KOCHA mkuu wa timu za Taifa za Wanawake Bakari Shime ameonesha kuwa na matumaini makubwa katika kundi iliyopo timu ya Wakubwa ya Twiga Stars kuwania kufuzu fainali ya Afrika kwa wanawake.
Twiga Stars imehamishwa katika ukanda wa Cecafa na kuwekwa kwenye kanda ya Cosafa ambapo imepangwa kucheza mechi ya mzunguko wa kwanza dhindi ya Namibia kati ya Juni 7 hadi 15 mwaka huu nchini Tanzania.
Akizungumza matarajio katika Kundi walilopo Twiga Stars, kocha huyo maarufu kama mchawi mweusi amesema ubora wa timu yake ndio umefanya timu ikahamishwa kanda na itaenda huko kufanya vizuri.
“Ni heshima kubwa kwetu, Caf wameona ubora wetu ndio maana wametuweka kwenye kundi linaloonekana kuwa na kundi bora zaidi hivyo na sisi kwa kuwa ni bora tutaenda kupambana na kufanya vizuri kwani hata ukanda wa Cecafa tulikuwa tunaongoza sisi.
Tumejipanga vizuri na mechi ya kwanza dhidi ya Namibia naamini tutafanya vizuri na watanzania waondoe shaka kuhusu Twiga Stars,” alisema Shime.
Tayari kikosi cha Twiga Stars kipo kambini jijini Dar es Salaam kikijiandaa na mechi za kufuzu Afcon kwa wanawake mwakani nchini Morocco.
Baadhi ya timu zinazopatikana katika ukanda huo wa Cosafa ni Malawi, Zambia, Zimbabwe, Eswatini, Angola, Botswana, Msumbiji na Afrika Kusini.
Ukanda wa Cecafa umebakia kuwa na timu za Uganda, Ethiopia, Kenya, Sudani Kusini, Eritrea, Burundi, Rwanda na Djibouti huku ule wa UNAF ukiwa na timu nne pekee za Algeria, Sudan, Misri na Tunisia.