Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Uchaguzi Yanga Aprili 28

49182 Yanga+pic

Thu, 28 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Wakati Baraza la Wadhamini la Yanga likiunda kamati ndogo itakayosimamia mechi za timu hiyo, uchaguzi mkuu wa klabu hiyo umepangwa kufanyika Aprili 28, mwaka huu.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini la Yanga, George Mkuchika alisema wameunda kamati ya uchaguzi itakayokuwa chini ya mwanasheria nguli nchini Sam Mapande.

Wajumbe wengine ni Daniel Mlelwa, Mustapha Nagali, Godfrey Mapunda, Edward Mwakingwe, Samuel Mangesho, Issa Gavu, Venance Mwamoto, Seif Gulamali na Dastan Kitandula.

Akizungumzia hatima ya wagombea waliochukua fomu katika mchakato wa awali, Mkuchika alisema wagombea hao wanatakiwa kuchukua fomu upya klabuni hapo, lakini hawatalipa ada.

“Kama nilivyosema uchaguzi huu utakuwa chini ya Yanga na kila kitu kuanza kwake mpaka mchakato kukamilika mambo hayo yatafanyika hapa klabuni, lakini wagombea ambao walichukuwa fomu kule TFF wao watatakiwa kuchukua fomu hapa lakini hawatatozwa fedha zozote,”alifafanua Mkuchika

Pia Mkuchuka alisema wameunda kamati ya watu saba itakayosimamia kazi za Yanga ambayo itakuwa chini ya Mwenyekiti Lucas Mashauri.

Alisema kamati hiyo itakuwa na jukumu la kusimamia timu hiyo katika mechi zilizobaki mpaka watakapopatikana viongozi wapya katika uchaguzi mkuu wa Aprili 28.

Mkuchika aliwataja wengine Said Ntimizi ambaye atakuwa makamu mwenyekiti na wajumbe ni Hussein Ndama, Moses Katabaro, Maulid Kitenge, Hussein Nyika na Samuel Lukumay.

Alisema uamuzi wa kuwarudisha Lukumay na Nyika umetokana na ufanisi mzuri uliofanywa na wajumbe hao ambao jana walitangaza kujiuzulu nyadhifa zao.

Mkuchika alisema uzoefu wao umewapa nafasi ya kurudishwa katika kamati hiyo baada ya wajumbe wengine wawili Siza Lyimo na Thobias Lingalangala kujiuzulu wiki chache zilizopita.

“Naomba nieleweke hatujaunda kamati ya kuendesha timu, hiyo inakatazwa na Fifa (Shirikisho la Soka la Kimataifa).

“Sisi tumeunda kamati ya kusimamia timu kwamba itaondokaje kwenda kucheza mpira watalala wapi, lakini mambo ya uendeshaji yapo chini ya sekretarieti,” alisema Mkuchika.



Chanzo: mwananchi.co.tz