Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

UKWELI NDIVYO ULIVYO: Maxime tumeanza kukuelewa buana!

92149 Pic+mexime UKWELI NDIVYO ULIVYO: Maxime tumeanza kukuelewa buana!

Mon, 17 May 2021 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

HATA mimi nilipomsikia kwa mara ya kwanza, Mecky Maxime, sikumwelewa! Maneno aliyotamka nyota na nahodha huyo wa zamani wa Mtibwa Sugar na Taifa Stars, yaliyowachanganya wengi. Mimi nikiwamo! Haikuwa rahisi kumwelewa.

Maxime, alikaririwa akisema soka letu linaendeshwa na watu wajinga wajinga. Watu wasiolijua vyema soka letu. Ni maneno makali na yanayochoma.

Ni kauli inayochonyota, ndio maana sikushangaa saa chache baadaye Shirikisho la Soka nchini (TFF), likatoa waraka kukemea jambo hilo, japo halikumtaja moja kwa moja Maxime.

Ilionyesha ni kama vile TFF ilijishtukia imepigwa dongo wao. Klabu yake ya zamani nayo ilitoa ujumbe. Ilionekana kama kijembe kile kiliwahusu wao zaidi.

Jambo zuri ni katika kauli yake, Maxime hakumtaja yeyote. Uliwachapa wengi. Waliojishtukia ndio waliojitokeza kumjibu, tena kwa mafumbo na ilitosha kutoa somo kwa wadau, soka letu linaendeshwa na wengi wenye sifa zilizoainishwa na kocha huyo kijana mwenye maneno ya shombo.

Narudia tena awali wala sikumuelewa Maxime aliwalenga kina nani?

Hata hivyo, baada ya sarakasi zilizojitokeza Jumamosi iliyopita kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa nilianza kumwelewa sana. Tukio la kushindwa kupigwa kwa pambano la watani wa jadi, Simba na Yanga kwa sababu ambazo hazikuwekwa wazi ilitosha kuonyesha Maxime hakukurupuka kwa alichokisema. Lile neno halikumponyoka. Alijua anachokisema! Soka letu linaendeshwa kibabaishaji na waliopewa dhamana ya kulisimamia hawajali kitu. Wanachukulia taasisi kama mali zao binafsi, hivyo wana uhuru wa kufanya lolote, bila kujali athari zinazojitokeza!

Fikiria tu, pambano linasogezwa mbele na kushindwa kuchezwa kabisa kwa kilichoelezwa ni maagizo kutoka juu. Kauli hizi za ‘maagizo kutoka juu’ tulizoea kuzisikia kwenye ishu za kisiasa, zikitolewa hasa kwa viongozi wasiojiamini. Kauli zilizowaumiza wengi, kama zilivyowaumiza mashabiki waliosafiri kutoka mbali kuja kuzishuhudia Simba na Yanga Kwa Mkapa. Waliopoteza muda wao na fedha. Yaani hivyo tu!

Na kibaya zaidi hata walipokumbushia viingilio vyao, walizawadiwa mabomu ya machozi. Starehe waliyoifuata ikageuka kuwa dhahama kwao!

Mshangao zaidi ni danadana zilizojitokeza baadaye. Ukisikiliza walichokuwa wakikisema wahusika waliokwamisha mchezo huo wa 106 kwa watani katika Ligi ya Bara tangu 1965 kufanyika, kuwa ni agizo la serikali utabaini halikuwa la kweli.

Kama ilikuwa ni serikali iliyotaka mchezo usogezwa mbele, isingekuwa rahisi yenyewe iishangae! Kama ilitolewa na TFF, mbona hata wao nao walishangaa? Kama ni ya Bodi ya Ligi imekuwaje nao wakashangaa? Klabu nazo zikashangaa na zilishindwa hata kuwaheshimu mashabiki wao.

Nilisoma posti ya Madame kabla ya kuifuta katika akaunti yake ya Twitter ikiwa na kipengele kilichokuwepo pia kwenye waraka wa kuchosha wa klabu yake, nikabaini bado tuna safari ndefu kwenye soka letu!

Ukisoma ule waraka wa Simba ulioonekana wazi haukuandikwa na mtu mwenye weledi na uliojaa ubabaishaji, utabaini wazi kuna kitu ilichokuwa nyuma ya kuahirishwa kwa mchezo huo. Ilijenga hisia pengine wao ndio walisababisha mchezo usipigwe katika muda wa awali wa saa 11:00 jioni. Kwa hapo kwa nini Maxime asipate pointi tatu kwa kauli yake?

Klabu inayoendeshwa kisasa katika dunia ya kileo inawezaje kutaka pointi za mezani? Inawezaje kuinanga klabu pinzani eti ni wasaliti wa nchi na serikali, kwa ishu waliyoajua wazi inavunja kanuni ya soka na litakalowatesa mashabiki waliojaza uwanjani?

Siku zote TFF, Bodi ya Ligi na klabu zimekuwa zikihimiza suala la kuzingatia kanuni na sheria za soka. Hakuna mahali kokote katika waraka wao walikiri kulikuwa na ukiukwaji mkubwa wa kanuni ya muda wa uahirishwaji wa mchezo ambao Yanga waliamua kuing’ang’ania. Ni kama vile wenyewe waliona ilikuwa sahihi mechi kuahirishwa ndani ya muda mchache kabla ya kuchezwa tena bila sababu za maana. Mechi ingekuwa na uhalali wa kusogezwa mbele au kurudishwa nyuma kama kungekuwa na ishu ya kiusalama au majanga ya kiasili kama inavyokubalika, tena isingefanywa siri. Ingeainishwa katika taarifa ya TFF ya kuahirishwa ili isilete mkang’anyiko! Soka letu linachekesha sana, we fikiria kama katika dunia ya sasa tena kwa klabu inayoendeshwa kisasa, inazililia pointi za mezani bila kuzitolea jasho?

Sitetei wala simnangi yeyote, kwani hata hao Yanga, licha ya usahihi kwa ilichokifanya, lakini nao, waliwakosea adabu mashabiki waliojazana uwanjani. Wangewafikiria walivyohenyeka tangu asubuhi kuwasubiri uwajani, hata kama ni kweli kanuni zilipindishwa. Hii ni kwa sababu ni mara ngapi kanuni hizo zimekuwa zikipindishwa na wao kuridhia?

Inawezekana Yanga ‘imewakomoa’ TFF, kwa yale ambayo imekuwa ikiwafanyia. Pia kwa hisia zao kuwa, viongozi wa juu wa TFF wana mahaba kwa wapinzani wao kiasi cha kuionea hata katika haki inazostahili na ilipotokea nafasi ile wiki iliyopota,ikaona liwale na liwe na bahati imeeleweka sana!

Hata kama mchezo huo utachezwa upya, bado kuna darasa limepatikana kupitia tukio hilo la Jumamosi. Sio kwa Simba na Yanga tu, bali hata kwa viongozi wa TFF, TPLB na serikali iliyobebeshwa mzigo kutokana na taarifa iliyotolewa na TFF mapema kwamba mchezo unasogezwa kwa agizo lao.

Hata kama inafichwa, lakini zipo hisia kulikuwa na mpango wa Rais Samia Suluhu kuhudhuria kwenye mchezo huo, lakini bado inaonekana mipango ni kama ililazimishwa na iliwasahau watazamaji waliofurika mapema Kwa Mkapa.

Uwanja usio na huduma kama viwanja vya wenzetu, ambazo zingeweza kuwafanya mashabiki wasichoshwe kwa muda wa ziada kusubiri mchezo huo.

Hii isaidie wafikirisha hata wamiliki wa viwanja kuweka huduma za vyakula, vinywaji na hata malazi, kusaidia kutoa nafuu kwa wanaoenda kwenye viwanja hivyo.

Nimalizie kwa TFF na TPLB, kama ni kweli kulikuwa na mipango wa Mama kuhudhuria ilikuwaje hawakujipanga mapema? Walishindwa nini kuliweka wazi hilo kwa klabu katika mkutano kabla ya mchezo (pre match meeting) asubuhi ya siku husika na kusubiria kutuma taarifa mchana, muda mchache kabla ya mechi kuanza?

IMEANDIKWA NA BADRU KIMWAGA

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz