Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Uchaguzi Bodi ya Ngumi wageuka kaa la moto

44184 BMTR+PIC Uchaguzi Bodi ya Ngumi wageuka kaa la moto

Thu, 28 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Siku chache baada ya Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kutangaza tarehe ya uchaguzi wa Bodi ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBRC), baadhi ya wadau wamepinga kitendo cha mabondia wakongwe kuenguliwa katika mchakato huo.

Kamati iliyoundwa kuratibu mchakato wa uchaguzi imesema watakaoruhusiwa kupiga kura ni mabondia wanaocheza ngumi, kocha au wakala ambao watapata vitambulisho maalumu vya kupigia kura.

Akizungumza jana, Makamu mwenyekiti wa kamati hiyo, Joe Anea alisema mabondia waliostaafu ngumi na hawako katika mchezo huo hawatakuwa na sifa ya kupiga kura.

“Mapromota, makocha, waamuzi na mawakala walio hai watapiga kura, lakini lazima wawe na vitambulisho. Mfano Rashid Matumla ataruhusiwa kama atakuwa ni kocha, promota au anafanya uwakala kinyume na hapo hana nafasi,”alisema Anea.

Kamati hiyo imeweka utaratibu bondia atanunua kitambulisho Sh12,000, mwamuzi na kocha Sh20,000 na promota au wakala Sh50,000.

Kauli ya Anea imekuja baada ya baadhi ya wadau kulalamikia muda mfupi wa kampeni wakidai wana wasiwasi huenda kuna baadhi ya wagombea wameandaliwa kushinda katika uchaguzi huo.

Wasikie mabondia

Utaratibu huo umewaibua baadhi ya mabondia nguli akiwemo Ally Bakari ‘Champion’ ambaye alisema uamuzi wa kamati hiyo hautendi haki katika ustawi wa maendeleo ya ngumi nchini.

Alisema utaratibu huo unawanyima fursa wadau wengi wa ngumi kufanya uamuzi wa kupata viongozi wa Bodi ambao wanawasubiri muda mrefu.

“Tulikubaliana mabondia wote ambao wanatambulika kwenye mtandao wa ngumi za kulipwa waruhusiwe kupiga kura. Katika uchaguzi ujao uwekwe utaratibu mzuri wa wanachama,” alisema Bakari.

Bakari alisema mabondia nguli wanatambua matatizo ya ngumi, wanajua ubora na ubovu wa viongozi waliopita, hivyo ingekuwa rahisi kwao kuchagua watu sahihi katika uchaguzi huo.

“Wangeachwa mabondia wa zamani nao washiriki, sioni sababu ya kuwaengua wakati wanajulikana, sijui kwanini imekuwa hivyo ngoja tuone mwisho wake,”alisema bondia wa uzito wa juu Alphonce Mchumiatumbo.

Kauli ya BMT

Akizungumzia utaratibu wa kupiga kura, Ofisa Habari wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Najaha Bakari alisema watakaoshiriki ni wale waliosajiliwa.

“Waliambiwa wanapaswa kujisajili wale wote watakaokuwa wamesajiliwa na kutambulika ndiyo watapiga kura,” alisema Najaha.

Pia Najaha alisema hakutakuwa na muda kuongeza wakati wa kampeni na utaratibu uliowekwa na baraza hilo utabaki kama ulivyotangazwa.

“Hata kabla ya kutangaza uchaguzi baadhi walianza kampeni za chini chini, niwambie BMT haitaongeza muda wa kampeni,” alisisitiza Najaha.

Juzi, BMT ilitangaza Machi 25 kuwa mwisho wa kuchukua fomu na Machi 29 itakuwa siku ya usaili kwa wagombea na siku inayofuata Machi 30 utafanyika uchaguzi.



Chanzo: mwananchi.co.tz