Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tulieni tunatoboa

47823 Kagere+pic

Thu, 21 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

SIMBA imerudishwa tena nchini DR Congo na sasa wakipewa kigogo mwingine wa nchi hiyo TP Mazembe katika mechi itakayokuwa na visasi viwili.

Anzia hapa Simba mara ya mwisho kukutana na TP Mazembe ilikuwa ni mwaka 2011 walipokutana katika mechi ya mtoano na Mazembe kushinda nyumbani na ugenini kwa jumla ya 6-3 .

Simba tena ikajikuta ikikutana na AS Vita ya huko na baada ya mechi ya kwanza kupoteza vibaya wekundu hao wakalipa kisasi kibaya cha kuwachapa Vita kwa mabao 2-1 na kuwatupa nje kipigo kilichowauma sana Wakongomani hao.

Caf imewarudisha tena Simba ikikutana na Mazembe, ambapo Wekundu hao watataka kulipa kisasi huku Mazembe nao wakitaka kuendeleza ubabe, lakini pia kuwazibia aibu wapinzani wao.

Ratiba iliyotoka jana Simba itaanzia nyumbani Aprili 6 kisha kurudiana tena na Mazembe safari hii wakielekea jijini Lubumbashi na sio Kinshasa tena wanakotoka Vita.

Simba walivyopasua anga

Simba ilianza harakati zake Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu kwa kukutana na Mbabane Swallows ya e- Swatin katika raundi ya awali na iliibuka na ushindi wa jumla wa mabao 8-1 ikishinda 4-1 nyumbani na kuibuka na mabao 4-0 ugenini, kisha kwenye raundi ya kwanza ikaitupa nje Nkana FC ya Zambia kwa jumla ya mabao 4-3 ikifungwa 2-1 ugenini na kushinda 3-1 nyumbani.

Baada ya hapo ilifuzu hatua ya makundi ilikopangwa kundi D sambamba na Al Ahly, JS Saoura na AS Vita Club ya DR Congo.

Ilianza kwa kuichapa Saoura nyumbani mabao 3-0 na mechi mbili zilizofuata ugenini dhidi ya Vita na Ahly ilichapwa mabao 5-0 kwenye kila mchezo.

Ilijipanga upya na kuibuka na ushindi wa bao 1-0 nyumbani dhidi ya Ahly, ikafungwa ugenini dhidi ya Saoura mabao 2-0 kisha mchezo wa mwisho ikaibugiza Vita kwa mabao 2-1 na kufikisha pointi tisa zilizoivusha kuingia robo fainali.

Hapana shaka mshambuliaji raia wa Rwanda, Meddie Kagere ndiye mchezaji hatari zaidi Simba na aliyechangia kwa kiasi kikubwa wawakilishi hao wa Tanzania kufuzu hatua ya robo fainali, akiwa amefunga mabao sita kwenye mashindano hayo, pia nyota mwingine ni kiungo mshambuliaji Cletous Chama ambaye amefunga mabao matano.

Silaha kubwa kwa Simba kwenye mashindano hayo ni safu yake ya ushambuliaji ambayo imepachika jumla ya mabao 18 kwenye mechi 10 ilizocheza, lakini udhaifu mkubwa walionao ni safu yao ya ulinzi ambayo imekuwa haimudu kukabiliana na washambuliaji wa timu pinzani wenye kasi na kwa kulidhihirisha hilo, imeruhusu nyavu zake kutikiswa mara 16 hadi sasa.

Ni timu ya Tanzania ambayo imekuwa na rekodi nzuri ya ushiriki wa mashindano ya kimataifa kwani, kabla ya mafanikio ya msimu huu, iliwahi kufika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 2003, ilifika fainali ya Kombe la CAF mwaka 1993, pia mwaka 1974 walicheza hatua ya nusu fainali ya klabu bingwa Afrika.

Kwa mujibu wa mtandao wa www.transfermkt.com, Simba ambayo inaendeshwa kwa mfumo wa uwekezaji chini ya mfanyabiashara Mohammed Dewji, thamani ya kikosi chake ni Euro 650,000 (Zaidi ya Sh1.7 bilioni).

Benchi la ufundi la Simba linaongozwa na Mbelgiji Patrick Aussems akisaidiwa na Dennis Kitambi. Kocha wa viungo ni Adel Zrane, makipa wananolewa na Mohammed Muharrami ‘Shilton’, meneja wa timu ni Patrick Rweymamu, daktari ni Yassin Gembe na mtunza vifaa ni Hamis Mtambo.

HAWA NDIO TP Mazembe

Vigogo wa Soka nchini DR Congo TP Mazembe walianza msimu huu kwenye hatua ya mtoano wakiitoa Zesco ya Zambia inayofundishwa na kocha wa zamani wa Yanga, George Lwandamina kisha kutinga hatua ya makundi ikipangwa kundi C na hapo walijikusanyia jumla ya pointi 11.

Msimu huu kuanzia hatua ya mtoano Mazembe ameshinda jumla ya mechi nne akishinda tatu katika hatua ya makundi na moja hatua ya mtoano akiwa hana ushindi ugenini taarifa ambayo Simba wanaweza kuchekelea kutokana na rekodi ya wekundu hao kushinda nyumbani.

Mazembe imepoteza mechi moja pekee msimu huu alipofungwa na CS Constantine ya Tunisia walipochapwa kwa mabao 3-0 huku wakitoa sare tatu.

Ushindi kwa Mazembe ni wanapokuwa nyumbani, msimu huu wakishinda mechi nne na ushindi mkubwa kwao ni pale walipoichapa Club Africain ya Tunisia kwa mabao 8-0 matokeo yaliyomlazimu aliyekuwa kocha wa Watunisia hao Chiheb Ellili kuachia ngazi.

Simba inatakiwa kuwa makini na mastaa saba wa Mazembe wakiongozwa na washambuliaji Muleka Jackson Tresor Mputu na Meshack Eliana beki Mondeko Zatu wote wenye mabao matatu kila mmoja wengine wakiwa kiungo Miche mika na ushindi Chico wenye bao moja kila mmoja wakati mkongwe Raiford Kalaba akitokea benchi katika mechi zake nyingi.

Ikiwa katika ligi ya kwao Mazembe iko pale juu ikiongoza msimamo ikicheza mechi 23 wakishinda 21 wakitoa sare moja na kupoteza moja na kujikusanyia jumla ya pointi 64.

Katika historia yao TP Mazembe wameshachukua kombe hili mara tano huku kikosi chao kilichohesheni mastaa kibao wa Afrika kikiwa na thamani ya Euro 3.9 milioni (zaidi ya Sh10 bilioni).



Chanzo: mwananchi.co.tz