Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tumepita Afcon 2019

Mon, 25 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Tanzania imeandika historia mpya kwa kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa Afrika (Afcon) baada ya kupita miaka 39.

Tanzania imefuzu fainali za Afrika, baada ya Carpe Verde kutoka suluhu na Lesotho katika mechi nyingine ya mwisho ya Kundi L jana.

Taifa Stars ikicheza soka ya kuvutia mbele ya maelfu ya mashabiki, jana ilipata ushindi mnono wa mabao 3-0 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Mabao ya Simon Msuva, Aggrey Morris na Erasto Nyoni yalitosha kuipa tiketi timu Stars kufuzu fainali za Afrika zilizopangwa kufanyika Misri, Juni mwaka huu.

Tanzania imekuwa timu ya nne katika Jumuiya ya Afrika Mashariki kufuzu fainali hizo ikitanguliwa na Uganda, Burundi na Kenya. Nchi ambazo hazijafuzu ni Rwanda na Sudan Kusini.

Mara ya mwisho Taifa Stars kucheza fainali hizo ilikuwa mwaka 1980 katika zilizofanyika mjini Lagos, Nigeria. Katika mchezo wa jana, Taifa Stars ilicheza kwa kiwango bora kwa takribani dakika zote 90. Kocha Emmanuel Amunike, alipanga kikosi ambacho kilicheza kwa nidhamu katika idara zote huku nahodha Mbwana Samatta anayecheza soka ya kulipwa katika klabu ya KRC Genk ya Ubelgiji, akiwa mwiba kwa mabeki wa Uganda.

Safu ya ushambuliaji ya Taifa Stars ikiongozwa na John Bocco, Samatta na Msuva anayecheza soka la kulipwa katika klabu ya Difaa Al Jadida ya Morocco, ilionyesha soka ya kiwango cha juu.

Pia Nyoni aliyecheza nafasi ya kiungo mkabaji, alionyesha ukomavu katika eneo la katikati sanjari na Mudathir Yahya.

Mabeki wa pembeni Hassan Kessy na Gadiel Michael walifanya kazi nzuri katika eneo la ulinzi wakishirikiana na mabeki wa kati Kelvin Yondani na Aggrey Morris.

Mchezo ulivyokuwa

Dakika ya 21 Msuva alifunga bao la kwanza kwa shuti la mguu wa kulia baada ya kupata pasi ya Bocco na kufumua shuti lililomshinda kipa na nahodha wa Uganda, Dennis Unyango.

Stars nusura ifunge bao dakika ya 45 kwa mpira wa faulo baada ya beki Gadiel Michael kuchezewa madhambi, lakini Samatta alipiga shuti juu.

Timu hiyo ilipata bao la pili dakika ya 49 baada ya beki wa Uganda kushika mpira ndani ya eneo la hatari kutokana na kazi nzuri ya Samatta na mwamuzi aliamuru kupigwa mkwaju wa penalti.

Nyoni alifunga bao hilo kwa mpira wa penalti aliyofunga kwa ustadi. Stars iliendelea kushambulia lango la Uganda na dakika ya 56 Aggrey alifunga bao la tatu kwa kichwa akiunganisha krosi ya Bocco.

Amunike aliyetumia mfumo 4-4-2 alifanya mabadiliko dakika ya 70 kwa kumtoa Farid Mussa na kumuingiza Himid Mao ili kusaidia eneo la kiungo.

Pia alimtoa Bocco dakika ya 81 na kuingia Feisal Salum ‘Fei Toto’ kabla ya kumtoa Msuva na kuingia Thomas Ulimwengu dakika ya 89.

Stars: Aishi Manula, Hassan Kessy, Gadiel Michael, Aggrey Morris, Kelvin Yondani, Erasto Nyoni, Mudathir Yahya, Farid Mussa/Himid Mao, Mbwana Samatta, John Bocco/ Feisal Salum na Simon Msuva/ Thomas Ulimwengu.

Uganda: Dennis Onyango, Awany Timothy, Taddeo Lwanga, Emmanuel Okwi, Kirizestom Ntambi, Nico Wadada, Godfrey Walusimbi, Faruku Miya, Allan Kyambadde, Patrick Kaddu na Moses Waisw.

Wakati huo huo, Rais John Magufuli ameipongeza timu ya Taifa kwa kufuzu kucheza fainali za michuano ya Afrika mwaka 2019 baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Uganda.

Mabomu

Askari wa kutuliza ghasia walipiga mabomu ya machozi kutawanya mamia ya mashabiki baada ya kuvunja geti la upande wa Uwanja wa Uhuru na kuingia ndani ya Uwanja wa Taifa.

Mashabiki hao walivunja geti hilo baada ya uuzwaji wa tiketi kusuasua kabla ya kuchukua uamuzi huo kabla ya polisi kupiga mabomu ya machozi kuwatawanya.

Stars hadi kufuzu

Stars ilianza kampeni ya kuwania tiketi hiyo kwa kutoka sare ya bao 1-1 na Lesotho, ililazimisha suluhu na Uganda, ilifungwa mabao 3-0 na Carpe Verde kabla ya kulipa kisasi kwa kuilaza 2-0 na baadaye ilifungwa 1-0 na Lesotho.

Rekodi za mechi tano kati ya timu hizo zinaonyesha Uganda imeshinda mara mbili na Taifa Stars mara tatu. Mara ya mwisho Taifa Stars kuifunga Uganda ilikuwa mwaka 2007 mjini Dar es Salaam.

Lagos-1980

Kwa mara ya kwanza na mwisho Tanzania ilifuzu Fainali za Afrika mwaka 1980 zilizofanyika mjini Lagos, Nigeria. Katika michuano hiyo iliyoshirikisha timu 12, Nigeria ilitwaa ubingwa.

Taifa Stars ikiwa chini ya Kocha Mkuu Slowmir Work wa Poland akiwa na wasaidizi wake Joel Bendera na Ray Gama ilikata tiketi ya kushiriki fainali hizo ambazo kwa sasa zinashirikisha timu 24.

Mshambuliaji nguli wa zamani wa Pan African na Yanga, Peter Tino aliweka rekodi kwa kufunga bao lililoipeleka Taifa Stars katika fainali hizo katika mchezo uliochezwa Agosti 29, 1976 iliporuana na Zambia ‘KK Eleven’. Katika mchezo wa kwanza Taifa Stars ilishinda bao 1-0, lililofungwa na nyota wa zamani wa Pan Africans na Yanga, Mohammed ‘Adolf’ Rishard kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Timu hizo zilirudiana baada ya wiki mbili mjini Ndola nje kidogo ya Lusaka, Taifa Stars ililazimisha sare ya bao 1-1, licha ya kutanguliwa kufungwa kabla ya Tino kusawazisha zikiwa zimebaki dakika tano kabla ya mpira kumalizika.

Tino alipata pasi ya mwisho kutoka kwa Hussein Ngulungu ambako alipiga kiki kali ya mguu wa kulia iliyomshinda kipa wa Zambia, John Shileshi.

Kikosi cha Taifa Stars kiliundwa na Juma Pondamali, Leopard ‘Tasso’ Mukebezi, Mohammed Kajole/Ahmed Amasha, Salim Amir, Jella Mtagwa, Leodegar Tenga, Hussein Ngulungu, Omari Hussein, Peter Tino, Mohammed Salim na Thuweni Ally.



Chanzo: mwananchi.co.tz