MABOSI wa Simba bado wanaendelea kufanya mchakato wa muundo wa safu yao ya uongozi, lakini mipango mingine ya usajili inaendelea kama kawaida na sasa rada zao zimeelekezwa kwa kiungo wa Yanga, Papy Kabamba Tshishimbi.
Mbali na Tshishimbi ambaye aliingia pia kwenye rada za Azam, Simba nayo inamlia mingo, beki wa Prisons, Salum Kimenya ili kuziba pengo la Shomary Kapombe aliyepo Afrika Kusini kwa sasa akitibiwa jeraha la kifundo cha mguu.
Taarifa kutoka ndani ya Simba zinasema kuwa Kamati ya Usajili ya klabu hiyo, iliyokuwa chini ya Zacharia Hans Poppe inasubiri ripoti ya kocha mkuu Mbelgiji Patrick Aussems ili kujua anataka majembe yapi mapya yatue Msimbazi.
Aussems kabla ya kukutana na mabosi hao wa Simba ili kuwapa ripoti hiyo amefanya kikao na benchi la ufundi ili kukubaliana wachezaji wapya ambao watataka kuwaongeza kabla ya dirisha dogo kufungwa.
Katika kikao hiko cha Aussems na benchi la ufundi kilimalizika na maazimio ya kunasa vifaa vitatu, beki ya kulia, kiungo mkabaji wa kumsaidia Jonas Mkude na James Kotei na straika, japo msisitizo beki na kiungo wapatikane kwanza.
Chanzo makini kutoka klabuni zinasema, awali Mbelgiji alitaka straika tu, lakini kuumia kwa Kapombe kumemfanya aongeze idadi na wanaotajwa kuingia rada za Msimbazi ni Tshishimbi na Kimenya.
“Kabla ya kumsajili huyo beki nafasi hiyo huenda akawa anacheza Erasto Nyoni na katika nafasi yake tunaweza kumtumia Juuko Murshid ila tuna wasiwasi kama ikitokea mmoja akaumia tunaweza kuwa na shida katika eneo hilo ndio maana tunataka beki mpya mwenye uwezo wa kucheza kulia na katikati,” alisema.
“Nicholas Gyan huwa anatumika kama mlinzi wa kulia lakini asilia nafasi yake ni straika.
“Nafasi nyingine ambayo tumekubaliana kufanya usajili ni katika kiungo mkabaji ambaye tunataka ampya na aliyekamilika ili kuja kushindana na Jonas Mkude ambaye tumekuwa tukimtumia muda wote,” alisema.
“Nafasi ya tatu ni straika ambaye alikuwa na shida nae tangu awali lakini alitaka kabla ya kuanza kufanya usajili huu wa mbele lazima tuanze wa wawili ambao wanacheza nyuma na Aussems alisisitiza kwamba hakuna mchezaji ambaye atasajiliwa bila kumuona na kumfatilia zaidi kama kanda zake za video na mambo mengine ya msingi ambayo anayataka,” aliongezea mtoa taarifa huyo ambaye hakutaka jina lake liwekwe wazi kwa sababu za kiusalama.
Aussems alisema alipanga kusajili nyota mmoja katika kipindi hiki cha dirisha dogo la usajili lakini kuumia kwa Kapombe lazima atafute mbadala wa nafasi hiyo ingawa hataweza kumtumia katika mashindano ya Kimaataifa kwa maana usajili wa huko umesha kamilika.
“Kuumia kwa Kapombe kumetoa nafasi kwangu kutafuta beki mzuri ambaye anacheza katika nafasi hiyo kwa lugha rahisi kuna mpango wa kufanya usajili wa beki wa kulia katika kipindi hiki,” alisema Aussems. “Kukosekana kwa Kapombe kutafanya kuwa na mabadiliko katika safu ya ulinzi kwani alikuwa katika wachezaji wa kikosi cha kwanza lakini hata usajili ambao tutafanya pia” aliongezea Aussems.
Mkongomani Kabamba Tshishimbi mkataba wake na klabu hiyo unamalizika mwisho wa msimu huu wakati huo Simba ambao ni miongoni mwa timu zenye nguvu ya pesa katika usajili kwa sasa inahitaji kusajili mcheza wa aina yake.
Mabosi wa Simba huenda wakafika kwa Tshishimbi na kutaka huduma yake kama walivyofanya msimu mmoja uliopita walivyomnasa kiungo fundi Haruna Niyonzima kimya kimya.
Mbali ya Tshishimbi, mabosi hao wa Simba wanashida na mlinzi wa kulia na huenda wakaongeza nguvu ya kutaka kumnasa Salumu Kimenya wa Tanzania Prison ambaye walikuwa wakimsaka misimu miwili iliyopita.
“Hizo taarifa nasikia tu lakini kama wananitaka wakifike kwangu tukae mezani tuzungumze nao mambo ya msingi ninayohitaji,” alisema Kimenya.