Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Uchaguzi Yanga SC wachukua sura mpya

38352 Yanga+pic Uchaguzi Yanga SC wachukua sura mpya

Fri, 25 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeamuru Bodi ya Wadhamini wa Klabu ya Yanga, itangazwe gazetini kama njia ya wito wa kufika mahakamani kwa ajili ya kesi ya kupinga uchaguzi wa klabu hiyo iliyofunguliwa na wanachama wawili.

Amri hiyo ilitolewa jana na Hakimu Mkazi Mkuu Janeth Mtega, kufuatia maombi yaliyotolewa na wakili wa walalamikaji, Daud Mzeri, aliyedai imekuwa vigumu mdaiwa huyo kupokea hati ya wito iliyotolewa na mahakama.

Kesi hiyo ya kikatiba namba 1 ya mwaka 2019, imefunguliwa na wanachama wawili wa Klabu ya Yanga, Juma A. Magoma na Athman S. Nyumba, kupinga kufanyika uchaguzi huo kwa madai unakwenda kinyume na Katiba ya klabu hiyo.

Kesi hiyo iliyofunguliwa Januari 11, mwaka huu ilitajwa kwa mara ya kwanza mahakamani hapo jana, lakini wadaiwa wote wawili hawakuwepo mahakamani.

Mbali na Bodi ya Wadhamini wa Klabu ya Yanga, mdaiwa mwingine katika kesi hiyo ni Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), ambaye ndiye mdaiwa wa kwanza.

Wakati kesi hiyo ilipotajwa, Wakili Mzeri aliieleza mahakama kwamba wadaiwa wote leo hawajafika mahakamani na mdaiwa wa pili (Bodi ya Yanga) amegoma kupokea wito.

Hakimu Mtega alikubaliana na maombi hayo na akaamuru mdaiwa wa pili (Bodi ya Yanga) atangazwe gazetini kama njia ya wito wa kufika mahakamani na pia akaamuru mdaiwa wa kwanza (TFF) awasilishe utetezi wake.

Hakimu Mtega aliahirisha kesi hiyo hadi Februari 11, mwaka huu itakapotajwa mahakamani hapo.

Uchaguzi huo ulipangwa kufanyika Januari 13, 2019 kujaza nafasi zilizoachwa wazi, lakini haukufanyika baada ya kufunguliwa kesi hiyo.

Wanachama waliofungua kesi hiyo ya kikatiba namba 1/ 2019 ni Juma A. Magoma na Athuman S. Nyumba, ambao pamoja na mambo mengine, wanapinga kufanyika uchaguzi kwa madai unakwenda kinyume na Katiba ya Klabu ya Yanga.



Chanzo: mwananchi.co.tz