Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

USAJILI SIMBA, YANGA, AZAM WAPAMBA MOTO

7735719715db8d218833f5f18db0c87f USAJILI SIMBA, YANGA, AZAM WAPAMBA MOTO

Wed, 5 Aug 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

MABINGWA wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba wametajwa katika tetesi za usajili wa kimataifa wakivizia saini za wachezaji Jesse Were wa Zesco United na beki wa klabu ya Chippa United ya Afrika Kusini, Frederic Nsabiyumva.

Were ambaye ni mchezaji wa timu ya taifa ya Kenya, aliwahi kuzichezea Mathare United na Tusker za nchini kwake kabla ya kujiunga na Zesco ya Zambia. Pia, Nsabiyumva ni mchezaji wa timu ya taifa ya Burundi aliyewahi kuichezea Atletico Olimpic Bujumbura, akajiunga na Jomo Cosmos na mwaka juzi akajiunga na Chipa United.

Licha ya klabu hiyo kutoweka wazi juu ya usajili huo, Mtendaji wa klabu hiyo Senzo Mazingisa, hivi karibuni alisema wanatarajia kufanya maboresho ingawa wanapata wakati mgumu wa kuamua nani wa kumuacha ili kufanya ingizo jipya. Alisema watasajili kulingana na ripoti watakayopewa na kocha Sven Vandebroeck kujiandaa na michuano ya kimataifa mwakani.

Kwa upande wa Yanga, licha ya kusajili wachezaji wanne wazawa, bado inatajwa huenda wakati wowote ikawatangaza Salum Abubakari kutoka Azam FC na Farid Mussa kutoka Tenerife ya Hispania na baadaye itahamia kimataifa.

Wachezaji iliowasajili mpaka sasa ni Waziri Junior kutoka Mbao, Yassin Mustapha kutoka Polisi Tanzania, Bakari Mwamnyeto kutoka Coastal Union na Zawadi Mauya kutoka Kagera Sugar.

Kwa upande wa Azam FC, imewasajili Ally Niyonzima kutoka Rayon Sport ya Rwanda, Ismail Aziz kutoka Tanzania Prisons, Awesu Awesu kutoka Kagera Sugar na Ayoub Lyanga kutoka Coastal Union.

Chanzo: habarileo.co.tz