Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tusitegemee ushindani mechi za Ligi

3c5adc9e0233cd30cf07c611fc7a6998 Tusitegemee ushindani mechi za Ligi

Sat, 29 Aug 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

UHONDO wa michezo ya Ligi Kuu Tanzania Bara unatarajia kuanza kutimua vumbi kuanzia Jumamosi ijayo ya Septemba 6 kwa msimu mpya wa mwaka 2020/2021.

Ligi hiyo itakayoshirikisha timu 18 inaanza kuchezwa baada ya timu kupata mapumziko mafupi yaliyochangiwa na ligi iliyomalizika kusimama kwa takribani miezi mitatu kupisha janga la kidunia la ugonjwa unaosababishwa na virusi vya corona ambao umemaliza maelfu ya watu duniani kote wakiwemo wadau wa soka.

Timu zitakazoshiriki ni Simba, Yanga, Azam FC, Tanzania Prisons, Mbeya City, Namungo FC, KMC, Gwambina FC, Ihefu FC, Polisi Tanzania, JKT Tanzania, Mtibwa Sugar, Mwadui FC, Ruvu Shooting, Dodoma FC, Coastal Union na Biashara United.

Corona ni kama imevuruga ratiba yote kwani timu zimepata mapumziko ya mwezi mmoja tu, ikiwa ni tofauti na misimu ya nyuma ambapo klabu zilikuwa zinapata muda wa kutosha hali iliyokuwa inasababisha klabu shiriki kupata mapumziko mazuri ya kuandaa vikosi vyao kiushindani.

Ndani ya mapumziko hayo, mabenchi ya ufundi kwa kila timu yalikuwa yanatumika kutengeneza muunganiko wa vikosi kwa kuwaunganisha pamoja nyota wapya wanaosajiliwa na wa zamani kuimarisha kwa kujenga ushindani.

Sababu ya mapumziko mafupi, kuna baadhi ya klabu ambazo hazikujipanga kisaikolojia kwa kulinda wachezaji wao tegemeo na kuwaacha kwenda kwenye timu nyingine hazitaweza kutoa ushindani ambao wadau wengi wanatarajia kuuona.

Kwa sababu benchi la ufundi litashindwa kutimiza majukumu yake, ndani ya mapumziko ya mwezi huo mmoja uliotolewa na Shirikisho la Soka, klabu zilikuwa na kazi kubwa ya kutumia nafasi hiyo kusajili wachezaji na nyingine hadi wazo hili limeandikwa hazijamaliza kufanya usajili.

Mfano, timu kama Yanga ambayo kwa asilimia kubwa walipitisha fagio la chuma kwa kuwaacha asilimia kubwa ya wachezaji waliokuwa wanaunda kikosi cha kwanza, licha ya kukamilisha kusajili wachezaji wa ndani bado benchi lao la ufundi halijakamilika kwa kumkosa kocha mkuu, hivyo ni nadra kutegemea kuona ushindani kwenye michezo yao ya awali.

Sio Yanga tu na kuna timu nyingine ambazo zina matatizo zaidi ya hayo ikiwemo kukosa udhamini ambao unaweza kuwa chachu kwa uongozi kuhudumia wachezaji kwa kuwalipa stahiki zao kwa wakati na kuondoa msongo wa mawazo kwa familia zao na kubaki na kazi moja tu ya kucheza soka uwanjani.

Simba ambao ni mabingwa wa mara tatu kwa ligi hiyo, wanaonekana kujipanga vyema kupokea mafanikio kama waliyopata msimu ulioisha kwani hadi sasa wamefanikiwa kulinda wachezaji wao wote tegemeo na kuongeza wengine ambao kimsingi wachagiza ushindani miongoni mwa nyota wa kikosi hicho na kuendelea kuwa tishio kwa klabu zingine.

Kwa maoni yangu, licha ya baadhi ya timu kufanya usajili mkubwa michezo ya kwanza ya ligi hiyo haitakuwa na ushindani mkubwa isipokuwa TFF kama msimamizi wa mchezo wa mpira wa miguu nchini anatakiwa kuzisaidia timu ambazo uchumi wake si imara kwa kuwapa fungu la fedha ambalo litasaidia kupunguza makali kwa baadhi ya changamoto za maandalizi ya timu.

Chanzo: habarileo.co.tz