Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

UNAWAKUMBUKA?: Walivuma, wakapotea ghafla

14075 Pic+wakapotea TanzaniaWeb

Mon, 27 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara umerejea na majina kadhaa ya wachezaji wa kigeni kwa Yanga yupo, Herietier Makambo na Simba kuna mtu anaitwa Meddie Kagere.

Makambo ambaye ni mchezaji wa zamani wa FC Saint-Éloi Lupopo ya DR Congo alitua Yanga kama mchezaji huru baada ya mkataba wake na klabu aliyokuwa akiichezea kumalizika.

Mshambuliaji huyo raia wa DR Congo ameonekana kuwa moto wa kuotea mbali na aliweka rekodi katika mchezo wa kwanza wa Yanga wa msimu ambao walicheza dhidi ya Mtibwa Sugar Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Rekodi hiyo, Makambo aliyoiweka ni ya kufunga bao la kwanza la msimu wa 2018/19 kwa upande wa Yanga ambayo inatajwa kuanza taratibu kurejea kwenye kasi yao ya ushindani.

Meddie Kagere naye aliweka rekodi mbili, Agosti 22 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, rekodi ya kwanza ilikuwa ni kufunga bao la kwanza la msimu kwa upande wa Simba na nyingine bao lake limekuwa bao la mapema zaidi kufungwa msimu wa 2018/19.

Kagere aliiandikia bao Simba dakika ya pili kwenye mchezo dhidi ya Tanzania Prisons ambao wameuanza msimu bila ya washambuliaji wao hatari wa msimu uliopita, Mohammed Rashid ambaye yupo Simba na Eliuter Mpepo ambaye alitimkia Singida United.

Spoti Mikiki inakuletea nyota wa Kigeni ambao walitua nchini na mbwembwe kibao lakini mwisho wa siku walishindwa kuonyesha makali yao, je!! Kagere na Makambo nguvu zao ni za soda kama waliokuja na kuchemsha?

Kinachoweza kutoa jawabu la Swahili hilo ni muda hakuna kingine zaidi. Kundi la wachezaji wa kigeni waliochemsha nchini linaongozwa na Wabrazil wa Yanga, Andrey Coutinho na Genilson Santos ‘Jaja’ huku kwa upande wa Simba akiwa Laudit Mavugo.

Rostand Youthé/ Yanga

Mkameroon Rostand alijiunga na Yanga, Julai Mosi 2017 akitokea African Lyon ambayo msimu wa 2016/17 ilishuka daraja, kufanya kwake vibaya akiwa na watani hao wa Simba kulimgharimu kipa huyo ambaye mkataba wake umekatishwa wiki chache zilizopita. Akiwa Lyon alionyesha uwezo mkubwa ikiwemo kuwakatalia washambuliaji wa Simba na Lyon kuifunga Simba bao 1-0 na hapo ndipo Yanga ikamchangamkia.

Laudit Mavugo/ Simba

Mavugo alijiunga na Simba, Julai mosi 2016 akitokea Vital’O FC ya nchini kwao Burundi, mshambuliaji huyo alianza kwa kasi na taratibu akaanza kupoteza nafasi ya kucheza mara kwa mara kwenye kikosi cha kwanza cha timu hiyo.

Yahaya Mohammed / Azam

Mohammed ambaye ni raia wa Ghana alisajiliwa na Azam FC, aitokea Aduana Stars, lakini alishindwa kudumu katika kikosi cha Azam FC kutokana na kushindwa kuendana na kasi ya timu hiyo na mwishowe aliamua kurejea kwenye klabu yake ya zamani nchini kwao.

Justine Zulu/ Yanga

Yanga ilimnasa kiungo mkabaji wa ZESCO United, Zulu kwa lengo la kuziba pengo la kiraka Mnyarwanda mwenye asili ya DR Congo, Mbuyu Twite aliyekuwa akifanya vizuri kwenye eneo la kiungo mkabaji.

Kiungo huyo aliyejiunga na Yanga Novemba 30, 2016 aliondolewa kwenye kikosi hicho Januari mosi 2017.

Dan Sserunkuma/ Simba

Dan mwenye umri wa miaka 24, alitua nchini Januari 25, 2015 akitokea Gor Mahia FC ya Kenya kwa mbwembwe zote lakini alishindwa kuonyesha makali yake na kuamua kutimkia zake Armenia kwenye klabu ya Ulisses.

Allan Wanga / Azam

Mshambulizi wa timu ya taifa la Kenya Harambee Stars alionwa na matajiri wa Dar es Salaam, Azam FC alipokuwa anaitumikia timu yake ya Al-Merreikh ya Sudan na akasajiliwa na matajiri hao.

Wanga hakumaliza msimu Azam aliondolewa na baadaye akajiunga na Tusker msimu wa 2016/17 ambapo pia hakuwa na msimu mzuri na kuamua kujiunga na Kakamega Homeboyz ambapo ndio anacheza hadi sasa.

Saimon Sserunkuma / Simba

Mdogo wake na Dan, Saimon naye alichemsha na kaka yake kwenye kikosi cha Simba kwa pamoja msimu wa 2015/16.

Nyota hao waliondoka wakidai soka la Tanzania linamalizwa na mambo ya kishirikina ‘misumari’.

Mara baada ya Dan kutimkia Armenia na baadaye kuzichezea Bandari FC, Ittihad Tange, Express FC na Vipers SC, Saimon alijiunga na Express FC ya Uganda mara baada ya kuondoka Simba.

Genilson Santos ‘Jaja’/ Yanga

Kipindi alichotua Yanga, Marcio Maximo alikuja na wachezaji wawili wa Kibrazil akiwemo Jaja, mshambuliaji huyo alishindwa kuonyesha makali yake akiwa na kikosi hicho na mara baada ya kutimuliwa kwa Maximo naye akatimuliwa.

Raphael Kiongera/ Simba

Ni mshambuliaji ambaye alitua nchini kwa mbwembwe nyingi kama ilivyo kawaida kwa watani Simba na Yanga pale wanapomsainisha mkataba mchezaji kutoka nje ya Tanzania lakini hakuweza kufanya vizuri na baada ya kupata majeraha ndiyo malango wake wa kutokea ulipofunguliwa.

Kiongera alijiunga na Simba akitokea KCB ya nchini Kenya msimu wa 2014/15 hakuweza kudumu kikosini baada ya kupata majeraha na baadae akatolewa kwa mkopo na kurudishwa tena KCB ambapo pia hakudumu na kuamua kujiunga na A.F.C Leopald.

Andrey Coutinho/ Yanga

Coutinho ndiye angalau alianza kuwaingia mashabiki wa Yanga na hata baada ya Maximo kutimuliwa na Jaja alisalia kwa miezi kadhaa kabla na yeye kushindwa kuonyesha makali yake na kupoteza namba ya kucheza kwenye kikosi hicho.

Samuel Afful/ Azam

Afful alisajiliwa na Azam mwanzoni mwa Disemba, 2016 lakini hakufanikiwa kuingia kwenye kikosi cha kwanza cha timu hiyo na mara baada ya mkataba wake kumalizika akaachwa Februari 13, 2018 na kwenda kujiunga na Al-Talaba SC ya Iraq.

Kpah Sherman/ Yanga

Yanga ilimnasa Sherman aliyekuwa na umbile kubwa, 2014 akitokea Cetinkaya TSK ya Cyprus na alipotua alishindwa kuonyesha makali yake ya ufungaji na ilipofika Agosti 2, 2015 Yanga waliamua kuachana naye.

Sherman alitimkia zake Afrika Kusini kwa kwenda kuichezea Black Aces na baadaye akazichezea Santos FC, Cape Town City na MISC-MIFA ya Malaysia.

Stephan Kingue / Azam

Kingue alikuwa mmoja wa viungo bora wakabaji Ligi Kuu Tanzania Bara kipindi alichotua Azam, lakini majeraha yalimfanya taratibu kupoteza ubora wake na hatimaye kuchemka kwenye kikosi cha matajiri hao ambao waligoma kumuongeza mkataba mpya.

Kingue anatajwa kurejea kwao Cameroon kabla ya kiungo huyo kutua Azam Desemba 14, 2016 alizichezea klabu kadhaa nchini kwao zikiwemo Cotonsport na Racing Bafoussam.

Steven Bengo / Yanga

Yanga iliachana na Bengo, 2010 kutokana na kutokuwa na kiwango bora cha kuendelea kuitumikia timu hiyo, majeraha ya mara kwa mara yalihusishwa kuporomosha kiwango cha kungo huyo mzaliwa wa Rugaba nchini Uganda.

Bernard Arthur/ Azam

Arthur aliendelea kuwa kwenye rekodi za wachezaji wa Kighana ambao asilimia kubwa wamekuwa wakishindwa kuonyesha makali yao nchini hasa wale ambao wamekuwa wakisajiliwa na Azam.

Waghana pakee ambao wapo kwenye kiwango bora kwa muda mrefu kwenye kikosi cha Azam ni beki wao wa kati, Yakubu Mohammed na kipa Razak Abalora.

Kilichomtokea Arthur aliamua kukaa chini na viongozi wa klabu yake ya Azam na kuamua kukatisha mkataba wa kuendelea kuitumikia timu hiyo.

Hiyo ni baada ya kuanza kupoteza nafasi ya kucheza mara kwa mara kutokana na kutoonyesha makali katika michezo aliyokuwa akicheza kikosi cha kwanza.

Chanzo: mwananchi.co.tz