Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tumaini pekee la Watanzania Olimpiki

MICHEZO Wanaridha watakaoiwakilisha Tanzania

Fri, 6 Aug 2021 Chanzo: Mwanaspoti

Mashindano ya Olimpiki yanazidi kushika kasi katika Jiji la Tokyo, Japan huku Tanzania ikiwa bado haijaanza kushuhudia wawakilishi wao wakitupa karata zao.

Tanzania imewakilishwa na wanariadha pekee ambao ni Gabriel Geay, Alphonce Simbu pamoja na Failuna Matanga ambao wote hukimbia Marathoni.

Failuna atakimbia kesho Jumamosi huku Simbu na Geay wao wakikimbia Jumapili ambayo ndio itakuwa siku ya mwisho ya mashindano hayo yaliyoanza kutimua vumbi Julai 23.

GEAY NI NANI?

Alizaliwa Septemba 10, 1996 Arumeru, Arusha ni mwanariadha aliyejikita zaidi kwenye mbio fupi hasa mita 5,000 na muda wake bora anaotamba nao ni dakika 13:20:35 aliuweka Palo Alto CA huko Marekani Mei 5,2017.

Alipata elimu ya msingi katika Shule ya Msingi Endallah na Sekondari Umagi zilizopo Manyara, lakini baada ya kumaliza alijiunga na chuo cha utumishi Singida na kusoma ngazi ya stashahada.

“Mwaka 2014 nilienda Arusha kwa Kocha Thomas (Tlanka) na hapo nikajikita kushiriki mbio za hapa na pale ili mradi nipate fedha za kujikimu na maisha mapya niliyoyachagua,” anasema Geay.

Geay alijikita sana kwenye mbio fupi ambazo zilimpa umaarufu mkubwa tangu mwaka 2014 alipojitosa ndani na nje ya nchi baada ya kupata dili mara kadhaa kwenda kuiwakilisha nchi na hata mialiko yake binafsi.

Moja ya mashindano makubwa ambayo alishiriki ni pamoja ‘African Junior Championships’ yaliyofanyika Addis Ababa, Ethiopia mwaka 2015 na kumaliza nafasi ya nne akitumia muda wa dakika 14:37.”

Pia ameshiriki Mashindano ya mbio za Nyika za Dunia yaliyoifanyika mwaka 2017 nchini Uganda na kumaliza nafasi ya 22. Mwaka 2018 aliibuka kinara Boston 10K alipotumia muda wa dakika 28:24, akatesa tena Utica Boilermaker 15K akitumia dakika 43:36 na baadaye kushinda Crazy’8 8K akitumia dakika 22:43.

Geay ndio bingwa mara mbili wa mashindano ya Bolder Bolder ya 10K baada ya kushinda mwaka 2018 akitumia muda wa dakika 29:14:02 na Mei 28 mwaka huo huo akiibuka kinara kwa kutumia dakika 28:39.

REKODI YA TAIFA

Mapema mwaka huu huko Italia, Generali Milano Marathoni ikiwa marathon yake ya kwanza na alifanikiwa kuweka rekodi ya taifa huku akivunja ile ya Agustino Sulle Oktoba 2018 alipokimbia saa 02:07:45.

Kwa sasa anashika rekodi mbili za taifa hii ya marathoni aliyoiweka mwaka huu ya saa 2:04:55 huko Generali Milano Marathoni na ile ya Kilometa 15 muda wa dakika 42:15+ ya 2017.

SIMBU NDIYE HUYU

Mwaka 2016 katika Olimpiki iliyopita nchini Brazili alikuwa sambamba na kina, Saidi Makula, Fabiano Joseph na Sarah Ramadhan na mwaka mmoja baadaye alinyakua medali ya shaba katika mashindano ya Dunia yaliyofanyika London.

Safari yake ya riadha ilizidi kushika kasi mwaka 2015 pale aliposhiriki mashindano ya Gold Coast Airport Marathon yaliyofanyika nchini Australia alipomaliza kwa kutumia muda wa saa 2:12:01.

mwaka 2014 alishiriki michuano ya Lake Biwa Marathon, iliyofanyika nchini Japan ambayo pia alishiriki Machi 6 mwaka 2015 na kumaliza katika nafasi ya tatu kwa kutumia muda wa saa 2:09:19.

Januari mwaka 2017, Simbu alishinda mbio za Standard Chartered Mumbai Marathon kwa kutumia muda wa 2:09:32 akimshinda Mkenya Joshua Kipkorir aliyemaliza wa pili kwa muda wa 2:09:50, na Mkenya mwenzake Eliud Barngetuny akamaliza wa tatu na muda wa 2:10:39.

Alianza kuupenda mchezo wa riadha tangu akiwa kwao kijiji cha Mampando mkoani Singida alipokuwa akisoma shule ya Msingi ya Mampando aliyohitimu mwaka 2005, kisha kujiunga na Shule ya Sekondari Winning Spirit 2006 iliyopo jijini Arusha.

Licha ya kumaliza kidato cha nne na kupata ufaulu wa daraja la nne alama ya 27 alianza kuwaza kuwa Mwanajeshi, kazi ambayo alikuwa akiipenda zaidi tangu akiwa mdogo na kuanza kuisaka nafasi hiyo kwa muda mrefu bila mafanikio lakini kupitia riadha amefanikiwa kupata kazi hiyo.

Yeye ndiye nahodha wa timu ya Tanzania mjini Tokyo, Japan na atapeperusha bendera ya taifa, Jumapili akiwa sambamba na Geay katika marathoni, ikiwa ni siku moja tu tangu mwanariadha wa kike, Failuna Abdi kuliamsha Agosti 7 kwa upande wa wanawake.

Rekodi zake zimebeba matumaini ya Watanzania kwenye michezo hiyo, licha ya ukweli atakabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa wanariadha wa nchi nyingine kama za Kenya, Ethiopia, Uganda, Burundi na Morocco.

FAILUNA MATANGA

Alizaliwa Oktoba 20, 1992 mkoani Dodoma katika Wilaya ya Kondoa. Mara nyingi alipenda kushiriki mbio fupi kama ilivyo kwa wanariadha wengine wa mbio ndefu huanzia huko. Failuna alipenda kukimbia mbio za mita 10,000 na muda wake bora kwenye mbio hizo ulikuwa dakikia 31:47:37 aliouweka katika mbio za Hengelo FB, zilizofanyika Julai 10, 2017 nchini Uholanzi.

Failuna anakwenda Tokyo ikiwa mara ya kwanza kushiriki Olimpiki baada ya kufanya vyema katika mashindano ya Victoria Marathon mwaka jana huko Afrika Kusini.

Mwanariadha huyu ndiye atakayekuwa wa kwanza kutupa karata kwa timu ya Tanzania nchini Japan, Jumamosi hii atakapokimbia kwenye marathoni kwa wanawake kisha ndipo Simbu na Geay nao watafuata Jumapili ili kuona safari hii kama nchi itavuna kitu gani baada ya kuchemsha Brazili 2016.

Chanzo: Mwanaspoti