Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ubabe Makambo, Wawa kuziponza Yanga na Simba

20801 Pic+makambo TanzaniaWeb

Thu, 4 Oct 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Wakati Simba ikiendelea kumkosa nahodha John Bocco katika mashindano ya Ligi Kuu Tanzania Bara kwa kuonyeshwa kadi nyekundu dhidi ya Mwadui FC, timu hiyo iko hatarini kuwakosa wachezaji wengine wawili muhimu wanaonyemelewa na adhabu ya kufungiwa na faini kutokana na kosa kama hilo.

Licha ya kutoonyeshwa kadi nyekundu kwenye mechi dhidi ya Yanga, kiungo James Kotei na beki Pascal Wawa kwa nyakati tofauti walifanya makosa ya utovu wa nidhamu kwa kuwapiga ngumi Gadiel Michael na Heritier Makambo, kosa ambalo walistahili kuonyeshwa kadi nyekundu.

Mbali na hao, adhabu hiyo huenda ikawakumba Makambo aliyempiga kiwiko Wawa na beki Andrew Vincent ‘Dante’ ambaye alionekana akimpiga kichwa beki wa kushoto wa Simba Mohammed Hussein ‘Tshabalala’.

Hata hivyo Wawa, Kotei, Dante na Makambo walinusurika kukutana na makucha ya mwamuzi Jonesia Rukyaa wa Kagera, baada ya kufanya makosa hayo kwa nyakati tofauti katika mchezo huo uliomalizika kwa miamba hiyo kutoka suluhu.

Wawa anayecheza nafasi ya beki wa kati alikuwa mwanzilishi wa tukio hilo baada ya kumpiga ngumi Makambo wakati mshambuliaji huyo wa Yanga alipokuwa akiwania mpira wa kona langoni mwa Simba.

Picha za marudio ya televisheni, zilionyesha Wawa akimchapa ngumi hiyo dakika ya 27 baada ya Makambo kumpiga kiwiko katika harakati ya kuwania mpira.

Kupitia marudio hayo na ushahidi wa picha za video, dakika sita baadaye Kotei alimpiga ngumi beki wa Yanga, Gadiel ingawa naye alinusurika hadi akamaliza mechi hiyo pasipo kuonyeshwa kadi.

Tukio jingine ni lile la dakika ya 61 ambalo Dante alimpiga kichwa Tshabalala baada ya majibizano ya sekunde kadhaa ingawa nalo halikuonwa na mwamuzi Jonesia.

Matukio hayo yametokea kabla hata haijatimia wiki moja tangu Bocco alipoonyeshwa kadi nyekundu ya moja katika mchezo dhidi ya Mwadui FC baada ya kumpiga ngumi beki Revocatus Mgunga.

Hata hivyo, tofauti na wenzake, Bocco ameanza kutumikia adhabu ya kukosa mechi tatu kutokana na kadi nyekundu aliyoonyeshwa. Tayari mshambuliaji huyo amekosa mechi dhidi ya Yanga iliyochezwa, Jumapili lakini huenda akaongezewa adhabu ya faini Sh500,000 kwa mujibu wa kanuni.

Ingawa Kotei, Wawa, Dante na Makambo hawakuonyeshwa kadi nyekundu, kanuni za Ligi Kuu 2018/2019 zinafafanua kuwa mchezaji yeyote anayefanya makosa ya namna hiyo anafungiwa kucheza michezo kuanzia mitatu na faini Sh500,000.

“Mchezaji atakayetolewa nje kwa kadi nyekundu kwa kosa la kupiga/kupigana atasimama kushiriki michezo mitatu (3) inayofuata ya klabu yake na atalipa faini ya Shilingi 500,000 (laki tano),” inafafanua ibara ya tatu ya kanuni hiyo ya udhibiti kwa wachezaji.

Kaimu Mwenyekiti wa Kamati ya saa 72 Shani Christoms, alipoulizwa kuhusu matukio ya utovu wa nidhamu yaliyotokea katika mchezo huo, alimtaka mwandishi kuwasiliana na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi, Boniface Wambura ambaye ndiye msemaji wa kamati hiyo.

Akizungumza jana, Wambura alisema kamati hiyo itakutana wakati wowote wiki hii kujadili matukio yaliyotokea katika mchezo huo wa watani wa jadi.

“Hizo ‘clip’ zinazotembea za mchezo wa Simba na Yanga ndizo zinatukutanisha, lakini siwezi kuzungumzia hatua ambazo tutachukua hadi kamati itakapokutana,” alisema Wambura.

Yanga inashika nafasi ya pili katika msimamo wa ligi ikiwa na pointi 13 na watani wao wa jadi Simba, wako nafasi ya tano kwa pointi 11.

Chanzo: mwananchi.co.tz