Novemba 16 na baada ya hapo mchezo wa mwisho ambao itacheza dhidi ya Uganda nyumbani, Machi 22 mwakani.

Kocha wa Taifa Stars, Emmanuel Amunike alisema matokeo ya sare sio mabaya kwa timu hiyo.

“Tunatakiwa kujitazama wenyewe kadri muda unavosogea. Hii ilikuwa ni mechi yangu ya kwanza tangu nilipoanza kazi siku nane (8) zilizopita.

Pia ni vyema tukaendelea kufanyia tathmini timu na kufanya kazi kwa kuzingatia tabia. Tulijiwekea malengo ugenini na tumefanikiwa kutimiza,” alisema Amunike.

Baadhi ya wadau wametoa maoni kuhusu kiwango cha Taifa Stars na maandalizi ya mchezo ujao dhidi ya Carpe Verde.

“Jana Stars walifanya vizuri ingawa kipindi cha kwanza ilionekana kucheza kwa kujilinda zaidi, lakini kipindi cha pili walifunguka, wanapokwenda kucheza na Cape Verde watulie na hakuna haja ya kwenda kujilinda, wapambane washinde huko,” alisema kocha msaidizi wa Simba Masoud Masudi.

Djuma alisema kiwango cha Cape Verde sio cha kuitisha Taifa Stars kama itaamua kufanya maandalizi kabambe na mapema kujiandaa na mchezo huo.

Aliyewahi kuwa kocha wa Taifa Stars, Abdallah Kibadeni alisema kocha ana kazi ndogo ya kutengeneza muunganiko wa washambuliaji Simon Msuva, Thomas Ulimwengu na Samatta.

“Changamoto iliyopo ni kutengeneza nafasi za kufunga, kujilinda hakuna faida tena katika mechi na Cape Verde, bahati nzuri washambuliaji tulionao wote wako ‘on fire’na kocha ameanza kuwaelewa hivyo atengeneze ‘chemistry’ ya washambuliaji.

“Cape Verde timu yao ya taifa wanapenda kutumia wachezaji wanaoishi nje ya nchi yao, lakini bado sio tatizo sababu Tanzania pia kwa sasa tuna kikosi kipana chenye uwezo wa kutupa matokeo, cha msingi ni kocha kutengeneza safu yake ya ushambuliaji vizuri,” alisema Kibadeni.

Chanzo: mwananchi.co.tz